Sunday, 6 September 2015
DK SHEIN: ONDOENI HOFU TUTASHINDA
NA MWANDISHI WETU
MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein, amerejesha fomu ya kugombea nafasi hiyo na kuwahakikishia wanachama na wapenzi wa CCM kwamba Chama kimejiandaa na kujidhatiti kushinda uchaguzi.
Dk. Shein alirejesha fomu hizo jana katika Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na kusema Chama kimejiandaa na kiko tayari kwa uchaguzi.
Mgombea huyo akizungumza katika Ofisi Kuu ya Chama iliyoko Kisiwandui akitokea ofisi za muda za ZEC kwenye Hoteli ya Bwawani, alisema CCM ni Chama chenye dhamira ya kuwatumikia Watanzania. Dk. Shein pia ni Rais wa Zanzibar.
“Sisi tuko tayari kwa uchaguzi, tumekamilika katika kila idara. Tutaanza kwa gia kubwa na hatufanyi utani lazima (wapinzani) waisome namba,”alisema.
Akizungumzia mchakato mzima wa kujaza na kurejesha fomu ZEC, alisema haikuwa kazi rahisi kwa kuwa nyaraka za tume ni nyingi na zilihitaji umakini mkubwa.
“Ninawashukuru viongozi na wanachama wa Chama chetu katika ofisi zetu zote Unguja na Pemba pamoja na wananchi wengine kwa kunisaidia kufanikisha mchakato huu na hatimaye leo (jana) nimeweza kurejesha fomu hizo,” alisema.
Baada ya kuwasili katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui akitokea Hoteli ya Bwawani, alisalimiana na wanachama na wapenzi wa CCM pamoja na wananchi waliokuwa wakimsubiri.
Dk. Shein alisema uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, utakuwa huru na wa haki.
Akiwa katika Hoteli ya Bwawani baada ya kurejesha fomu, Shein alisema ZEC ni huru na anatarajia itaendelea kusimamia haki katika uchaguzi kama ambavyo imekuwa ikifanya siku za nyuma.
Dk. Shein alisema kutokana na hali hiyo, yapo matumaini makubwa kuwa wananchi wa Zanzibar watatumia vyema haki yao ya kupiga kura kuwachagua viongozi wanaowataka.
Kuhusu ujazaji wa fomu, aliuthibitishia uongozi wa ZEC na makamishna wake kuwa alizijaza kwa kufuata maelekezo yote aliyopewa pamoja na maelezo mengine yaliyomo katika fomu hizo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment