Wednesday 26 July 2017

MAKONDA AWATUMBUA MAOFISA ELIMU KATA 12


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametangaza kutafuta  hadi kukipata kiini cha shule za msingi na sekondari mkoani humo kufanya vibaya kitaaluma.

Kufuatia azma hiyo, ametoa siku saba kwa wakuu  wa shule hizo kuandaa na  kuwasilisha taarifa rasmi  za changamoto zote zinazozorotesha elimu pamoja na mapendekezo ya ufumbuzi wake.

Pia, ametoa siku 20 kubomolewa kwa nyumba zote za kulala wageni  na baa zilizo katika maeneo ya shule, kwa madai kuwa zinachangia kuharibu maadili ya wanafunzi.

Makonda alitoa maagizo hayo, Dar es Salaam, jana, katika mkutano uliohusisha wataalamu wa elimu, wakuu wa shule za msingi na sekondari kutoka halmshauri zote  tano za mkoa huo, wakaguzi na  maofisa  elimu wa kata zote.

Katika mkutano huo, Makonda alimwagiza ofisa elimu wa mkoa huo,  kuwatimua  maofisa elimu kata 12, kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu na kutumia fedha za posho ya kufanyiakazi kwa mambo yao binafsi.

Alichukua hatua hiyo baada ya mmoja wa maofisa hao kukiri kuwa, amekuwa akitumia posho ya wadhifa ya sh. 250,000, kwa mambo binafsi, ikiwemo kuvaa huku akishindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu hana fedha zaidi kutoka serikalini.

Maofisa elimu kata wengine 11, walimuunga mkono, wakidai kuwa, wamekuwa wakizitumia fedha hizo kwa matumizi yao binafsi, hali iliyomchukiza Makonda na kuwatimua papo kwa papo.

“Kuanzia leo nyinyi sio maofisa elimu kata, mmeshindwa kutekeleza majukumu yenu,”alisema.

Makonda alisema dhamira ni kuhakikisha Dar es Salaam, inakuwa kinara wa elimu  tofauti na ilivyo sasa.

“Baada ya walimu wakuu kuainisha changamoto zao, tutakaa na maofisa elimu wote kuchambua changamoto hizo na mapendekezo, kisha taarifa itakwenda kwenye Kikao cha Halmshauri ya Mkoa (RCC) na mapendekezo yatawasilishwa kwa wataalamu, ambao wataunda Mkakati wa Elimu Mkoa wa Dar es salaam,”alisema.

Kuhusu hatua za  haraka za utatuzi wa changamoto mbalimbali za elimu, Makonda ameahidi kugawa pikipiki kwa ajili ya maofisa elimu kata wote mkoani humo kuanzia mwezi ujao.

Pia, ameahidi  kutatua tatizo la usafiri kwa wakaguzi wa ubora wa elimu,  ambao walidai kukwamishwa na uhaba wa magari.

Vilevile, ameahidi kumaliza changamoto za walimu kukosa ofisi na samani zake, upungufu wa matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa, uchakavu wa mabati na miundombinu ya shule pamoja na shule zote mkoani humo kupatiwa umeme wa uhakika.

“Pia, ndani ya siku 20, nataka nyumba zote za kulala wageni na baa zilizoko kwenye maeneo ya shule, ziwe zimebomolewa kwa sababu zinachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu maadili ya wanafunzi,” alisema.

Aliongeza: “Unaweza  kujua mwanafunzi yuko darasani, kumbe yuko gesti. Pia, kuna baa zinapiga muziki  kwa sauti ya juu huku walevi wakitukana  matusi mazito.Nataka zibomolewe.”

Makonda aliagiza kuanzia Agosti mosi, mwaka huu, maeneo yote ya shule kupimwa  na shule hizo kupewa hati ili kuepuka uvamizi wa maeneo hayo.

Mbali na hayo, ametaka walimu wote wanaotakiwa kupandishwa madaraja,  kutekelezewa madai yao hayo pamoja na kulipwa madai yao ya likizo  ili waweze kufanyakazi kwa ari.

“Pia, kuna changamoto ya walimu kujilundika katika shule moja, nataka wahamishwe na kila shule iwe na uwiano wa kueleweka. Hivyo ofisa elimu wa mkoa hilo lifanyike kwa haraka,”alisema Makonda.

Alisema yuko tayari kukutana na viongozi wote wa ngazi za juu ili kutetea maslahi ya walimu mkoani humo pamoja na kumaliza changamoto katika sekta ya elimu.

Mkoa wa Dar es Salaam, ulifanya vibaya katika mtihani wa kidato cha nne mwaka juzi, ambapo shule tatu zilishika mkia katika matokeo hayo.
 

Miongoni mwa shule hizo ni Azania, ambayo ilishika nafasi ya tisa kitaifa  kutoka mwisho na shule Mbondole, ambayo ilikuwa ya mwisho.

No comments:

Post a Comment