Friday 10 February 2017

KISWAHILI SASA LUGHA RASMI RWANDA



Na Immaculate Makilika -MAELEZO

Wabunge nchini Rwanda wamepitisha kwa kauli moja muswada wa sheria ya kuifanya lugha Kiswahili kuwa lugha rasmi nchini humo.

Kufuatia hatua hiyo, sasa Kiswahili nchini Rwanda kinakuwa moja kati ya lugha
tatu za Kinyarwanda, kiingereza na kifaransa zinazozungumzwa na wananchi
kama lugha rasmi miongozi mwao na kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya nne
nchini humo.

Lugha ya Kiswahili nchini Rwanda inatazamiwa kuanza kutumika katika shughuli za uongozi na katika nyaraka za kiofisi.

Aidha, Waziri wa Michezo na Utamaduni nchini Rwanda, Julienne Uwaci alisema
kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na lugha hiyo kuwa na wazungumzaji
wengi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo kuweza
kurahisisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Aliongeza kuwa, “Kiswahili ni lugha rasmi ambayo nchi wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki wanatakiwa kuitumia kwa kuwa kitaongeza tija kwa nchi
ya Rwanda kufaidi matunda ya utengano wa kiuchumi”

Wabunge mbalimbali wa nchi hiyo wametoa maoni, akiwemo mbunge Jean Baptiste
Rucibigango ambapo alisema kuwa “Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na
watu wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki na hakika itakuwa na faida
kuzungumzwa nchini Rwanda”.

Kiswahili kuwa lugha rasmi katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, kunaleta faida nyingi ikiwemo kuongeza wigo wa shughuli za kibiashara na kukuza uchumi wa nchi
wananchama ambazo ni Tanzania, Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi na Sudani
ya Kusini, pamoja na kuimarisha ushirikiano na mahusiano ya kidiplomasia
baina ya nchi hizi.

Hatua hiyo ya Rwanda kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya rasmi ya Taifa ni fursa ya adhimu kwa nchi jirani zinazozungumza zaidi Kiswahili ikiwemo Tanzania, kwani itasaidia
raia wake kuwa na nafasi murua kushiriki katika shughuli za kibiashara
na elimu.

No comments:

Post a Comment