Tuesday, 1 March 2016

HAYA NDIO MAENEO HATARI KWA DAWA ZA KULEVYA DAR




WAKATI Rais Dk. John Magufuli, akitangaza vita dhidi ya dawa za kulevya, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini maeneo hatari zaidi yanayoongoza kwa uuzaji wa dawa hizo.
Imefahamika kuwa maeneo hayo yaliyopo jijini Dar es Salaam, yamekithiri kwa biashara hiyo haramu inayoangamiza nguvu kazi ya taifa, hususan vijana, huku wauzaji na watumiaji wa dawa hizo, wakijiwekea ulinzi na kutoa vitisho kwa wananchi na askari.
Uchunguzi huo pia umebaini kuwa baadhi ya vigogo waliofungwa kwa tuhuma za kuhusika na biashara hizo, wamekuwa wakiendesha biashara hiyo wakiwa gerezani.
Imeelezwa kuwa, wamekuwa wakiwatumia baadhi ya ndugu na marafiki zao wanaowatembelea gerezani, kuwapa maagizo ya namna ya kusimamia shughuli zao.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, uchunguzi huo umebaini namna ambavyo baadhi ya wafanyabiashara hao wanavyotumia mbinu za hali ya juu kuingiza dawa hizo nchini.
Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya utoaji mizigo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNIA), ambaye jina lake na kampuni limehifadhiwa, ambaye alibainisha mbinu hizo.
Alisema wafanyabiashara hao wamekuwa wakitumia simu za mkononi kuingiza dawa hizo nchini.
“Mimi nilifanikiwa kuokota simu tatu, ambazo zilidondoka kutoka kwenye mzigo wa mteja, lakini simu hizo zilikuwa hazifanyika kazi na nikalazimika kuzifungua.
“Nilipozifungua, nilibaini kuwepo kwa unga, ambao kutokana na uzoefu wangu wa kazi sikuwa na shaka kuwa ni dawa za kulevya, ambazo pia zilithibitishwa na watumiaji niliowapelekea ili kubaini,” alisema.
Maeneo yaliyokithiri kwa biashara hiyo ni ufukwe wa bahari ya hindi kuanzia ofisi za kukatia tiketi za boti ziendazo Zanzibar hadi kandokando ya ukuta wa klabu ya kuogelea ya Tanganyika, maarufu kwa jina la Lebanoni.
Katika ukanda wa ufukwe huo, watumiaji hao wamekuwa wakitumia dawa hizo pasipo kuogopa askari.
Kwa mujibu wa uchunguzi, watumiaji hao pamoja na wauzaji, ambao mara kadhaa huweka vijiwe vyao kwenye bustani ya kupumzikia, mkabala na benki ya NBC, wamekuwa wakiwatumia baadhi ya vijana kama walinzi ili kubaini endapo kuna askari au watu wenye kufuatilia nyendo zao.
Gazeti hili lilifanikiwa kukutana na mmoja ya watumiaji wa dawa hizo, ambaye aliweza kuonyesha namna ambavyo biashara hiyo imekuwa ikifanyika kwa njia ya usiri ambao sio rahisi kubainika.
“Huku kama sio mzoefu, huwezi ukabaini ni nani anayetuuzia dawa za kulevya kutokana na kuendesha biashara hiyo kwa kujificha na wakati wote wamekuwa na walinzi, ambao ni miongoni mwa ‘mateja’ wenzetu, ambao huwapa taarifa endapo kuna polisi au watu wenye kuwafuatilia,” alisema mtumiaji huyo, ambaye jina lake linahifadhiwa.
Alisema hakuna msako madhubuti uliofanywa na polisi kuwanasa wauzaji hao kutokana na kuendelea kuwepo.
Aliongeza kuwa, hata msako ukifanyika, wanaokamtwa wamekuwa ni watumiaji wadogo, ambao wameshaathirika zaidi na dawa hizo, lakini hawapewi nafasi ya kushirikiana na jeshi hilo ili kuwataja vinara wa biashara hizo.
Pia, alisisitiza kuwa baadhi yao, ambao wako tayari kuwataja vigogo wanaouza dawa hizo, wamekuwa na hofu ya usalama wao kutokana na baadhi yao waliothubutu kufanya hivyo kubainika.
“Tunaogopa kuwataja kwa sababu wenzetu waliothubutu kufanya hivyo walijulikana na kujikuta wakipata vitisho kutoka kwa wauzaji, hivyo baadhi yao wamekimbia eneo hilo kwa hofu ya usalama,” aliongeza.
Maeneo mengine kwa upande wa wilaya ya Ilala ni Kigogo Mwisho njia panda ya Mbuyuni, Kariakoo mtaa wa Pemba, Ilala Sokoni, Malapa, Bungoni pamoja na Mnazi Mmoja, maarufu kijiwe cha zege.
Katika wilaya ya Kinondoni, maeneo yaliyokithiri kwa biashara hiyo haramu ni Kinondoni kwa Manyanya, mtaa wa Brazil, Block 41 karibu na ukumbi wa Pazi Social Club, Msasani -barabara ya Maandazi, Mwananyamala kituo cha daladala, Kisiwani, kwa Manjunju na kituo cha mabasi Mwenge.
Maeneo mengine ni Magomeni kwa Macheni, karibu na msikiti wa Kichangani na mtaa wa Takadiri, ambapo wapo baadhi ya wauza dawa ambao wanaishi na kituo cha mabasi ya yaendayo mikoani.
Kwenye kituo hicho, imebainika kuwepo kwa mabasi yanayotumika kuingiza dawa hizo nchini.
Mabasi yanayotumika kuingiza dawa za kulevya kutoka nje na ndani ya nchi ni kutoka Tanga na Bukoba, ambayo yanatoka Uganda, Rwanda, Mombasa, Nairobi, Mbeya, Malawi na Zambia.
Kwa upande wa wilaya ya Temeke ni Sandari, Temeke mtaa wa Yombo, viwanja vya Mwembe Yanga, Mtoni kwa Azizi Ally na Kijichi.
Aidha, uchunguzi huo ulibaini kuwepo kwa baadhi ya vilabu vya pombe za kienyeji, ambazo zimekuwa zikitumika kuficha dawa hizo.
Gazeti hili lilishuhudia kwenye kituo cha mabasi cha Kwa Azizi Ally, Mtongani na Kijichi, kuwepo kwa watumiaji hao, maarufu kama mateja, wakiwatoza makondakta sh. 500 kwa kila daladala, kwa madai ya tozo ya kituo.
Mbali na fedha hizo kukusanywa bila utaratibu, baadhi ya madereva waliozungumza na gazeti hili, walisema wamekuwa wakitishwa na hata kuvunjiwa vioo endapo wakikaidi kutoa kiasi hicho cha pesa.
“Hawa mateja wamejiwekea utaratibu wao wa kukusanya sh. 500 kwa kila gari pindi likichukua abiria bila kufahamu fedha hizo zinapelekwa wapi,” alisema mmoja wa madereva hao.
Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na miongoni mwa watumiaji wa dawa hizo kwenye kituo cha mabasi cha Mtoni Kijichi, ambaye alisema fedha wanazozikusanya zinawasaidia kununua dawa hizo.
Alisema kutokana na dawa hizo kupanda bei, wamekuwa wakikosa fedha za kutosha kugharamia dozi ya kila siku, hivyo hutumia fedha hizo kununua dawa hizo.
Akizungumza mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, CP. Simon Sirro, alisema jeshi hilo limeandaa oparesheni maalumu ya kuwakamata vijana wanaotumia dawa za kulevya pamoja na wauzaji wa dawa hizo.
Kamanda  Sirro alisema oparesheni hiyo itawahusisha wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya, hususan wanaojidunga sindano.
Alisema kila mtu atakayekamatwa akiwa ametumia dawa za kulevya, atahojiwa na polisi ataje anakozipata.
“Watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya wanafahamika, wapo wanaopita bandarini na wanaopita nchi kavu, lakini tunataka tuwakamate na vithibitisho ili tunapowafikisha mahakamani, tuwe na ushahidi.
“Ni lazima tuwasaidie vijana wetu, ambao wanataka kuharibikiwa kwa matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu wanapozurura hovyo, nchi yetu ndiyo inayopata aibu,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema jeshi hilo halitamwonea haya kijana yeyote  atakayebainika kuuza au kutumia za kulevya na atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
CHANZO CHA HABARI: UHURU

No comments:

Post a Comment