Saturday, 5 September 2015
MIKOA SITA YAONYESHA DK. MAGUFULI ANAONGOZA KWA ASILIMIA 85
NA WAANDISHI WETU
UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM), umesema utafiti walioufanya kwa wiki mbili wa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, alikofanya kampeni katika mikoa sita unaonyesha anakubalika kwa asilimia 85.
Umesema hali hiyo inachangiwa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na rekodi nzuri, uadilifu na uchapakazi uliotukuka wa mgombea huyo.
Aidha, umesema uwepo wa upinzani dhaifu na aina ya wagombea ambao wanatumia muda mwingi kujitetea na kujisafisha badala ya kuzungumzia matatizo ya wananchi, inazidi kumtofautisha Dk. Magufuli na wagombea wengine.
Katibu wa Hamasa, Sera, Utafiti na Mawasiliano wa UVCCM, Egla Mamoto, alisema hayo mjini Dar es Salaam, jana.
Alisema chama chochote makini kinapotafuta kushika dola na hasa inapofikia wakati wa uchaguzi mkuu, ni lazima kijiwekee utaratibu wa kujifanyia tathmini ya kilipotoka, kilipo na kinapokwenda.
Egla alisema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, utafiti uliofanywa na Umoja huo unaonyesha Chama kinakubalika kwa asilimia 78, lakini baada ya Dk. Magufuli kuanza kuzunguka kwenye maeneo mbalimbali kukubalika kwa CCM kumeongezeka na kufikia asilimia 85.
Alisema kwenye maeneo ambayo tayari Dk.Magufuli amezunguka ameonyesha uwezo mkubwa kueleza suluhu ya matatizo yanayowakabili wananchi.
“Ukimuangalia Dk. Magufuli unaona kabisa kuwa anachotamka kinaendana na muonekano wake, anaposema anachukia rushwa na ufisadi na kuunda mahakama maalum ya kushughulikia wezi, wala rushwa na wahujumu uchumi unaona kabisa anayoyasema yanatoka moyoni,” alisema.
Alisema hali hiyo inamtofautisha na wagombea wengine ambao rekodi zao za nyuma zinaonyesha kote walikopita walijihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Egla alisema baadhi ya wagombea hivi sasa hawawezi kuzungumzia tena vitendo vya rushwa kutokana na kukumbatia mafisadi.
Alisema mgombea wa CHADEMA, Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, ameanza kuonyesha dalili za kuchoka na kushindwa kufika katika maeneo aliyopangiwa ikiwemo Ludewa na Tunduru ambako wananchi walisubiri wamuone, lakini aliingia mitini.
Hata hivyo, alisema CHADEMA inachagua baadhi ya maeneo ya kufanyia mikutano na badala yake wanakwenda kwenye maeneo ambayo wanayaita muhimu.
Alisema hali hiyo inaonyesha Lowassa na chama chake ni wabaguzi na wamekosa hoja za kuzisimamia baada ya wimbo wa ufisadi kupamba moto kila kona.
Egla aliwataka Watanzania kuungana pamoja kuwakataa mafisadi, wala rushwa wanaoamini wanaweza kuwanunua wananchi kwa sababu wamenunulika na wamekubali kuwa wajasiriamali wa kisiasa.
Alimnukuu aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema ni heshima kwa Mungu kumzomea mwizi na fisadi na kwamba, kuwazomea pekee haitoshi, bali wananchi wawanyime kura.
Egla alisema Umoja huo unawashukuru wananchi kwa namna ambavyo wanajitokeza kwenye mikutano ya kampeni ya Dk. Magufuli na hiyo ni dalili kuwa mgombea huyo anakubalika na makundi yote.
Alisema hadi sasa Dk. Magufuli ametembelea mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe, Katavi, Rukwa na Mtwara ambako alitembelea majimbo yote ya mikoa hiyo.
“Mgombea wetu hadi sasa amefanya mikutano ya hadhara zaidi ya 49, mikutano ya barabarani zaidi 126 ambayo wananchi walimuandalia ili wamsalimie na amezunguka zaidi ya kilomita 5,900,” alisema.
Nathaniel Limu anaripoti kutoka Ikungi, kuwa aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CHADEMA wa kata hiyo mkoani Singida, Hamisi Mazonge, amerejea CCM na kukiomba radhi Chama kwa madai kwamba alifanya kosa kubwa kwenda upinzani.
Mazonge alitaja kosa hilo kuwa ni kukinyang’anya Chama vijiji vya Ikungi, Ighuka, Mbwajiki na Matongo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kuwa chini ya mikono ya chama hicho.
Mazonge alisema katika kipindi hicho alitumia nguvu kubwa kuchangia vitongoji 11 kati ya vitongoji 22 vya Kata ya Ikungi, kuhamia CHADEMA.
"Wana CCM wenzangu kutoka chini ya sakafu ya moyo wangu najutia sana kufanya kosa hili ambalo kwa vyovyote litakuwa limeathiri kwa kiasi kikubwa ustawi wa CCM katika kata yetu," alisema.
Hata hivyo, Mazonge aliahidi kuanzia sasa atakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na atatumia nguvu za ziada kuhakikisha vijiji na vitongoji hivyo vinarejea mikononi mwa CCM.
Naye mkulima na mfugaji wa Kijiji cha Ng’ogousoro katika Kata ya Isuna, Chapachapa Elias, ambaye amerejea CCM baada ya kutofurahishwa na chama chao cha zamani kupokea makapi kutoka CCM na kuyauzia chama, alisema hana mpango wa kugeuka nyuma.
“CHADEMA kilianza kwa na nguvu ya upinzani ya kweli kimebadilika ghafla. Kwa ujumla hakieleweki kabisa,”alisema.
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste wa Kijiji cha Ikio, Ponisian Ghumpi, aliyehamia CCM alisema chama chao cha zamani hakina dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi.
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kutoka wilayani Rombo, Evod Mmanda, alisema anamfahamu Tundu Lissu kwamba uwezo wake wa kuongoza ni mdogo, hivyo kuendelea kumchagua kuwa mbunge ni sawa na kutafuta matatizo.
Kuhusu mgombe wa CCM, Jonathan Njau, alisema anamfahamu kwa miaka 15 kuwa mtu mwelewa na mpenda maendeleo na kuwa, Lissu anamfahamu tangu akiwa kidato cha nne ni msanii na mhamasishaji wa fujo na kamwe wasifanye kosa kumrejesha madarakani tena.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment