CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kinajiandaa kufanya mabadiliko makubwa ndani ya miaka
mitano ijayo ili kuwa cha kisasa na kujiendesha kwa ufanisi zaidi katika
kuwahudumia Watanzania.
Kimesema
hatua hiyo inalenga kuhakikisha Watanzania wanaendelea kufurahia matunda ya
uhuru na kuwa na maendeleo ya haraka, ambapo suala la uboreshwaji wa maslahi ya
watumishi, uwezo wa kiutendaji na mazingira bora katika sekta zote ni mambo
yatakayopewa kipaumbele zaidi.
Hata
hivyo, kimeonya kuwa serikali yake haitasita kuwawajibisha watumishi na
watewndaji wote, ambao watakwenda kinyume cha taratibu na kukwamisha
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwani, kufanya hivyo ni kurudisha nyuma
jitihada za nchi kujikwamua.
Hayo
yameelezwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rajab Luhwavi, alipokuwa
akizungumza na watumishi na watendaji, ambapo alisema kupitia mpango huo, CCM
inalenga kuwa Chama kinachokwenda na wakati kwa kuwa na watumishi wenye uwezo
kulingana na wakati.
Alisema
Chama kimewaagiza watumishi wake wote kujiendeleza kielimu na kwamba, kipo
tayari kugharamia mafunzo yao kitaaluma katika vyuo vya ndani na nje ili
kuongeza tija na ufanisi katika utendaji.
Kwa
mujibu wa Luhwavi, amewataka watumishi wa CCM wenye elimu ya darasa la saba,
kuhakikisha kati ya sasa na Juni, mwaka huu, wanajitokeza kujiorodhesha na
kujisajili kwenye mpango maalumu wa elimu ili waweze kujiunga na masomo ya
kidato cha kwanza.
“Tunatoa
miaka mitatu kwa walio na elimu ya darasa la saba wahakikishe wanamaliza kidato
cha nne na baada ya hapo watakaoshindwa kwenda na agizo hili tutaachana nao kwa
amani. Katika hili hatutanii kwani Chama sasa kinataka kujijenga zaidi na kuwa
bora katika kila idara,” alisema.
Alisema
chini ya mpango huo, mtumishi wa chama katika kila ngazi ya elimu atatakiwa
kujiendeleza na kwamba, CCM itashirikiana nao kuhakikisha azma hiyo inatimia.
Luhwavi
alisema mpango huo wa maboresho pia utahusu kuwajengea uwezo watumishi wa chama
kupitia mafunzo mbalimbali yatakayoanza kutolewa na CCM kupitia chuo chake cha
Ihemi kilichoko mkoani Iringa.
“Tutaanza
na makatibu muhtasi kuwapeleka Ihemi ili wakapate mafunzo maalumu na kurudi
kwenye utaratibu wetu wa awali, ambao ulituwezesha kuwa na watumishi makada,
wenye uwezo na ari ya kukitumikia Chama,” alisema.
Awali,
akizungumza katika mkutano huo uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Katibu
Msaidizi Mkuu wa CCM, anayeshughulikia vyama vya wakimbizi kusini mwa Afrika,
Amos Siyantemi, aliwaomba wana-CCM kutembea kifua mbele kutokana na kazi nzuri
ya Rais wa awamu ya tano, Dk. John Magufuli.
Siyantemi
alisema kila mwana-CCM anapaswa kujivunia mafanikio hayo na kuwapinga
wanaojaribu kumtenganisha Dk. Magufuli na CCM.
Mkutano
huo uliwahusisha watumishi wa CCM na jumuia zake kutoka mikoa ya Mwanza,
Shinyanga, Simiyu, Geita na Mara.
No comments:
Post a Comment