Saturday, 5 September 2015

JK AACHA WOSIA SEKTA BINAFSI



NA RACHEL KYALA

Rais Jakaya Kikwete ameitaka sekta binafsi kuwa wazi katika utoaji wa taarifa kuhusu mambo mbalimbali na si kuitaka tu serikali kufanya hivyo, ili kutoa mchango wake katika maendeleo endelevu ya taifa.

Aidha, amesema hivi sasa serikali imepiga hatua nzuri katika uwekaji wazi taarifa zake mbalimbai kwa wananchi na hata nje ya mipaka ya nchi.

Rais Kikwete alisema hayo, jana, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mkutano wa kwanza wa kimataifa wa uwekaji taarifa na takwimu mbalimbali uliohudhuriwa na zaidi ya watu 500 kutoka mataifa 30 duniani zikiwemo nchi washirika wa maendeleo.

“Kama ni misaada sote tunapata kwa wafadhili, msihoji tu serikali imefanya nini, bali ninyi pia mnapaswa kuweka wazi taarifa za mapato, matumizi na michango mbalimbali mliyoitoa, hususani huduma za jamii,” alisema.

Alisema serikali imetunga sheria ya uwekaji wazi taarifa kwa wananchi ambamo imo haki ya wao kuhoji juu ya uwajibikaji na utawala bora, ingawa haijapitishwa na kuwa sheria kamili.

“Ni wakati mgumu kuelekea uchaguzi mkuu, si rahisi kukamilisha ingawa watu wanahoji juu ya kuanzishwa kwa sheria hii. Serikali ya sasa inamaliza muda wake, si rahisi tena kuwahi kuipitisha, lakini serikali ijayo inao wajibu wa kuhakikisha inakamilisha toka kwenye hatua ilipofikia,” alisema.

Kikwete, alitaja faida za uwekaji wazi taarifa kuwa ni kutambua hali halisi ya mambo na kusaidia kutafuta ufumbuzi wa kutatua changamoto zilizopo, ikiwemo kutoa nafasi kwa wananchi kutoa maoni.

Alitoa mfano wa sekta muhimu ya kodi ambayo serikali imekuwa ikiweka wazi kwa wananchi kuanzia kiasi cha mapato yanayokusanywa, matumizi na faida ambapo takwimu za fedha zilizotumiwa na serikali huwekwa wazi bungeni.

Rais alisema changamoto iliyopo katika uwazi ni wananchi kutaka kuwekwa wazi kwa taarifa ambazo ni siri ya serikali, suala ambalo hata mataifa makubwa duniani hayafanyi hivyo ili kutohatarisha usalama wa taifa.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema serikali ina takwimu nyingi zinazoweza kusaidia wananchi kuhoji uwajibikaji wa serikali, kutumika kuchambua, kuchanganua na kutafuta ufumbuzi wa masuala mbalimbali, kubadili mfumo wa utendaji na uwajibikaji.

No comments:

Post a Comment