Sunday, 6 September 2015

DK. MAGUFULI: WASIOENDELEZA MASHAMBA TUTAWANYANG'ANYA

Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wakazi wa Ifakara wilayani Kilombero kwenye mkutano wa kampeni za CCM ambapo aliwaambia wananchi hao kuwa wakati wake utakuwa wa kiutendaji zaidi ili kufanikisha maendeleo ya haraka kwa nchi na wananchi kwa jumla.

Wananchi wa Ifakara wakimsikiliza Mgombea wa urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa, Ifakara wilayani Kilombero.
Wakazi wa Ifakara wakiwa wamefurika kumsikiliza mgombea wa urais kupitia CCM Dk.John Pombe Magufuli

Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akimtambulisha mgombea ubunge jimbo la Kilombero Ndugu Abubakar Assenga almaarufu kama mtoto wa fundi Cherehani kwenye mkutano wa kampeni za CCM zilizofanyika Ifakara wilayani Kilombero.

 Mgombea wa Urais kupitia CCM Dk. John Pombe Magufuli akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni za CCM uliofanyika Mtimbira


NA SELINA WILSON, KILOMBERO

MGOMBEA urais Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema akipata ridhaa ya wananchi kuwa Rais atawashughulikia vigogo wote waliohodhi mashamba bila kuyaendeleza watanyang'anywa na watagawiwa wafugaji na wakulima.

Amesema anakerwa na inamuuma kuona wakuliwa na wafugaji wanagombana kwa sababu ya ardhi wakati kuna watu wakubwa wamelijilimbikizia mashamba makubwa bila kuyaendeleza.

Dk. Magufuli asema hayo huku kukiwa na kero kubwa inayosababishwa na baadhi ya vigogo kulalamikiwa kuhodhi ardhi katika maeneo mbalimbali nchini na mkoani Morogoro.

Mgombea huyo alisema hayo wakati akihutubia wananchi katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu aliyoifanya katika maeneo mbalimbali ya wilaya za Mahenge, Malinyi na Kilombero mkoani Morogoro.

Akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofurika katika Kata ya Mtimbira wilayani Malinyi, alisema wapo watu waliohodhi ardhi wakati wakulima na wafugaji hawana maeneo ya kufanyia shughuli zao.

"Wapo watu wakubwa wakubwa na wengine wako serikalini wana ekari maelfu, mashamba yamekaa vilevile hawayalimi na wala hawafugii lakini wameyahodhi.

“Nikiapishwa kuwa Rais nitahakikisha watu wakubwa waliohodhi ardhi hawalimi watanyang’anywa mashamba yote ili yatumike kwa ajili ya wakulima na wafugaji," alisema.

Alisema atashughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji na kumaliza tatizo hilo kwa kutenga maeneo kwa kuwa suala ni kupata mahali pa kulima na kufugia.

Dk. Magufuli alisema wakati nchi inapata uhuru mwaka 1961 ukubwa wa ardhi ilikuwa 949,000 na watu walikuwa milioni tisa, lakini sasa wanakaribia milioni 50 ila ardhi bado ni ileile.

“Wakati tunapata uhuru ng'ombe walikuwa milioni 10 leo ni milioni 23 tukiwa wa pili barani Afrika, wakati tunapata uhuru mbuzi hazikufika hata milioni moja sasa ziko ni milioni 14, kondoo milioni sita.

“Kwa hiyo ardhi haijaongezeka watu tumeongezeka na mifugo ineongezeka ndiyo maana katika Ilani tumepanga matumizi bora ya ardhi hivyo tutayapanga vizuri maeneo yetu.

“Nafahamu kuna mgogoro wa pori ambalo walinyoosha mstari kukaingizwa shule na makazi ya watu. Nikiwa rais nitalishughulikia na bahati nzuri nimewahi kukaa wizara ya ardhi,”alisema.

Alisema atashughulikia migogoro kupitia Sheria ya Ardhi namba 4 ya 1999, Sheria ya Ardhi ya Vijiji namba 5 ya 1999, Sheria ya Mipango Miji na Sheria ya Matumizi Bora ya Ardhi ya 2007.

Dk. Alisema sheria hizo zitatumika ili kuhakikisha wakulima na wafugaji wanaishi kwa amani na upendo na kila mmoja afanye biashara atakavyo.

Aliahidi kuanzisha viwanda kwa ajili ya wakulima na wafugaji kusindika mazao ya ufugaji, maziwa, nyama na ngozi na kwamba upande wa wakulima serikali yake itajenga viwanda ili kuhakikisha wakulima wanakoboa mpunga na kuuza nje ya ya nchi.

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli aliwapokea vigogo wawili wa CHADEMA walioamua kujiunga na CCM.

Vigogo hao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Ulanga, Said Rashid ambaye aliwahi kuwa diwani kwa tiketi ya chama hicho, alisema sio chama cha siasa bali SACCOSS ya ambayo ipo kwa ajili ya kuwanufaisha wanachama wake.

Alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na timu yake wamekuwa wakigawana vyema kikanda na hivyo wanachama wengine wasio wakanda kubaki kuwa wapambanaji lakini wanaonufaika ni wengine.

Mwingine ni Evance Tagaya ambaye alikuwa mratibu wa jimbo la Ulanga Magharibi aliyesema ameamua kuhama kutokana na ubabaishaji wa viongozi wakuu wa chama hicho.

Alisema mwaka jana Mbowe alifika Mtimbira wilayani Malinyi na kueleza kwamba CHADEMA imefunga milango ya kupokea makapi kutoka CCM.

Lakini katika uchaguzi wa hivi karibuni, wanachama wameshuhudia Mbowe akifanya biashara ya kukiuza chama kwa Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kuwania urais baada ya kumnyofoa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.

Tagaya alisema pia Mbowe amekuwa akiitumia msemo kwamba asiyefanya kazi na asile  na kusisitiza kwamba hakuna mtu ayakayekatwa kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

“Sasa mpaka sasa hawaelewi  Lowassa amefanya kazi gani ndani ya CHADEMA mpaka atunukiwe kuwa mgombea urais wa chama hicho.Lakini cha kushangaza watu wamekuwa wakikatwa na kuchukuliwa mtu wa tatu kuwa mgombea ubunge au udiwani,”alisema.

Alisema Mbowe alianza kumtaka Dk. Slaa baada ya kumaliza ‘biashara yake’ na Lowassa na baadaye aliendelea kuwakata wagombea ubunge na kuchukua watu aliowaita makapi kutoka CCM.

Aliwataka wananchi wasikubali kurubuniwa na siasa za UKAWA kwa kuwa hakuna siasa, bali ni biashara ndani ya SACCOS na badala yake wamchague Dk. Magufuli awe Rais, wabunge na madiwani wa CCM ili waweze kupata viongozi bora wa kuwaongoza.

“Msikubali kumpa uongozi mtu asiye na chama. Lowassa hana chama ni mgombea wa UKAWA na hiyo sio chama. Dk. Magufuli anatosha kuwa Rais sote tumuunge mkono, tusithubutu kuchagua upinzani,”alisema.

Msafara wa Dk. Magufuli ulilazimika kusimama na kuhutubia makundi makubwa ya wananchi yaliyokuwa yakijitokeza njiani wakati akitokea Mahenge kwenda Malinyi  na baadae kwenda Ifakara Mjini.

Dk. Magufuli alihutubia maeneo mbalimbali ikiwemo  eneo la Ilagua, Lupilo alisema analenga kuunganisha wilaya za mkoa huo kwa barabara za lami na kuunganisha na mikoa jirani ili kufungua fursa za kibiashara.

Apata mapokezi makubwa Ifakara

Umati wa wananchi maelfu ulifurika katika Mkutano wa Kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Tangani eneo la Viwanja Sitini Mjini Ifakara na kumlazimisha Dk. Magufuli kutoa ahadi mbalimbali za kuwaletea maendeleo wananchi.

“Mapokezi haya yamenipa furaha kubwa. Kutukana na mlivyofurika kuja kunipokea nawaahidi kuwafanyia kazi ili kuleta mabadiliko ya kimaendeleo,”alisema.

Alisema ahadi kubwa ni kuhakikisha ujenzi wa daraja kubwa la Mto Kilombero unaogharimu sh. bilioni 53 unakamilika mwakani.

Dk. Magufuli katika maeneo mbali Dk. Magufuli aliwanadi wagombea ubunge wa majimbo ya Kilombero Abubakar Asenga, Ulanga Mashariki, Celina Kombani, Ulanga Magharibi, Dk. Hajji Mponda.

Hata hivyo Celina Kombani, hakuwepo kutokana na kuugua ambapo taarifa iliyotolewa ni kwamba amelazwa na yuko kwenye matibabu.

Kutoka Moshi, Wilium Paul anaripoti kuwa, kundi la vijana wanaodhaniwa kuwa CHADEMA wamefanya hujuma ya kuharibu na kuchana baadhi ya picha za Dk. Magufuli katika maeneo mbalimbali mjini humo.

Aidha, imebainika kuwa baadhi ya picha hizo zimechafuliwa na kuchanwa chanwa, huku nyingine zikiwekewa alama mbalimbali za ajabu.

Baadhi ya wakazi wa mji humo walisema wapo vijana wamekuwa wakitumika vibaya kuchana picha na machapisho ya wagombea.

Katibu wa CCM mkoani Kilimanjaro, Deogratius Rutta, alisema wafuasi wa  vyama vya upinzani wameanza siasa chafu na kukisababishia hasara Chama.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoani, Fulgence Ngonyani, alisema hajapata taarifa za malalamiko ya kuwepo kwa watu waliofanya kitendo hicho, lakini alionya dhidi ya yeyote atakayekamatwa kuhusika na suala hilo kuwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments:

Post a Comment