NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Mhandisi Edwin Ngonyani, amezitaka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo
kufanyakazi kwa uadilifu, bidii na kwa uharaka ili kuendana na kasi ya madiliko
ya serikali ya awamu ya tano.
Alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, wakati alipofanya ziara katika
taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ikiwemo Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC), kwa
lengo la kupata mafunzo ya kiutendaji katika taasisi hizo.
Aidha, alizitaka taasisi hizo kuongeza ukusanyaji wa
mapato katika vyanzo vya mapato walivyonavyo, badala ya kutegemea ruzuku kutoka
serikalini.
“Nataka ifikapo mwaka wa fedha ujao, makusanyo ya
mapato yawe yameongezeka zaidi kuliko matumizi na kamwe msikae kusubiri ruzuku
kutoka serikalini, kikubwa ni kubuni vyanzo vyengine vya mapato ili kuweza
kujiendesha”, alisema.
Hata hivyo,
naibu waziri huyo aliwataka watendaji wa taasisi hizo kufanyakazi kwa weledi na
bila woga kwani serikali haitamuonea huruma yeyote anayekiuka kutekeleza wajibu
wake.
“Nawaomba mfanyekazi kwa morali kubwa ili kuisaidia
jamii, ambayo inahitaji huduma muhimu kutoka serikalini,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Ngonyani alimtaka
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Mhandisi Manase Ole Kujan, kutatua changamoto
walizonazo ili kuleta mabadiliko chanya katika taasisi hiyo.
“Unayo nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko hasa katika
mfumo mzima wa ukatishaji tiketi eneo la Magogoni, ambalo limekuwa kero katika
mfumo mzima wa ukusanyaji wa mapato,” alisisitiza.
Mbali na hilo, alimtaka Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius
Mwakalinga, kuandaa taarifa ambayo itaonyesha idadi ya nyumba za serikali
wanazomiliki na ibainishe taarifa ya watumishi wenye stahili ya kupangishwa
kwenye nyumba hizo.
Kwa upande wake, Mhandisi Ole Kujan alisema wakala
huo umepanga kuboresha miundombinu, hasa katika usafiri wa majini na
kuhakikisha inapunguza changamoto ya
usafiri katika vivuko.
Naye Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa baraza la taifa la
ujenzi, Mhandisi Julius Mamilo, alieleza changamoto walizonazo, ikiwemo uhaba
wa fedha, hali inayosababisha baraza hilo kukwama katika kufanya kazi katika
miradi yake ya maendeleo, hususan kazi za utafiti.
No comments:
Post a Comment