Wednesday 26 July 2017

MAJALIWA AZICHARUKIA TAASISI ZA VYUO VIKUU



WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amezitaka baadhi ya Taasisi za Vyuo Vikuu nchini zilizofutiwa kudahili wanafunzi kwa mwaka 2017/18, kuacha malumbano, badala yake zifanye marekebisho yanayotakiwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

Wakati Majaliwa akitoa agizo hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Simon Msanjila, amezitaka taasisi hizo kutoa fomu za maombi ya kujiunga na chuo kwa sh. 10,000.

Juzi, TCU ilivifutia udahili wa wanafunzi vyuo 19 na kufuta kozi 75, katika vyuo 22, kutokana na kukiuka sheria, taratibu na kanuni za utoaji wa elimu ya juu hapa nchini.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akizindua Maonyesho ya 12 ya Elimu ya Juu, yaliyoandaliwa na TCU,  yanayofanyika kwenye viwanja wa Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

Alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuhakikisha kuwa wanaendana na hali ya sasa ya taaluma ili iweze kuwaingiza kwenye ushindani.

"Kila mmoja aweze kufanya marekebisho badala ya kulumbana kwenye vyombo vya habari na makongamano, kwani marekebisho haya yanaendana na lengo letu la kufikia hatua nzuri," alisema.

Vilevile, alisema Watanzania wengi, ambao wana umri wa kufanyakazi, ndio hasa wanaoishi vijijini na idadi yao inazidi kuongezeka.
 
"Takwimu za hivi karibuni, zinaonyesha kuwa watu milioni 25.8, walikuwa wanaishi vijijini, mwaka 2004, ikilinganishwa na watu milioni 21 mwaka 2006. 

"Inafurahisha kuona kwamba, asilimia 87 ya Watanzania ni watu wenye umri wa kufanyakazi za kujenga uchumi na theluthi mbili ya Watanzania wote walioajiriwa wako katika sekta ya kilimo," alisema.

Hata hivyo, alisema tatizo la ajira limebaki kuwa kubwa na linaongezeka siku hadi siku. ambapo kila mwaka watu wanaoingia kwenye soko la ajira
wanakadiriwa kufika 650,000 hadi 750,000.

"Takwimu hizi zinaonyesha kazi kubwa tuliyonayo, hususan vyuo na taasisi zinazotoa elimu ya juu hapa nchini, katika kuandaa namna ya kupanga mikakati na ufumbuzi wa tatizo la ajira nchini," alisema.

Kutokana na hali hiyo, alitoa wito kwa taasisi zote kutoa mafunzo yanayoendana na soko la ajira na changamoto za kiuchumi zinazoikabili jamii.

"Wakati umefika sasa wasomi katika vyuo vyetu tujiridhishe kuwa mitaala yetu inawaandaa wahitimu kupata taaluma na stadi za kuweza kujiajiri na kupambana na changamoto za kimaisha," alisema.

Alisema maonyesho hayo ni jukwaa la kipekee, ambalo litaibua mjadala sahihi kuhusu uhalali wa kozi zinazotolewa na vyuo husika vya elimu ya juu.

Kwa upande wake, Profesa Msanjila alisema wizara hiyo haitaivumilia taasisi yoyote kuendelea kutoa elimu ya juu yenye mapungufu.

Alisema vyuo vilivyofutiwa kudahili kabisa kwa baadhi ya progamu zao, vinatakiwa kukaa chini na kuondoa mapungufu hayo na kuomba upya kuhakikiwa.

"Tukumbuke kuwa vijana wanaosoma programu hizo ni wetu na sio sahihi kwao na hata kwa nchi kwa vijana hao kupata elimu yenye mapungufu," alisema.

Alisema wameanza kuona baadhi ya vyuo hivyo vikitafuta njia za mkato badala ya kufuata utaratibu unaotakiwa ili kuhakikiwa tena.

"Hivyo, TCU mhakikishe kuwa utaratibu uliotumika kufanya uhakiki wa vyuo,  utumike huo huo na wale watakaosema wameondoa mapungufu yao, uhakiki ufanyike tena," alisema.

Aliongeza: "Fuateni utaratibu unavyotaka, nimesikia wengine watakaa kwenye mabaraza ili watoe tamko, lakini msimamo wa serikali utabaki kuwa palepale."

Profesa Msanjila pia aliziomba taasisi hizo kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kufundishia katika vyuo vyao.

Alisema serikali imeendelea kuzikumbusha taasisi hizo kuhusu mapungufu kupitia uhakiki unaofanywa mara kwa mara ili kuhakikisha elimu bora inatolewa kwenye taasisi zao.

"Tunapozungumzia utoaji wa elimu bora, unapimwa kwa kuangalia vigezo vya kitaalamu na kimazingira, ambapo hali chanya ya vigezo hivyo huonyesha uhalisia kwamba, wahitimu kutoka chuo husika wana sifa na ubora unaotakiwa," alisema.

Alitaja vigezo hivyo kuwa ni miundombinu, wahadhiri wenye sifa za kielimu na ujuzi unaotakiwa, mtaala unaokidhi viwango vinavyotakiwa, wanafunzi wenye sifa, kuwajibika kwa wahadhiri na mfumo mzuri wa utoaji wa elimu kwenye taasisi.

Kuhusu ada ya maombi ya kujiunga na chuo, alisema vyuo vinatakiwa kuangalia ada hiyo na kuzifanyia kazi. Alisema wizara hiyo imeshatoa maelekezo kuwa, vyuo vyote vya umma, ada ya maombi inatakiwa isizidi sh. 10,000.

No comments:

Post a Comment