Na Hamis
Shimye, Zanzibar
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM), kimesema mgombea wake wa urais wa Zanzibar, Dk. Ali
Mohammed Shein, atashinda kwa asilimia zaidi ya 60 dhidi ya wapinzani wake.
Kimesema
ushindi huo unatokana na tathmini yao walioifanya visiwani hapa pamoja na
kukubalika kwa Dk. Shein kwa makundi yote ya jamii ndani ya visiwa vya Unguja
na Pemba.
Tathmini
hiyo ya awali ya ushindi ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Zanzibar,
Vuai Ali Vuai, katika ukumbi wa mikutano wa Afisi Kuu ya CCM,
Kisiwandui-Zanzibar.
Alisema
tathmini hiyo ya awali iliyofanywa na CCM inabainisha kuwa Chama kimefanikiwa
sana kwenye kampeni zake kutokana na kukubalika kwa wananchi wake.
"Uhudhuriaji
wa watu kwenye kampeni zetu kwa wingi tena kwa makundi ni kielelezo kimojawapo na
pia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwa mwaka 2010 kwa asilimia 90,"
alisema.
Naibu
Katibu Mkuu huyo alisema dalili za ushindi kwa CCM zimeanza kuonekana mapema
tangu ilipozindua kampeni zake na kutoa viashiria vingi.
Alisema
miongoni mwa sababu kubwa zinazomfanya Dk. Shein kupata ushindi huo ni pamoja
na udhaifu wa vyama vya upinzani, ikiwemo CUF na mgombea wake Maalim Seif
Shariff Hamad.
Vuai
alisema sababu nyingine inayompa ushindi Dk. Shein ni kushindwa mara nne kwa
Maalim Seif katika uchaguzi uliofanyika katika awamu nne tofauti huku mgombea
wa CCM akitelekeza ilani kwa vitendo pamoja na vigezo vingine 19.
Kwa
mujibu wa Vuai, tathmini hiyo wameifanya kwa umakini mkubwa kuanzia ngazi ya
shehiya hadi taifa.
"Tuna
mtandao mpana na tunajua ni wanachama wangapi watatupa kura, wakeretwa wetu ni
kina nani na vipi watatupa kura. Hivyo hatuna wasiwasi na ndio maana tunasema
uchaguzi huu tutashinda zaidi ya asilimia 60," alisema.
Alisema
kwa siasa za Zanzibar ni rahisi kujua kura zako kwani jamii nyingi zinajuana na
ndio maana CCM imekuja na tathmini hiyo ya ushindi.
Vuai
alisema hata katika visiwa vya Pemba, mwamko wa wananchi umekuwa mkubwa zaidi
na kuanza kuwa na imani kubwa na CCM kutokana na sera zake.
Alisema
awali, Pemba kulikuwa na siasa za vitisho hasa kwa wafuasi wa CCM kupigakura
kwa woga na kuipenda CUF na ndio maana vijana wengi wamechoshwa na siasa za
Maalim Seif.
Alisema
utekelezaji wa ilani, kukuza pato la Zanzibar, kukuza zao la karafuu na utekelezaji
wa ujenzi bora wa miundombinu ni miongoni mwa mambo yanayoipa ushindi zaidi CCM
kwenye uchaguzi huu.
Vuai alisema
serikali ya umoja wa kitaifa ipo kikatiba na hata kama wakishinda uchaguzi kwa
asilimia nyingi, hawataivunja serikali hiyo.
Alisema
chochote kinachotaka kutokea kwenye serikali lazima kiendane na Katiba
iliyotengeneza serikali hiyo.
"Hapa
lazima Chama kiseme wazi kuwa hakuna anayeweza kuvunja serikali ya umoja wa
kitaifa kwa kuwa ipo kikatiba,” alisema.
AWAPONDA
WANASIASA UCHWARA
Akizungumza
kuhusiana na mafuta na gesi, Dk. Shein alisema Rasimu ya Muswada wa Sheria ya
Mafuta na Gesi upo tayari ofisini kwake.
Pia,
ameeleza kushangazwa kwake na baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuchukua ujiko wa
suala hilo, ambalo kwa kiasi kikubwa lilishamaliza kufanywa na serikali yake.
Alisema
yeye si mtu wa kujisifia na angekuwa ni mtu wa hivyo, angetaka sifa hizo kwa
kuwa alianza kulishughulikia suala la mafuta na gesi tangu alipokuwa Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Nawashangaa
sana wanaojisifia, lakini hawajui ukweli na hili lazima Wazanzibar mlifahamu
kuwa nilianza kulifanyia kazi muda mrefu sana,” alisema.
Pia,
alisema tayari serikali imeshaingia makubaliano ya awali na baadhi ya nchi
ikiwemo Uholanzi kwa ajili ya utafiti wa mafuta na gesi visiwani humo.
Hata
hivyo, alisema baada ya makubaliano hayo kuna nchi zaidi ya saba zimeonyesha
nia, lakini amewataka wasubiri hadi sheria itakapoanza.
No comments:
Post a Comment