Tuesday, 1 March 2016

MAPAMBANO YA POLISI, MAJAMBAZI YASHIKA KASI


JESHI la polisi mkoani Arusha, limewaua watu watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi, baada ya kubaini walikuwa na bunduki aina ya AK 47, milipuko na silaha nyingine za jadi, yakiwemo mapanga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, kisha alimtaja mmoja wa waliouwa kuwa ni Athumani Ramadhani (26) au kwa jina lingine Kassimu.
Alisema watu hao waliuawa eneo la Engosheraton-Sinoni, ambapo mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Nasra, ambaye ni mke wa Athuman Ramadhan, anashikiliwa na polisi kwa upepelezi.
Kamanda Sabas alisema majambazi wengine hawajafahamika na miili yao  imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru kwa ajili ya uchunguzi na kutoa nafasi kwa wananchi kuwatambua.
Akieleza ilivyokuwa, Kamanda Sabas alisema asubuhi mwishoni mwa wiki iliyopita, alipata taarifa kutoka kwa raia mwema kwamba, eneo la Engosheraton – Sinoni kuna kijana wanayemtilia shaka kuwa anajihusisha na matukio ya uhalifu.
Alisema baada ya taarifa hiyo, waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata Athumani na baada ya kumpekua, alikutwa na milipuko aina ya Explogil TMV6 water explosive 17 na Giogel Kubela 10.
Vitu vingine walivyomkuta navyo kijana huyo ni makoti makubwa mawili na kofia moja ya kuficha uso, ambapo baada ya kumkoji alibainisha juu ya uwepo wa wenzake wawili anaoshirikiana nao katika kufanya uhalifu.
“Tuliandaa mtego mapema na ilipotimu saa 5 usiku, polisi wakiongozana na mhusika walienda eneo la Faya, kwenye nyumba iliyodaiwa wenzake wapo. Polisi waligonga na wakati mlango ukifunguliwa, Athumani alipiga kelele ‘Takbir’, baada ya kelele hiyo polisi walianza kushambuliwa kwa risasi toka kwa watuhumiwa waliokwenda kuwakamata,” alisema.
Alisema kwa kutumia mbinu za medani za kivita, polisi walifanikiwa kuzima mashambulizi hayo na kuingia chumbani walikokuta vijana wawili waliokuwa wamejeruhiwa baada ya majibizano hayo ya risasi.
Kamanda Sabas aliongeza kusema kuwa, kwa bahati mbaya wakati wa majibizano ya risasi kati ya askari na wahalifu hao, walimpiga risasi Athumani, ambapo wote watatu walifariki wakiwa njiani kupelekwa hospitali kwa matibabu.
Alisema upekuzi ulipofanywa katika chumba cha wahalifu hao wawili, walikuta sare tano za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kofia tano za kuficha nyuso, vazi moja la karate na pikipiki moja yenye namba bandia za usajili MC 983 BMK.
Aidha, alivitaja vitu vingine kuwa ni bendera mbili nyeusi zenye maandishi ya lugha ya Kiarabu, zinazotumiwa na makundi ya kigaidi, kisanduku cha chuma na hati ya kusafiria ya Abrahaman Athuman Kangaa, iliyotolewa Aprili 2, 2013.
Vingine ni simu tano za mkononi, ambazo baadaye kati ya hizo, moja ilitambuliwa kuwa ya marehemu Mary Joseph, aliyekufa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Februari 20, mwaka huu, Engosheratoni-Sinoni mkoani Arusha.
Alisema pamoja na vitu hivyo, walikuta pia kifurushi cha unga wa baruti, kisu kimoja kikubwa, karatasi zenye ujumbe wa vitisho unaosema, ‘Nasaha kwa Kova, mzee andaa kamati ya mazishi ya vipolisi vyako, tukiwamaliza tutakufikia wewe.’
“Pia katika upekuzi huo, tulikuta mafuta ya kusafishia bunduki pamoja na bunduki aina ya AK 47 iliyosajiliwa 1998, yenye namba AVF 0822 na magazine yake iliyokuwa na risasi 18,” alisema Kamanda Sabas.
Juzi, jijini Dar es Salaam, Kamishna wa  Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema jeshi lake lilifanikiwa  kuwaua majambazi watatu kati ya 12,  waliohusika katika tukio la uporaji benki.
Alisema majambazi hao waliuawa  katika majibizano makali  ya risasi baina yao na polisi katika kijiji  cha Mchui, Mkuranga  mkoani Pwani .
Wakati hayo yakitokea, siku chache zilizopita serikali ilitangaza vita kali dhidi ya majambazi nchini, ambapo ilisema imeanza kufanya  operesheni kali yenye lengo la kuusambaratisha mtandao mzima wa ujambazi.
Taarifa hiyo ya serikali ilitolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, ambaye alisema itakapobidi, italiomba Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kusaidia operesheni hiyo.
Waziri huyo alisema, operesheni inayoendeshwa ni kubwa na inalenga kuvunja kabisa   mtandao wa ujambazi na kwamba, itakuwa kali zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
“Majambazi hawatasalimika. Tutawafyeka wote. Tutawasaka kwa namna na gharama yoyote. Tutazungumza na JWTZ ili watupe ruhusa na kusaidiana nao kufanya operesheni  kubwa  ya kuwasaka katika misitu ya mkoa wa Pwani.
“Kama kuna kambi za ujambazi au mafunzo yanayotolewa katika misitu hiyo au kokote nchini, tutazisambaratisha,” alionya Kitwanga.
Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi, kushiriki kikamilifu katika kuwafichua watu wanaojihusisha na matukio ya ujambazi ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
“Tutahitaji ushirikiano mkubwa wa raia wema kutupa taarifa za wahalifu hao popote walipo,”alisema Kitwanga.
Serikali imefikia hatua hiyo baada ya vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha nzito za kijeshi, yakiwemo mabomu na milipuko mingine vikishamiri kwa kasi maeneo mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment