Tuesday, 1 March 2016

VIGOGO WA TRA KUHOJIWA ZAIDI


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeruhusu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tiagi Masamaki na wenzake 10, wanaokabiliwa na kesi ya kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 12.7, kwenda kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Kanda ya Dar es Salaam  kwa kuhojiwa zaidi.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, aliruhusu jana, washitakiwa hao wanaodaiwa kuisababishia serikali hasara hiyo kutokana na kuondolewa makontena katika Bandari ya Dar es Salaam, bila ya kulipiwa kodi kwenda polisi.

Hatua hiyo inatokana na ZCO kuwasilisha barua mahakamani hapo kwa ajili ya kuwataka washitakiwa hao kwa mahojiano jana.

Awali, Wakili wa  Serikali, Estazia Wilson, alidai kesi ilikuja kwa kutajwa na kwamba upelelezi haujakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyingine.

Wakili huyo pia aliieleza mahakama kwamba kuna barua kutoka kwa ZCO, ambayo inawataka washitakiwa wote kwa kuhojiwa zaidi.

Hakimu Shaidi alisema naye amepata barua hiyo na kusema kwamba, barua hiyo haijaeleza wanachokwenda kuhojiwa, lakini aliruhusu na kumtaka Wakili wa Serikali  kufuatilia ili kujua utaratibu ukoje.

Pia, alisisitiza juu ya uhuru wa washitakiwa hao kwa kuwa wapo nje kwa dhamana na aliahirisha shauri hilo hadi Machi 29, mwaka huu, kwa kutajwa.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha ICD Azam, Eliachi Mrema, Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara  TRA,  Hamis Omary, Meneja wa Oparesheni  za Usalama na Ulinzi  ICD, Raymond  Louis na Meneja wa Azam ICD, Ashrafu Khan.

Pia, wamo  Habib Mponezya, Meneja Msimamizi na Ufuatiliaji wa Forodha, Burton  Mponezya na Haroun Mpande wa kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta ICT.

Kwa pamoja wanadaiwa kati  ya Juni Mosi na  Novemba 17, mwaka jana, walikula njama kwa kuidanganya serikali  kuhusu sh. bilioni 12.7, baada ya kudai kwamba makontena 329  yaliyokuwepo katika Bandari Kavu ya Azam (ICD), yalitolewa baada ya kodi zote kufanyika wakati wakijua si kweli.

Pia, wanadaiwa  katika kipindi hicho hicho jijini, Dar es Salaam,  walishindwa kutimiza majukumu yao  na kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.

No comments:

Post a Comment