UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umesema muda wa kuoneana haya
ndani ya Chama sasa umekwisha na kwamba viongozi wote wasaliti wanapaswa
kuwekwa hadharani.
Umesema wana-CCM wanatambua kuwepo kwa wenzao, wakiwemo waliowahi kushika nafasi za juu za Chama na serikali, ambao wamekuwa wakikihujumu Chama na kukisababishia kufanya vibaya kwenye baadhi ya uchaguzi.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alitoa kauli hiyo jana, alipongumza na viongzi wa UVCCM na CCM, katika ukumbi wa CCM kata ya Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, ambapo alisema vijana watasimama imara kuhakikisha wanalinda mapinduzi ya mwaka 1964.
Kwa mujibu wa Shaka, umefika wakati kwa wana-CCM kukilinda Chama kwa hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoendelea kuwaficha wanachama wenye sumu ndani ya CCM, ambao kwa muda mrefu wameendelea kukihujumu.
"Wakati wa kuoneana aibu au muhali umepita, hatuwezi tena kuendelea kuwachekea maadui wapya hatari, wakijificha ndani ya Chama chetu huku wakituhujumu, inasikitisha kuona waliofaidika na matunda ya mapinduzi ni washirika wa vibaraka na mabeberu wapya, " alisema.
Kwa mujibu wa Shaka, viongozi na wanachama wa CCM wanapaswa kutambua hata ndani ya Chama wako baadhi ya viongozi wastaafu wa kisiasa ambao bila aibu wameamua kushirikiana na wapinga mapinduzi ili kuyasaliti, kuyafuja na ikibidi hata wavunje misingi yake.
Akizungumzia uchaguzi mkuu uliofutwa kisheria na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), alisema iwapo mechi haijamalizika kutokana aidha, kuingia giza au mvua kubwa kunyesha kabla ya dakika 90 na mwamuzi kuamuru mchezo urudiwe, timu yenye ubavu na stamina haiwezi kutia mpira kwapani, isipokuwa itajipanga kucheza bila ulalamishi.
Katibu mkuu huyo alisema baadhi ya vyama vya siasa, ambavyo vimeanza kugwaya na kudai uchaguzi ukirudiwa havitashiriki, ni rahisi kwao kuiaminisha jamii kwamba ni vyama vya ubabaishaji, visivyojiamini na pia vinapenda hadaa na hila ili kupata ushindi na madaraka ya dezo.
"Thamani ya utu na uhuru huu uliotokanana na mapinduzi yaliofanywa na wazee wetu, anapotokea jambazi mmoja mkorofi kutaka kuubomoa ukuta uliohifadhi hazina ya urithi wetu, tusimuonee muhali, tukabiliane naye haraka," alieleza shaka huku akipigiwa makofi.
Alisema kuna kila sababu ya vijana wa CCM kujifunza kutokana na kasoro, hitilafu au jambo lolote dhaifu, ambalo limetokea katika uchaguzi uliofutwa na sasa kutorudia makosa.
"Tumejipima vya kutosha sasa tumejijua, tumejitambua
na hatutakubali kumvumilia yeyote asiye na nia njema. Ndani
ya jahazi la safari yetu atakayetukoroga , tutamdhibiti kisha
tutamtosa mkondoni bila kumuhurumia.
“Huu si wakati wa kuendelea kucheka na nyani kwani kufanya
hivyo tutavuna mabua. Tunawataka viongozi ambao wanajijua kwamba tunawajua
wanatuhujumu, waache mara moja na wakishindwa kufanya hivyo tutawataja
hadharani,” alisema.
Alisema si busara, hekima wala fikra njema kwa kiongozi mmoja
akawa anafikiri anaweza kufanya kila kitu peke yake bila msaada wa wenzake,
hivyo amewataka vijana wa UVCCM kuhakikisha wanafanya kazi za kisiasa kwa
ushirikiano kama wafanyavyo mchwa, nyuki au siafu.
Shaka yuko visiwani
Zanzibar katika ziara ya kutembelea mikoa yote kumi ya kichama, Unguja na Pemba,
akikutana na makundi ya vijana, wazee na wanawake katika mkutano ya ndani.
No comments:
Post a Comment