Saturday, 5 September 2015
GODBLESS LEMA AKAMATWA NA POLISI KWA MAANDAMANO
NA LILIAN JOEL, ARUSHA
POLISI mkoani Arusha inamshikilia mgombea ubunge wa jimbo la Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema, na wenzake watatu kwa tuhuma za kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali.
Wengine wanaoshikiliwa ni dereva wake Joseph John, Abdul Mohamed na Eliud Jonathan ambaye ni mlinzi.
Inadaiwa Lema alikamatwa baada ya kumaliza mkutano wa uzinduzi wa kampeni katika jimbo hilo uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ngarenaro, juzi.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, alisema Lema alikamatwa saa 12.30 jioni katika eneo la Posta ya Meru baada ya kufanya maandamano haramu yasiyokuwa na kibali alipomaliza mkutano wake.
Alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida mgombea huyo alizima kwa makusudi gari lake lenye namba za usajili T 501 ACH aina ya Ford, eneo la Posta ya Meru na kuwataka wafuasi wake kulisukuma hadi Hoteli ya Kibo Palace iliyopo eneo la Uzunguni.
Kwa mujibu wa Sabas, polisi waliokuwa wakiangalia hali ya usalama katika eneo hilo walimtaka kuwasha gari na kuondoka kwa kuwa wafuasi wake walikuwa wamefunga barabara, lakini alikaidi amri hiyo na kuzidi kuwaomba wafuasi wake anaowaita ‘makamanda’ kuendelea kulisukuma.
“Tulimuonya Lema kuacha kuhamasisha maandamano hayo haramu kwa kuwa hayakuwa na kibali, lakini alikaidi amri ya polisi huku akikataa kuwasha gari lake hilo kwa madai kuwa limeharibika wakati siyo kweli alifanya tu makusudi,” alisema.
Alisema kufuatia hali hiyo watumiaji wengine wa barabara hiyo walikwama kuitumia kwani mgombea huyo pamoja na wafuasi wake walifunga barabara hiyo na shughuli zote kusimama hali iliyowafanya polisi kumkamata na kumpeleka Kituo Kuu cha Polisi cha Arusha.
Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilitoa kibali kwa Lema kufanya mkutano na sio maandamano na walimpa ulinzi wa kutosha, na mkutano wake ulimalizika salama kwa wakati .
Sabas alisema mikutano mingi ya kampeni ya vyama mbalimbali vya siasa inaendelea katika sehemu mbalimbali jiji hapa na hakuna chama chochote ambacho kimeleta vurugu, isipokuwa CHADEMA.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment