Monday, 16 November 2015

NDUGAI, MWINYI , DK. TULIA WAPENYA KIKWAZO CHA KWANZA CHA KUWANIA USPIKA




 HATIMAYE Kamati Kuu ya CCM, imeteua majina ya Job Ndugai, Dk. Tulia Akson na Abdullah Mwinyi, kuwa wagombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Majina hayo ndiyo yatakayopelekwa kwenye kikao cha wabunge wa CCM kwa ajili ya kupigiwa kura na kupatikana kwa jina moja la mgombea wa nafasi hiyo atayepambana na wagombea wa vyama vingine.

Nafasi hiyo ilikuwa ikiwaniwa na makada 21 wa CCM, akiwemo aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye alikuwa akiwania nafasi hiyo kwa mara nyingine tena.

Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alitangaza majina hayo jana, nje ya Ukumbi wa White House, muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu.

Alisema majina hayo yatapigiwa kura katika kamati ya wabunge wa CCM leo saa nne asubuhi na baadaye jina la mshindi litawasilishwa Ofisi ya Bunge kwa hatua zaidi.

Kati ya wana-CCM hao 21 waliogombea, Balozi Costa Mahalu, hakuweza kurudisha fomu na hivyo kufanya idadi ya wagombea waliojadiliwa na CC kubaki 20.

Mbali ya Ndugai, ambaye ni Naibu Spika wa Bunge lililopita, Dk. Tulia (Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali) na Abdullah Mwinyi, ambaye ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, wengine ni Rita Mlaki, George Nangale, Dk. Medard Kalemani na Julius Pawatila.

Pia, wamo Agnes Makune, Mwalika Watson, Dk. Kalokola Muzamil, Dk. Didas Masaburi, Simon Rubugu, Veraikunda Urio, Gosbert Blandes, Banda Sonoko na Leonce Mulenda.

NAFASI YA UNAIBU SPIKA

“Kwa bahati mbaya jana kwa makosa tulieleza ratiba ambayo ilikuwa inazungumza kwamba suala la Naibu Spika lingeshughulikiwa leo na kamati kuu. Kwa mujibu wa kanuni za CCM, suala la Naibu Spika halishughulikiwi na kamati kuu,” alisema.

Alifafanua kuwa suala la Naibu Spika linashughulikiwa na kamati ya wabunge wa CCM.

“Kwa mujibu wa kanuni ya kamati ya wabunge wote wa CCM, toleo la 4, 2011, ibara ya 57, inasema mwanachama wa CCM anayetaka kugombea nafasi ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, atajaza fomu maalumu ya maombi na kuiwasilisha kwa katibu wa kamati ya wabunge wote wa CCM.

“Kwa muda uliowekwa na ada ya fomu itakuwa shilingi 100,000, ambazo zitalipwa wakati mgombea anarudisha fomu kwa katibu wa kamati,” alisema Nape.

Aidha, alifafanua kuwa suala la mgombea unaibu spika ni suala ambalo linamalizwa na kamati ya wabunge wa CCM.

Alisema kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya kamati ya wabunge wa CCM, wanaotaka kugombea nafasi hiyo watachukua fomu kuanzia leo na kurudisha kesho,  kabla ya saa 10 jioni.

Katibu huyo alisema, uchaguzi utafanywa na wabunge wa CCM, Novemba 17 kwa kumpata mgombea mmoja atayegombea nafasi ya unaibu wa spika kupitia tiketi ya CCM.

No comments:

Post a Comment