Tuesday, 1 March 2016

MHASIBU IGUNGA ATUMBULIWA JIPU



MHASIBU wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Maganga Kakema, amesimamishwa kazi kwa muda usiojulikana kwa tuhuma za ubadhirifu wa sh. milioni 23.

Kakema, amesimamishwa kazi ikiwa ni siku chache baada ya gazeti hili kuripoti taarifa ya ubadhirifu wa fedha hizo zinazotuhumiwa kutafunwa na ofisa huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Ntulila Nkunga, alisema kusimamishwa kwa mtumishi huyo kunatokana na fedha anazodaiwa kuzila, sh. milioni 23, zitokanazo na vyanzo vya mapato vya halmashauri, ambazo alikuwa hazipeleki benki.

Nkunga alidai baada ya kufuatilia, ndipo walipoweza kugundua upotevu wa fedha hizo na walipomuuliza, alikiri na kurudisha sh. milioni tisa.

Aidha, kaimu mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, hatua za kumsimamisha kazi zilichelewa kwa sababu ya kufuatilia taratibu za kiutumishi.

Hata hivyo, alidai kuwa uchunguzi zaidi unaendelea kwa mtumishi huyo juu ya upotevu wa fedha hizo na kuwataka watumishi wengine kuwa makini kiutendaji pasipo kufanya ubadhirifu wa fedha za serikali pamoja na wananchi.

Kufuatia tuhuma hizo, Uhuru lilimtafuta Kakema ili kujua kama amepata barua ya kusimamishwa kazi, ambapo hakuwa tayari kuzungumzia tuhuma hizo.

No comments:

Post a Comment