Saturday, 5 September 2015

SAMIA: BUNDI AKIBADILI MITI HABADILIKI



NA WAANDISHI WETU

MGOMBEA Mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, amesema bundi atabaki kuwa bundi hata akibadilisha miti na kamwe hawezi kuwa jogoo.

 Samia alisema hayo jana baada ya kuzungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, kwenye Viwanja vya Kopa Mwananyamala, Dar es Salaam.

Alisema mabadiliko si lazima yalete maendeleo, lakini maendeleo ndani ya serikali ya awamu ya tano ya CCM yataleta mabadiliko makubwa nchini.

Samia alisema Rais Jakaya Kikwete amefanya kazi kubwa kusafisha mafisadi ndani ya Chama na kilichobakia ni kufanya kazi.

Alisema wapinzani wamekuwa wakidai wanataka kuondoa mfumo ndani ya CCM ambao ni kero, lakini ni vyema wananchi kujua mfumo wa ufisadi ndani ya Chama uliletwa na walioondoka ambao wameondoka nao.

Kwa upande wake, Makonda alisema ana imani kero za ardhi 1,600 zilizoko Kinondoni zitaondolewa na mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, akisaidiwa na Samia kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kupambana na wezi.

Mgombea Mwenza huyo alisisitiza Ilani ya CCM imejitosheleza na wananchi watarajie neema katika miradi mikubwa ya barabara za juu na kuboresha barabara za ndani ili kupunguza msongamano.

Alisema uboreshaji wa sekta ya afya utasaidia kujengewa uwezo zaidi Hospitali ya Mwananyamala.

"Wanaohoji ahadi nyingi za CCM katika miaka mitano ijayo ni vizuri kuelewa kuwa serikali iliyopo madarakani imejiimarisha katika uchumi wa gesi, utalii, kodi na kuwepo miundombinu mizuri ya uchumi hivyo ahadi zilizopo zinatekelezeka,"alisema

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Kinondoni, Idd Azan, alisema kazi kubwa imetekelezwa na serikali na ile ijayo itaboresha miundombinu ya mji ili kukabiliana na mafuriko.

Alisema akipewa tena ridhaa na wakazi wa Kinondoni atashirikiana na Dk. Magufuli kumaliza tatizo la ajira na tayari kila kata imetengewa sh. milioni 100 kuwawezesha wanawake na vijana.

Akizungumza katika Jimbo la Kawe, Samia alisema maendeleo yameshindwa kufikia malengo kutokana na mbunge wake kutoshughulikia kero za wananchi.

Alisema wakiingia madarakani watahakikisha wanashirikiana na viongozi wengine kurudisha hadhi ya jimbo hilo na kuwapatia wananchi mahitaji ya lazima.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, alisema UKAWA wanatafuta laana kutoka kwa Mungu kwa kuwa mabadiliko ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyataka sio ya kutoa uongozi kwa fisadi wala ya ukanda.

Sitta alisema mgombea wa urais wa UKAWA waliona hafai akiwa CCM na alipewa nafasi kubwa katika awamu zote, lakini alipopewa miaka miwili ya uwaziri mkuu akajinufaisha mwenyewe.

"Je tunaweza kuchukua mtu aliyeshindwa uwaziri mkuu kwa kukosa uadilifu tumpe nafasi ya juu ya urais? Tumieni kadi zenu za kupigia kura vizuri ili muweze kumkataa mtu asiye muadilifu," alisema Sitta.

Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Mtera mkoani Dodoma na mjumbe wa Kamati ya Ushindi ya CCM, Livingstone Lusinde, alisema sera za Lowassa ni kumtoa Babu Seya ambaye alifungwa kutokana na kubaka watoto na kuelezea masikitiko yake kuwa kama angembaka mwanawe hadhani kama angemtoa.

No comments:

Post a Comment