Thursday, 27 July 2017
VIGOGO WALIOSIMAMISHWA NEMC WAENDELEA KUPIGA MZIGO
WINGU zito limetanda katika Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), baada ya vigogo wanne waliosimamishwa kazi kwa tuhuma za vitendo vya rushwa na urasimu katika mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira, kuendelea na kazi.
Julai 18, mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, aliwasimamisha kazi vigogo hao wanne na kutengua uteuzi wa wajumbe saba wa bodi ya baraza hilo.
Miongoni mwa vigogo waliosimamishwa ni Mwanasheria Mkuu wa baraza hilo, Manchare Heche, Deus Katware, Andrew Karuwa na Benjamini Doto.
Akizungumzia suala hilo, Waziri Makamba alisema utaratibu na mfumo wa serikali katika kusimamisha mtumishi, unachukua muda mrefu na kwamba hatua nyingine zitachukuliwa.
Makamba aliongeza kuwa, barua za kuwasimamisha kazi zitawafuata vigogo
hao kwa vile mchakato wa hatua za kuwasimamisha unachukua muda mrefu.
“Baada ya kuwasimamisha watumishi hawa, bado kuna mamlaka nyingine zitachukua hatua zaidi kwa jambo hili la kuwasimamisha kazi na inachukua muda,”alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa baraza hilo, Carlos Mbuta, alisema aliwaona vigogo hao wakienda ofisini, lakini hana taarifa zaidi.
Alisema ni kweli kumekuwa na taarifa za kusimamishwa kazi, lakini bado hajafahamu taratibu zikoje za kuwasimamisha kazi watumishi hao.
"Nilikuwa nimesafiri Morogoro, hivyo sikuwepo ofisini kwa muda mrefu tangu Waziri Makamba alivyowasimamisha kazi. Isipokuwa nimewaona baadhi yao wamefika ofisini, hivyo ni vyema ukamuona kaimu mkurugenzi au ofisa utumishi wa baraza,"alifafanua Mbuta.
Aliongeza kuwa, mwenye majibu zaidi kuhusu suala hilo la kuendelea kufika ofisini vigogo hao ni Kaimu Mkurugenzi, ambaye hakuweza kupatikana jana kwa vile alikuwa kwenye kikao.
Waziri Makamba alitumia Sheria ya Mazingira Kifungu 19 (2), kutengua uteuzi wa wajumbe saba wa baraza hilo na kuwasimamisha kazi vigogo wanne.
Baada ya kuwasimamisha kazi vigogo hao, Makamba alimteua Dk. Elikana Kalumanga kutoka Taasisi ya Usimamizi na Tathmini ya Rasilimali Asili ya Chuo Kikuu cha Dar es Saalam (UDSM), kuwa kaimu mkurugenzi wa baraza hilo.
Mbali na hilo, Waziri Makamba alimrejesha Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa NEMC, Charles Wangwe kwenye Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine na nafasi hiyo ilichukuliwa na Adam Minja kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Wengine ni Risper Koyi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, ambaye aliteuliwa kuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria NEMC, ambaye amechukua nafasi ya Wanjara Jandwa, aliyehamishiwa Kanda ya Kati - Dodoma.
Waziri Makamba alifanya mabadiliko ya kuwahamisha watumishi wengine kwenye vituo vyao vya kazi, ambao ni Dk. Yohana Mtoni, Ofisa Mazingira Mkuu wa Idara ya Ufuatiliaji na Uzingatiaji wa Sheria, ambaye alichukua nafasi ya Dk. Ruth Rugwisha, anayekuwa Mkuu wa Kanda ya Ziwa -Mwanza.
Makamba aliwataja baadhi ya wakuu wa kanda, ambao walipangiwa vituo vipya kuwa ni Jafari Chimgege, aliyekuwa Mkuu wa Kanda ya Mashariki, ambaye amehamishwa Kanda ya Kati.
Goodlove Mwamsojo, aliyekuwa Kanda ya Mashariki- Dar es Saalam, anakwenda Kanda ya Nyanda za Juu, Dk. Vedastus Makota, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma, atahamishiwa Kanda ya Kusini- Mtwara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment