MWENYEKITI mstaafu wa CCM, John Malecela akihutubia mkutano wa kampeni wa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, uliofanyika jana mjini Makambako, Iringa |
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli akihutubia mkutano wa kampeni Mafinga mkoani Iringa |
Dk.Magufuli akionyesha kadi ya kada wa CHADEMA, aliyejiondoa katika chama hicho na kujiunga na CCM |
MFUASI wa CCM akionyesha bango lenye picha ya mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli |
Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi, Abdalla Bulembo akihutubia wakazi wa Mabarali |
Mgombea ubunge wa CCM katika jimbo la Mafinga, Costa Chumi akiomba kura kwa wananchi |
NA CHARLES MGANGA, MBARALI
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema mgogoro wa mwekezaji wa shamba la Kapunga na wananchi, ataumaliza kwa kurudisha ekari 1,800.
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema mgogoro wa mwekezaji wa shamba la Kapunga na wananchi, ataumaliza kwa kurudisha ekari 1,800.
Dk. Magufuli amesema mwekezaji aliomba ekari 5,000, lakini alipewa 6,800, hivyo kiasi hicho kiliongozewa kinyume na utaratibu na kwamba kitarejeshwa.
Akizungumza na wananchi wa Igulusi, mgombea huyo urais wa CCM, alisema ekari hizo zilizozidi zingeweza kurejeshwa haraka, lakini aliyekuwa mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi, alikuwa kikwazo.
Alisema Kilufi hakuwa akifuatilia kwa ukaribu na ushirikiano wake haukuwa mzuri, jambo lililosababisha jambo hilo lichelewe.
"Mbunge wenu Kilufi ndiye alikuwa akikwamisha.
Akiambiwa alete nyaraka fulani, hatekelezi. Lakini nawaomba mnichague niweze
kulimaliza kwa kurudisha ekari hizo 1,800," alisema Dk Magufuli.
Alisema akiwa rais, atatumia sheria ya ardhi namba 5 ya mwaka 1999, kwa ajili ya kurudisha ardhi hiyo.
Alisema mashamba hayo yakirudishwa, yatagawanywa
kwa wananchi wote bila kujali itikadi za vyama.
"Maendeleo kwa kawaida hayana vyama, shamba
likirudi litawanufaisha wote," alisema Magufuli.
Dk. Magufuli alisema mchakato wa kurejesha ekari
hizo umeanza na unaweza kukamilika kabla hajawa rais.
Katika kuhakikisha suala hilo amedhamiria
kulimaliza, alimtaka mgombea ubunge jimbo la Mbarali, Haroun Mohammed,
kumpelekea nyaraka zote zinazohusu mgogoro huo kwa utekelezaji.
Alisema asingependa likwame kama ambavyo Kilufi amesababisha.
Alipokuwa akitokea uwanja wa ndege wa Songwe, Dk. Magufuli alisimama maeneo ya Mwanjelwa, Soweto, Uyole, Kongolo, Igurusi na Chimala ambako aliwaomba wamchague awe rais kwa kura nyingi.
Pia, aliwataka kuwachagua wabunge na madiwani wa
CCM kwa ajili ya maendeleo.
Akiwa Soko Mwanjelwa, Dk. Magufuli alisema lina hadhi kubwa, lakini wananchi ndiyo wanaochelewesha maendeleo.
"Wakati mwingine ninyi wananchi wa Mbeya
ndiyo mnachelewesha wenyewe maendeleo ya jiji hili kwa kuchagua wapinzani.
" Mmekuwa mkichagua wabunge wa upinzani, hiyo imekuwa sababu kubwa ya kuwa hivi," alisema Dk. Magufuli.
Aliwataka wananchi wa Mbeya Mjini wampigie kura Sambwe Shitambala awe mbunge wa jimbo hilo.
Mbunge aliyemaliza muda wake ni Joseph Mbilinyi wa CHADEMA.
Dk. Magufuli alisema anataka kuifanya Mbeya yenye
mabadiliko, ambapo aliibua kionjo kingine kwa kusema M4C ni Mbeya For Change
kama alivyoanza kuitafsiri awali, M4C ni Magufuli For Change.
"Naipenda Mbeya, naipenda Tanzania, nataka nifanye kazi. Naombeni kura zenu niwatumikie kwa pamoja," alisema Dk. Magufuli.
Alisema atahakikisha hata kero za maji na zingine,
zitakwisha.
Kabla ya kuzungumza na wananchi wa Rujewa, wilaya ya Mbarali, Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu, John Malecela, aliwaambia wananchi hao wasifanye makosa Oktoba 25, mwaka huu.
Malecela alirusha dongo kwa wapinzani kwamba UKAWA
imegawanyika makundi mawili.
Malecela alisema kundi la kwanza ni lile ambalo tuliliruhusu kuanzisha Chama, lakini jingine ni lile la waasi waliohama kutoka CCM na kujiunga upinzani.
Akimkaribisha Dk. Magufuli kuzungumza na wananchi wa Lujewa, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Abdallah Bulembo, alisema Kilufi ni Kilusi, ni vyema wananchi wa Mbarali wamchague Haroun Mohammed.
"Kilufi naweza kumuita kirusi kwa sababu
baada ya kukatwa, akahama chama na kujiunga mara Chadema, mara ACT,"
alisema Bulembo.
Akiwahutubia wananchi hao, alisema atahakikisha barabara zilizo Mbarali, zitajengwa kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi.
Dk. Magufuli alisema barabara ya Rujewa mpaka
Mafinga ya kilomita 153, itajengwa na taratibu zimeanza.
Kuhusu vijiji 21 ambavyo vimechukuliwa na TANAPA, alisema atahakikisha suala hilo linamalizwa kwa majibu wa sheria.
Alisema atalimaliza suala hilo baada ya kuapishwa na kuwataka maofisa wa TANAPA kuacha kuwasumbua wananchi walio katika vijiji hivyo.
Alisema atakayekaidi agizo hilo, ajiandae
kutimuliwa kazi.
"Nasema wazi atakayewasumbua wananchi walio
kwenye vijiji hivyo, ajiandae kuondoka kazini," alisema Dk. Magufuli.
Abomoa ngome za upinzani
Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli amezidi
kubomoa kambi za upinzani kwa watu kurudi CCM kutoka vyama vya upinzani.
Akiwa Rujewa, watu wa vyama mbalimbali walijitokeza kurudisha kadi na kisha kuomba kujiunga na CCM.
Mmoja kati ya waliorudisha kadi ni aliyekuwa
Katibu Mipango wa ACT Maendeleo, anayeshughulikia pia masuala ya uchaguzi
wilaya ya Mbarali, Ayoub Mlwilo, ambaye alisema amefikia uamuzi huo kutokana na
sera makini za CCM.
"Nilikuwa kiongozi ACT, nimeamua kurudi CCM kwa hiari yangu," alisema Mlwilo.
Aidha, kiongozi huyo aliwasihi vijana kuacha kudanganywa, waichague CCM kwani ndicho chama imara.
Pia, walikuwepo wanachama wa CHADEMA, ambao nao walirudisha kadi zao.
Dk. Magufuli amekuwa akibomoa upinzani kwa wafuasi wao wengi kurudisha kadi zao na kujiunga na CCM katika maeneo tofauti anayofanya kampeni.
Akiwa Kagera na Geita, Dk. Magufuli alipokea wanachama walioamua kuachana na vyama vyao.
Kila alipokuwa akimaliza kutoa hotuba za kuomba kura, hupata fursa ya kupokea wanachama wapya, ambao huwa tayari kuhama vyama vyao baada ya kusikiliza sera za CCM.
Makambako wafunika
Akiwa Makambako jana mchana, Dk. Magufuli alieleza
kufurahishwa kwake na umati mkubwa uliojitokeza kumpokea na kueleza kuwa hayo
ndio mabadiliko ambayo Watanzania wanayataka.
Alisema mabadiliko ya kweli kwa ajili ya kubadili
maisha ya Watanzania na uchumi, si porojo kama za wagombea wa vyama fulani,
ambao walipewa nafasi wakashindwa kufanyakazi.
"Kwa kweli ndugu zangu wa Makambako mmefunika,” alisema.
Akizungumza katika uwanja wa Polisi Makambako, Dk.
Magufuli alisema dhamira yake ni kuleta mabadiliko kwa kusubiriwa kujenga
Tanzania mpya.
Aliendelea kuwashangaa waliohama kutoka CCM kwa madai kwamba, serikali haijafanya chochote katika kipindi cha zaidi ya miaka 50 tangu Tanzania ipate uhuru.
Bila kuwataja majina, Dk Magufuli alisema baadhi ya
waliohama, walikuwa wasaidizi wa Rais kwa muda mrefu.
"Mtu amekuwa msaidizi wa rais kwa miaka kumi, halafu anatoka na kusema serikali haijafanya chochote.
"Mwingine alikuwa msaidizi wa rais kwa miaka mawili, sasa hii ni kweli jamani, " alihoji Magufuli.
Mgombea urais kupitia UKAWA, Edward Lowassa, alikuwa waziri mkuu kwa miaka miwili wakati Frederick Sumaye, alikuwa Waziri Mkuu kwa miaka 10 katika awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa.
Lowassa na Sumaye, katika kampeni zao, wamekuwa wakitoa ahadi ambazo zinatajwa kuwa ni danganya toto kutokana na kutokuwa na uhalisi.
Dk. Magufuli alisema anataka wafanyakazi wa sekta zote
kupata stahili ili kuwawezesha kufanyakazi kwa ufanisi na kwamba, wafanyakazi
wote wakiwemo wa majumbani wataangaliwa.
Bulembo amlipua Sumaye
Kabla ya Dk. Magufuli kupanda jukwaani, Mjumbe wa
Kamati Kuu ya CCM, Abdallah Bulembo, aliwaambia wananchi wamuulize Sumaye kuhusiana
na kesi yake ya meno ya tembo namna ilivyoisha.
"Gari ya Sumaye ilikamatwa Malinyi na meno ya tembo, aulizwe kesi imeishaje," alisema.
No comments:
Post a Comment