Monday, 7 September 2015

JK: HAWATUWEZI; ASEMA HANA SHAKA NA MAGUFULI; MAKAMBA AMTAPIKIA LOWASSA




 Mwenyekiti wa CCM Taifa,Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia wakazi wa Morogoro mjini ambapo aliwaambia wananchi hao kuwa mchakato wa kumpata Mgombea wa Urais ulikuwa wa haki na kila mjumbe alipiga kura.
DK. Magufuli akihutubia wananchi wakati wa mkutano huo
Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwahutubia wananchi wakati wa mkutano huo

Na Mwandishi Metu, Morogoro
MWENYEKITI wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, amesema hana shaka akistaafu akimkabidhi nchi Dk. John Magufuli, anakwenda kulala usingizi.
Dk. Magufuli ana sifa zote za kutosha kuwa Rais ana mapenzi na nchi itakuwa mikono salama, ana mapenzi makubwa na nchi yake, ana uchungu pale anapoona mambo hayaendi vizuri.
Amemtaka Dk. Magufuli asiwe na hofu mambo safi, atashinda uchaguzi mkuu Oktoba 25.
“Tulifanya uamuzi wa makini. Tuliwajadili wagombea kila mmoja kwa sifa yake. Kwenye NEC, tulichukua muda mrefu kujadili, kama kuna watu wengi walipata nafasi ya kuzungumza kwenye NEC ni watu waliomuunga mkono Lowassa walizungumza na kumpigania lakini tulikubaliana wote tukapiga kura na Lowassa alipiga kura,” alisema.
Rais Kikwete alisema hayo jana alipohutubia maelfu ya wakazi wa Mji wa Morogoro waliofurika kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika katika uwanja wa Jamhuri mjini hapa.
Aliwataka Watanzania wamuombee Dk. Magufuli afya njema ili aendeshe kampeni salama kampeni za uchaguzi na Oktoba 25, mwaka huu, wananchi hapana kubabaika wamchague Dk. Magufuli awe Rais.
Rais Kikwete alisemaanakubalika na uhakika baada ya Oktoba 25, mwaka huu, wanaojiita UKAWA watakuwa ukiwa, baada ya Dk. Magufuli kushinda uchaguzi na kuingia Ikulu.
Alisema hakupanga kuzungumza siku hiyo, kwa kuwa alikuwa Morogoro kwa ajili ya Mkutano wa Mkakati wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na aliposikia mgombea mwenyewe anakuja aliamua kuahirisha na baadae aliendelea na mkutano wake.

Mzee Makamba awalipua Lowassa
Jana, kwa mara ya kwanza Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Luteni Mstaafu Yusuf Makamba, alikuwa kivutio cha aina yake pale alipoanza kushusha makombora dhidi ya Lowassa.
Makamba, ambaye alikuwa akitajwa kuwa swahiba wa Lowassa, alisema mgombea huyo wa CHADEMA ni mtu mwenye tamaa ya madaraka na kwamba, hafai kabisa kuwa Rais.
Alisema katika uangozi wake alitumia madaraka yake vibaya kwa kujilimbikizia mali ikiwemo kupora ardhi, zikiwemo Ranchi za Taifa huku akiwaacha wananchi wanahangaika na migogoro kwa kukosa ardhi.
Makamba alitoboa siri ya Lowassa na dhamira yake ya kuondoka CCM mwaka 1995, enzi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipozuiwa kuwania urais.
“Kipindi kile kwenye mchujo hakuingia kwenye tano bora. Tulipoingia kwenye kikao cha NEC, nilihoji kwa nini jina la Lowasa halipo? Nilijibiwa wewe ni mtoto mdogo hujui kitu, Lowassa ni kijana mdogo na utajiri mkubwa kuliko,’’ alisema.
Makamba alisema alitaka Lowassa aitwe, Mwalimu Nyerere alisema kwamba akiitwa Makamba ndio amuulize swali hilo. “Bwana mkubwa hukuteuliwa kugombea urais kwa sababu ni kijana mdogo na una utajiri mkubwa, utueleze umezipataje,”
Makamba alisema Lowassa kwamba ana mali kama ilivyo kwa watu wengine, lakini sio nyingi. “Alikiri kwamba anazo lakini sio nyingi kama wanavyosema watu,” alisema.
Alisema alipotoka kwenye kikao Lowassa alimwandikia ujumbe kwenye karatasi na kumshukuru kwa kumtetea katika kikao hicho.
“Aliniuliza pamoja na kuniteteta unaona kuna sababu ya mimi ya kubaki CCM, nikamjibu baki huku kwani unaruka matope unakanyaga mavi…akabaki, lakini baadaye aliteuliwa Waziri Mkuu mliona yaliyotokea,’’ alisema.
Makamba alisema kutokana na kitendo hicho, walitegemea angejirekebisha na kujisafisha ila hakufanya hivyo.
Alisema anashangazwa na kauli ya Lowassa kudai anakerwa na umasikini na anataka kuiendesha nchi mchakamchaka.
“Umasikini anaosema ni umaskini wananchi, jambo ambalo si sahihi kwani amejilimbikizia ardhi kubwa hapa Morogoro huku wakulima na wafugaji wakikosa sehemu za kulima na kufuga.
Makamba alisema kuwa Lowassa amepora Ranchi ya Mkata na kumpa rafiki yake, Ranchi ya Mzeri – Handeni, ambako wananchi hawana maeneo ya kufugia na pia amechukua Ranchi ya Mteri na ana ng’ombe ambao anawatembelea kwa helkopta.
“Nilikuwa Katibu Mtendaji wa CCM Monduli, kule amechukua ranchi ya Leteni…wafugaji wanakosa maeneo ya kufugia na bado anadai anachukia umasikini. Kwenye shule yumo, kwenye bodaboda yumo sasa anachukiaje umasikini wakati kila kitu amekichukua,” alisema Makamba huku akishangiliwa na umati na kuongeza: “Lowassa amefanya hayo akiwa waziri, je akipewa urais si ndio atachukua kila kitu.”
Kuhusu tuhuma za Lowassa kufanya usanii kwa lengo la kuwahaada watanzania kwa kupanda daladala, Mzee Makamba, alisema wakati yeye akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam miaka 10 iliyopita, Lowassa akiwa Waziri Mkuu, alishindwa kufanya ziara mkoani humo na badala yake alitembelea na kukagua Barabara ya Shekilango tu.
Mzee Makamba, pia alimgeukia Sumaye, akisema Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alimvumilia katika kipindi chote cha uongozi wake kwa kuwa alikuwa hafai.
“Eti kaacha kusoma siku zote, anakuja kusoma baada ya kustaafu Uwaziri Mkuu wakati anataka kugombea urais,’’ alisema Makamba.
Alisema Sumaye amechukua ekari 300 za ardhi katika eneo la Magole wilayani Mvomero na uamuzi huo ndio chanzo cha kukithiri kwa migogoro ya ardhi mkoani Morogoro.
“CCM haihitaji wezi kabisa…Sumaye ni mnyonyaji asiye na aibu,’’ alisisitiza.
Aidha, Makamba aliwataka wanasiasa hao ambao wamekwenda upinzani kusaka madaraka baada ya kukatwa kutokana na kutokuwa waadilifu, wajitokeza kukanusha kama wamesingiziwa.
Alionya kuwa bado ana nondo nyingi kwa ajili ya kuwapasha Lowassa na Sumaye na kwamba, watanzania wawaogope.
Alitumia fursa hiyo kumpongeza, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kwa kujiengua ndani ya kundi la Ukawa kutokana na kuwalinda mafisadi.

Dk. Magufuli: Ahadi ya kurudisha mashamba pale pale
Akizungumza na wananchi, Dk. Magufuli alisema migogoro ya ardhi inaongezeka kwa sababu ya mafisadi kuchukua sehemu kubwa ya ardhi na kuyafanya mapori bila kuayaendeleza.
Alisema akiwa Rais atafuta hati zote za watu waliohodhi ardhi wakiwemo vigogo waliwahi kushika nyadhifa za juu serikalini na hilo halitakuwa na mjadala.
Kuhusu ujenzi wa miundombinu, Dk. Magufuli alisema kuanzia mwakani serikali yake itajenga barabara ya lami ya njia sita kutoka Dar es Salaam/Chalinze/Morogoro.
Alisema tayari wataalamu wameanza kufanya usanifu wa barabara hiyo ili mwakani kazi ianze pamoja na kuahidi ujenzi wa barabara ya Bigwa hadi Matombo yenye kilometa 78 ili kuhakikisha wananchi wanafanya kazi zao kwa ufanisi.
0000

No comments:

Post a Comment