Mgombea mwenza wa urais Samia Suluhu Hassan akihutubia umati wa wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Majohe, Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam |
Wananchi wakinyoosha mikono juu kufurahia hotuba iliyotolewa na mgombea mwenza wa urais, Samia Suluhu Hassan |
Mgombea ubunge wa jimbo la Ukonga, Jerry Silaa akiomba kura kwa wananchi wakati wa mkutano huo |
Umati wa wananchi uliofurika kwenye mkutano huo uliofanyika Majohe, Ukonga, Dar es Salaam. |
Baadhi ya wasanii wa filamu na muziki wa kizazi kipya wakiwa kwenye mkutano huo |
Msanii maarufu wa filamu nchini Wema Sepetu akisalimiana na mgombea mwenza wa urais, Samia Suluhu Hassan |
Mgombea mwenza wa urais Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga, Jerry Silaa |
Mgombea ubunge wa jimbo la Segerea akiomba kura kwa wananchi wakati wa mkutano huo |
EPSON LUHWAGO NA MARIAM MZIWANDA
TATIZO la mafuriko katika Jiji la Dar es Salaam, litapatiwa
ufumbuzi wa kudumu kutokana na kuwepo kwa mpango kamambe ulioandaliwa wa
kuzibua mitaro kuelekea baharini.
Sambamba na mpango huo, serikali ijayo ya CCM itajenga
hospitali kubwa Kibamba, ili kutoa huduma bora. Pia inatarajia kupanua
Hospitali ya Palestina iliyoko Sinza, ambayo itakuwa ya wilaya mpya ya Ubungo.
Hayo yalisemwa juzi na mgombea mwenza wa urais wa CCM, Samia
Suluhu Hassan, katika mikutano ya kampeni iliyofanyika Mbezi Mwisho na
Mburahati Barafu, jijini Dar es Salaam.
Alisema jiji la Dar es Salaam limekuwa likikumbwa na
mafuriko mara kwa mara kutokana na kuziba kwa mitaro ya maji kwenye maeneo
mbalimbali, hivyo serikali imeliona na italifanyia kazi.
“Wananchi wamekuwa wakiathiriwa na mafuriko mara kwa mara
ambayo husababisha pia magonjwa ya mlipuko. Sasa kuna mpango kamambe wa kuzibua
mitaro yote na kuelekeza maji kwenye Mto Ng’ombe hadi baharini.
Pia mitaro yote itazibuliwa kwa ajili ya kupeleka maji
kwenye mito na kuielekeza baharini,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Dar es Salaam ni jiji la pili kwa ukubwa
Afrika kwa maendeleo, lakini sifa yake kubwa ni uchafu. Tutalisimamia kwa
karibu suala hili na kuhakikisha uchafu ndani ya jiji hili unabaki historia,”
alisema.
Kuhusu afya, alisema serikali ijayo ya CCM itajenga
hospitali kubwa na ya kisasa ambayo itatoa huduma kwa saa 24 na kupunguza adha
kwa wakazi wengi wa jimbo la Kibamba kwenda kufuata huduma kwenye hospitali ya
Tumbi, Kibaha.
Alisema hospitali hiyo kubwa na kisasa itawezesha watu
kupata huduma bora na za uhakika pindi itakapokamilika na pia kupunguza adha za
kufuata huduma Tumbi na hata Muhimbili.
“Ndugu zangu, nawahakikishia kuwa hospitali hii kubwa na ya
kisasa itajengwa. Tuchagueni ili tuingie madarakani tuifanye kazi hii,”alisema
katika mkutano uliofanyika Mbezi Mwisho.
Naye mgombea ubunge wa jimbo la Kibamba, kupitia CCM, Dk.
Fenella Mukangara, alisema kuna mpango pia wa kujenga vituo vitatu vya afya ambavyo
vitachangia kutoa huduma na kupunguza tatizo hilo.
Akiwa katika mkutano wa jimbo la Ubungo, eneo la Mburahati, Samia alisema serikali ya awamu ya
tano ya CCM inatarajia kupanua hospitali ya Sinza Palestina ili kuwa ya ngazi
ya wilaya, baada ya kuanzishwa kwa wilaya mpya ya Ubungo.
Sambamba na hilo, alisema vituo vya afya vilivyoko katika
wilaya nzima ya ubungo vitaboreshwa kuhakikisha huduma za uhakika zinapatikana
kwa saa 24.
“Kituo cha afya cha Mburahati kinafanyiwa ukarabati mkubwa
kwa ushirikiano baina ya Manispaa ya Kinondoni na JICA (Shirika la Kimataifa la
Maendeleo la Japan). Kazi hii ikikamilika huduma bora na za kisasa
zitapatikana,” alisema.
AWAZODOA
WAPINZANI
Samia alisema wapinzani wamekuwa wakidai kuwa CCM haijafanya
chochote wakati wanapita kwenye barabara za lami za CCM na kupata huduma ambazo
zimepatikana kutokana na utekelezaji wa Ilani
za Uchaguzi za CCM.
“Hawa wanaosema hatujafanya kitu tunawashangaa sana. Magari
yao yanapita kwenye barabara zilizojengwa na CCM. Wanatibiwa kwenye hospitali
zilizo chini ya serikali za CCM. Wao wamefanya nini? Wapuuzeni watu
hawa,”alisema.
Akiwa katika jimbo la Kibamba, alimtumia salamu mgombea wa
CHADEMA, John Mnyika, kuwa ajiandae kufungasha virago kwa sababu hana chake
tena.
Alisema Mnyika atapigwa na mwanamke (Dk. Fenella) kwenye
uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, kwa kuwa CCM imejipanga
kuwaletea wananchi wa Kibamba maendeleo.
Kuhusu barabara, Samia alisema Ilani ya Uchaguzi wa CCM
imeweka bayana mpango wa kujenga barabara kadhaa kwa kiwango cha lami, ili
kurahisisha usafiri na kupunguza msongamano.
Kwa mujibu wa Ilani, baadhi ya barabara kuwa ni
Mbezi-Malamba Mawili- Kinyerezi hadi Banana (likomita 14); Tegeta Kibaoni-
Wazo- Goba- Mbezi Mwisho (kilomita 20); Tangi Bovu hadi Goba (kilomita 5.2 kati
ya tisa); Kimara Baruti- Msewe- Changanyikeni (kilomita 2.6); na Kimara
Kilungule hadi External (kilomita 8.8 kati ya tisa).
Zingine ni Kigogo round abaout- Bonde la Msimbazi- kona ya
Twiga/Msimbazi (kilomita 0.5 kati ya 2.7); Tabata dampo hadi Kigogo (kilimota
1.6 kati ya kilomita 2.25); na Kibamba- Mlonganzila (kilomita nane kati ya
12).
No comments:
Post a Comment