WATU wanaosaidikiwa kuwa majangili wameua twiga nane na pundamilia
mmoja katika tukio lililotokea mwishoni mwa wiki, kwenye kijiji cha Terrat,
wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara.
Kufuatia tukio hilo,mkazi mmoja wa kijiji cha Ojoro namba 5
wilayani humo,Hussein Ibrahim Janjiti (56), anashikiliwa na Kikosi maalum cha
Kupambana na Ujangili (KDU) Kanda ya Kaskazini,
akihusishwa na tukio hilo.
Kaimu Mkuu wa Kanda wa Kikosi hicho,Jesca Riwa, alithibitisha
jana kutokea kwa tukio hilo na kushikiliwa kwa Janditi, ambaye anahojiwa na
askari wa kikosi hicho, huku wenzake saba wakidaiwa kukimbia baada ya mauaji ya
wanyama hao ambao ni alama ya taifa.
“Tumepata taarifa za majangili kuua twiga eneo la Terati na leo (jana), tumetuma askari wetu eneo la
tukio na nitakuwa katika nafasi ya kulizungumzia suala hilo kwa undani zaidi watakapotuletea
ripoti, lakini tunaendelea kumshikilia Janditi ambaye anatoa ushirikiano
mzuri,”alisema Jesca kwa njia ya simu.
Alifafanua kuwa Janjiti alikamatwa akiwa na nyama ya twiga
mmoja na pundamilia mmoja, huku akiwa na pikipiki nne zilizokuwa zinatumiwa na
wenzake waliokimbia katika kutekeleza uwindaji haramu wa wanyamapori katika
maeneo hayo.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kwamba tukio la kuuawa
kwa wanyamapori hao lilitokea jirani na kituo cha askari hao wa kupambana na
ujangili katika eneo hilo, hatua inayoonyesha majangili kuwa na mbinu kuliko askari
hao wenye mafunzo maalum ya kukabiliana na ujangili huo.
Hata hivyo, Jesca hakukanusha wala kuthibitisha tukio hilo
kutokea karibu na kituo cha askari hao,
akisema kuwa bado hajapata taarifa rasmi ya tukio zima na hivyo hayuko katika
nafasi ya kulitolea ufafanuzi.
“Vijana wangu kama nilivyokwambia,vijana wetu wamekwenda eneo
la tukio, hivyo sina taarifa zaidi hadi hapo watakaponipatia na bila shaka
nitawaeleza, lakini kwa sasa ni kweli tunamshikilia mtu mmoja ambaye
tunaendelea kumhoji,” alisisitiza.
Eneo hilo la Terrat, wilayani Simnajiro lipo katika pori la
akiba la Loksale, linalopakana na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na limekuwa
likikabiliwa na matukio ya ujangili kutokana na wanyamapori kuingia katika
maeneo ya vijiji wakitafuta malisho na maji.
Wimbi hilo la ujangili, hasa wa twiga limezidi kuongezeka
katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na imani kwamba ute unaopatikana ndani
ya mifupa ya twiga unatumika kama moja ya tiba za kupambana na ugonjwa wa
ukimwi.
No comments:
Post a Comment