Thursday 11 August 2016

CHADEMA YAKWAA KISIKI MAHAKAMANI, OMBI LAO LA KUPINGA UAMUZI WA IGP KUZUIA MIKUTANO LATUPWA


MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imeyatupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA ya kutaka kupinga uamuzi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), kupiga marufuku mikutano na maandamano ya vyama vya siasa nchi nzima.

Uamuzi huo unatokana na Mahakama Kuu, kukubaliana na hoja mbili za pingamizi la awali, lililowasilishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ikiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu,  Gabriel Malata, akishirikiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Haruni Matagane.

Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali alitupilia mbali maombi hayo kwa gharama, kutokana na kukubaliana na mapingamizi ya serikali kwamba, hayajakidhi matakwa ya kisheria.

Julai 25, mwaka huu, Bodi ya Wadhamini ya CHADEMA kwa kupitia Wakili wao, Peter Kibatala, ilifungua maombi hayo katika Mahakama Kuu huku walalamikiwa wakiwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Baada ya kuwasilisha maombi hayo, Agosti 3, mwaka huu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliwasilisha pingamizi la awali kupinga maombi hayo akiwa na sababu mbili.

Agosti 4, mwaka huu, wakati shauri hilo lilipofikishwa mahakamani kwa kusikilizwa, mbele ya Jaji Kiongozi Wambali, upande wa jamhuri uliomba kuanza kusikilizwa pingamizi la awali, huku upande wa waleta maombi (CHADEMA), ukiomba kusikilizwa yote kwa wakati mmoja.

Hata hivyo, Jaji Kiongozi Wambali aliamuru kusikilizwa kwa pingamizi la awali la serikali, lililokuwa na sababu mbili, ikiwemo ya kwamba maombi hayo hayapo sahihi kisheria mahakamani hapo kwa kushindwa kufuata taratibu.

Mawakili wa Serikali walidai kwamba, waleta maombi hao walipaswa kwanza kukata rufani juu ya uamuzi wa IGP kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Hoja nyingine ni kwamba, maelezo yaliyoletwa na waombaji hao (Bodi ya Wadhamini CHADEMA) hayajakidhi matakwa ya kisheria kwa kushindwa kuonyesha mwombaji ni nani na anakopatikana.

Baada ya kusikiliza pingamizi hilo, Jaji Kiongozi Wambali alitoa uamuzi mdogo juzi, ambapo aliamua kuyatupilia mbali maombi hayo kutokana na kukubaliana na hoja za pingamizi la upande wa jamhuri.

Jaji Kiongozi Wambali alisema maombi hayo hayajakidhi matakwa ya kisheria, hivyo anayatupilia mbali kwa gharama.

Katika maombi hayo, Baraza la Wadhamini wa CHADEMA, lilikuwa likiiomba mahakama itengue amri iliyotolewa Julai 7, mwaka huu na IGP ya kupiga marufuku mikutano na maandamano ya vyama vya siasa.

Pia, lilikuwa linaiomba mahakama kutamka kwamba uamuzi au amri hiyo, ilitolewa bila ya kupewa haki ya kusikilizwa na inaua demokrasia nchini.

TUME YA HAKI ZA BINADAMU YAJA JUU

Katika hatua nyingine, Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora nchini, imekitaka  Chama cha CHADEMA kuacha kutumia neno 'udiktekta' kwenye harakati za kisiasa, kwani Tanzania ni nchi yenye kuzingatia misingi ya kidemokrasia na yenye kuheshimu utawala wa kisheria.

Aidha, imekitaka chama hicho kusitisha maandamano waliyopanga kufanyika Septemba mosi, hadi mahakama itakapotoa tafsiri ya uhalali wa zuio la mikutano ya kisiasa, lililotolewa na Polisi, Juni saba, mwaka huu.

Pendekezo hilo la tume, limetolewa kwa kuzingatia kuwa, CHADEMA imeshafungua mashauri mawili kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam na Mwanza, kuomba mahakama kutoa tafsiri kuhusu zuio la mikutano hiyo.

Kutokana na kesi hizo zilizofunguliwa na CHADEMA, tume hiyo imesisitiza kuwa, Tanzania inazingatia utawala wa kisheria, ndiyo sababu chama hicho kimeamua kufungua kesi hizo mahakamani kwa kuamini kuwa, mhimili huo muhimu wa kutoa haki unafanyakazi kwa mujibu wa katiba.

Maazimo hayo yalitolewa Dar es Salaam, jana na Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga, ambapo alisema polisi na CHADEMA wanapaswa kuacha kutoa kauli zenye kuashiria uvunjifu wa amani na haki za binadamu.

Nyanduga alibainisha kuwepo kwa kesi mbili zilizofunguliwa na CHADEMA kwenye Mahakama Kuu, Masijala ya Dar es Salaam na Mwanza, ambapo kesi hizo bado zinaendelea.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kwa kuzingatia Ibara ya 131 (2) (a) cha katiba, tafsiri sahihi ya zuio hilo la polisi litapatikana mahakamani, hivyo tume hiyo inaamini mashauri hayo yatapewa kipaumbelea na mahakama.

“Tume inaamini mahakama itayapa mashauri hayo kipaumbele kama ilivyofanya wakati wa kusikiliza kesi ya mita 200, mwezi Oktoba, mwaka jana, ili tafsiri yake ipatikane mapema,” alibainisha.

Alisema CHADEMA inapaswa kusitisha maandamano hayo ili kutoa nafasi kwa mahakama kufanyakazi kwa umakini bila shinikizo la muda kati sasa na Septemba mosi, siku ambayo chama hicho kimepanga kufanya maandamano hayo.

Aidha, alilishauri Jeshi la Polisi kutotumia neno 'tutawashughulikia wote wakataokaidi amri', kwa sababu neno hilo linaweza kusababisha matumizi mabaya ya mamlaka ya jeshi hilo nchini.

“Katika mazingira haya, tume imepata wasiwasi kuwa, endapo matamko hayo yakiachwa yaendelee, yana viashiria vya machafuko na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu unaoweza kutokea.

“Iwapo ushauri huu hautazingatiwa, tume inatahadharisha kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo kwa uvunjifu wa haki za binadamu na iwapo itatokea hivyo, wahusika wote itabidi wawajibike,” alisisitiza Nyanduga.

Hatua hiyo ya tume, imefikiwa baada ya kumalizika kwa mkutano wa pamoja uliohudhuriwa na viongozi wa tume hiyo, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Demokrasia nchini, Daniel Loya na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Vicent Mashinji, aliyeambatana na washauri wake.

Mkutano huo uliitishwa kufuatia tamko la CHADEMA la kukusudia kufanya maandamano nchini nzima, Septemba mosi, mwaka huu.

Kufuatia tamko hilo, baadhi ya viongozi wa kitaifa, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na makamanda wa polisi, wamekuwa wakisisitiza kupiga marufuku maandamano hayo, ambayo yamelenga kudhoofisha shughuli za kiuchumi.

No comments:

Post a Comment