Friday 10 February 2017

MKURUGENZI MTENDAJI WA BANDARI AKUTWA NA HATIA YA MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA


Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Ephraim Mgawe (pichani) amehukumiwa kulipa faini ya shilingi milioni tano au akishindwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka.

Hukumu hiyo imesomwa leo na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Cyprian Mkeha.

Hata hivyo, mshtakiwa Mgawe alifanikiwa kulipa faini hiyo na kuwa huru.

Mahakama pia imemuachia huru naibu wake aliyekuwa anashughulikia huduma, Hamad Koshuma baada ya upande wa mashtaka kushindwa kudhibitisha mashataka dhidi yake.

Akisoma huku hiyo, hakimu Mkeha alisema, upande wa mashtaka kupitia ushahidi wa mashahidi watano uliowasilishwa mahakamani hapo umeweza kuthibitisha pasipo na shaka kuwa mshtakiwa Mgawe alitenda kosa hilo la matumizi mabaya ya madaraka.

Alisema katika ushahidi inaonesha wazi kuwa mshtakiwa  Mgawe alisaini  mkataba huo wa kibiashara na Kampuni ya China Communications Construction Company Ltd (CCCC), kwa ajili ya kuifaidisha kampuni hiyo.

Katika utetezi wake, Mgawe alisema kuwa, yeye hakuwahi kusaini mkataba wa kibiashara kwa ajili ya ujenzi wa gati bali alisaini mkataba kwa ajili ya kupata mkopo ambao alipata baraka kutoka katika bodi ya wakurugenzi wa mamlaka hiyo na kuwa kitendo hicho hakikuipaatia serikali hasara yoyote.

Hakimu Mkeha alisema kuwa haiwezi kubishaniwa kuwa, Mgawe alisaini mkataba kati ya TPA na CCCC   Desemba 5, 2011.

Aliongeza kuwa mkataba huo ulikuwa kwa ajili  ya matumizi ya huduma za uhandisi, manunuzi pamoja na  ujenzi wa gati 13 na 14 .Kwa upande wa mashtakiwa wa pili, Koshuma Hakimu Mkeha alimuachia huru akidai kuwa mtuhumiwa alikuwa akituhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka ambayo hakuwa nayo.

Katika ushahidi na vielelezo vilivyoletwa na mshtakiwa huyo inaonyesha kuwa aliteuliwa kuwa naibu Mkurugenze  Juni 1, 2012 huku upande wa mashtaka ukileta tuhuma kuwa mshtakiwa nae alisaini mkataba huo tarehe  Desemba 5, 2011.

Aliwataka upande wa Jamuhuri kuhakikisha wanapeleleza  vya kutosha tuhuma zinazomkabili mtu  ili hata kama  ataachiwa na mahakama basi aachiwe kwa kuwa hana kosa siyo kwa mapungufu ya upelelezi.

Awali ilidaiwa kuwa Desemba 5, mwaka 2011 Mgawe na mwenzake walitumia madaraka yao vibaya kwa kutoa zabuni ya upanuzi wa gati namba 13 na 14, katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa Kampuni ya China Communications Construction Company Ltd (CCCC), bila kufuata taratibu za sheria ya manunuzi.

Inadaiwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo wakati wakitekeleza majukumu yao ya utumishi wa mamlaka hiyo kwa nafasi ya mkurugenzi mkuu na naibu wake.

Aidha, katika hati ya mashtaka, watuhumiwa hao wanadaiwa kuweka saini mkataba wa kibiashara na kampuni hiyo ya kichina bila zabuni shindanishi, ambapo ni kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma namba 21 ya 2004, ambapo walitumia dola za kimarekani milioni 600.

No comments:

Post a Comment