Wednesday, 30 September 2015

MAFISADI WAJIPANGE-MAGUFULI




NA CHARLES MGANGA, DODOMA
MGOMBEA urais wa CCM, Dk. John Magufuli, amesema dhamira yake ni kuiongoza nchi kupiga hatua za haraka kimaendeleo na kukabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Amesema anafahamu kuna changamoto nyingi, lakini hana shaka kuwa serikali yake itapambana kikamilifu kukomesha rushwa na vitendo vya unyanyasaji kwa wananchi wanyonge.
Wakati Dk. Magufuli akiyasema hayo, mgombea ubunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde maarufu kama Kibajaj, amesema mgombea urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, hana tofauti na popo.
Akizungumza akiwa njiani kutoka Iringa kwenda Dodoma, kuendelea na kampeni zake za kuomba ridhaa ya wananchi, Dk. Magufuli alisema anataka kujenga Tanzania mpya itakayokuwa sauti ya wanyonge.
"Nataka kuongoza taifa lenye amani na lisilo na rushwa na mafisadi. Nafahamu kuna changamoto, lakini nimejipanga kuhakikisha hilo napambana nalo kwa vitendo,” alisema.
Alisema atahakikisha anaboresha huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi kwa kutumia maliasili za taifa ili kuboresha mapato ya serikali.
Alisisitiza kuwa wanyonge wanaofanya biashara ndogo ndogo wakiwemo mamalishe, babalishe, bodaboda na wengine watafanya shughuli zao kwa amani na kwamba, utaratibu wa kuwaangalia utaangaliwa zaidi.
"Nchi yetu ina utajiri ambao tukiutumia vizuri, tutaendesha nchi kwenda kwenye maeneo kwa haraka. Tutaanzisha vyanzo vipya vya mapato na si kuwanyanyasa na kuwadhulumu wanyonge,” alisema.
Katika mikutano yake ya Migori, Idodi, Mtera na Pawaga mkoani Iringa na Chipogolo Jimbo la Kibakwe, Dk. Magufuli aliendelea kusisitiza kukabiliana na kero za afya na maji.
"Watanzania wenzangu tumetoka mbali, tumefika mbali na tunakwenda mbali. Mengi mazuri yamefanywa na awamu zilizotangulia, awamu ya tano ya Magufuli nayo itafanya mambo mazito na makubwa,” alisema.
KIBAJAJ AMVAA LOWASSA
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mvumi, jimboni humo jana, Kibajaj aliwafananisha wanasiasa wa upinzani na popo.
Alisema Lowassa na Sumaye wanaposimama na kutoa kauli zisizofaa dhidi ya serikali, zinawarudia wenyewe.
"Hawa watu ni sawa na popo. Huyu mnyama sijui ni ndege, huweka kichwa chini ili aweze kumchafua Mungu, lakini badala yake hujichafua mwenyewe. Sasa maneno machafu wanayotoa yanawarudia wenyewe," alisema.
Alisema hata Lowassa alipofika Mvumi, alizomewa kwa mwendo wake wa roboti huku akishindwa kuwaeleza Watanzania nini atafanya akipewa ridhaa, kitendo kinachowakera wengi.
"Hapa Lowassa alifukuzwa, alizungumza kwa dakika moja tu, kwa kweli hapa wenzetu wa upinzani wamepotoka,” alisema.
Alisema tayari Watanzania wanafahamu ukweli, wataichagua CCM kwani, hawawezi kumchagua Rais ambaye muda wote serikali itakuwa ikimuuguza.
MALECELA KATIKA UBORA WAKE
Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela amewaomba Watanzania kumpa kura Dk. Magufuli ifikapo Oktoba 25, mwaka huu na kamwe wasifanye makosa.
Alisema mgombea wa CHADEMA si mwadilifu na hastahili hata kukaribia Ikulu ya Tanzania, hivyo hakuna mtu aliyetayari kutumika kuwabeba mafisadi mgongoni.

KIMBISA: MAGUFULI  ATASHINDA
Awali, kabla ya Dk. Magufuli kupanda jukwaani, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, alisema wanaosema kiongozi huyo ni mkali wanakosea.
Alisema Dk. Magufuli ni kiongozi mpole, karimu na mwadilifu na kwamba, sifa kubwa ni uchapaji kazi na ufuatiliaji wa maagizo na maelekezo yake.
Alitumia fursa hiyo kumhakikishia Dk. Magufuli kuwa atapata ushindi wa kishindo na mkubwa mkoani Dodoma na Tanzania nzima, hivyo asiwe na shaka.
"Dodoma ndiyo ngome ya CCM, Dk. Magufuli atapata ushindi mkubwa bila wasiwasi. Achaneni na wanaoeneza propaganda kuwa Dk. Magufuli ni mkali. Sasa mwalimu hajapanda daraja akifuatilia kulikoni ni ukali huo ndugu zangu, "alisema Kimbisa.

No comments:

Post a Comment