Na
Mwandishi Wetu
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya vurugu
na uvunjifu wa amani vinavyofanywa na vyama vilivyo kwenye kundi la UKAWA ili
kuwapa fursa wananchi kusikiliza sera na Taifa libaki na umoja, mshikamano na
utulivu baada ya uchaguzi.
Pia, Chama kimevitaka vyama vinavyounda UKAWA, viwaambie
ukweli Watanzania kuhusu sababu za mgombea wao wa nafasi ya urais, Edward
Lowassa kushindwa kuhutubia baadhi ya mikutano ya hadhara badala ya kuwahadaa
kwa kutengeneza matukio na vioja ili kuficha udhaifu wake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CCM kwa vyombo vya
habari jana, kupitia kwa Mjumbe wa Kamati ya Kampeni, January Makamba, CCM
imesikitishwa na matukio ya vurugu yaliyofanywa na wafuasi wa UKAWA katika mikoa
ya Tanga na Mbeya mapema wiki hii.
Juzi, akiwa mkoani Tanga, Lowassa alipangiwa kuhutubia, lakini
wafuasi wa vyama hivyo waliwarushia mawe viongozi wa CCM na kutupa chupa, nyingine
zikiwa na mikojo, kwa lengo la kutaka kuzusha vurugu.
“CCM tumesikitishwa sana na vitendo vya wafuasi wa UKAWA
kurusha mawe na chupa, nyingine zikiwa na mikojo kwenye Ofisi ya CCM Mkoa wa
Tanga kabla na baada ya mkutano wao uliofanyika Uwanja wa Tangamano.
“Ifahamike kwamba tukio la Tanga si la kwanza kwani
Septemba 27, mwaka huu, viongozi wa UKAWA waliwapanga vijana katika Stendi ya
Uyole mkoani Mbeya, kwa lengo la kumfanyia vurugu mgombea wa CCM, Dk. John
Magufuli, na kumpigia kelele ili wananchi wasimsikilize.
“Kwa bahati nzuri, mgombea wetu alikabiliana na hali
hiyo kwa kuonyesha ukomavu mkubwa wa kisiasa, lakini vitendo vile havikuwa vya
kistaarabu. Mashabiki na wafuasi wa CCM wana uwezo wa kufanya mambo kama hayo,
tena kwa ufanisi zaidi, lakini hatuoni kama hiyo ni namna bora ya kuomba ridhaa
ya kuongoza Watanzania,” alisema January.
Aliviasa vyama hivyo kuwahimiza mashabiki wao kuachana
na mwenendo wa vurugu katika kipindi kilichobaki cha kampeni ili kuhakikisha
kuwa nchi inabaki salama mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
“Tukio la Ofisi ya CCM Tanga kupigwa mawe limewaudhi na
kuwakera wapenda amani wa mkoa huo. Hata hivyo, viongozi tumewasihi kuwa
wasilipize kisasi. CCM ina dhamana ya kuongoza na kulinda amani ya Watanzania,
lakini wenzetu hawana dhamana hiyo.
“CCM ina uhakika wa kushinda na kushika dola, lakini UKAWA
wana uhakika wa kushindwa na tayari wameanza kuonyesha ishara za kukata tamaa.
Tunawapongeza wana CCM kote nchini kutokana na utulivu waliouonyesha katika
wakati wote wa kampeni hadi sasa,” alisema Makamba.
Taarifa hiyo ya CCM pia imeeleza tukio la kuahirishwa
kwa mkutano wa hadhara uliopangwa kuhutubiwa na Lowassa juzi, mjini Tanga kuwa
ni hadaa na vioja ambavyo havitakiwi kufanyika katika siasa za sasa.
Katika taarifa hiyo, January alieleza kuwa wakati
umefika kwa viongozi wa genge la UKAWA kuwa wakweli na kueleza sababu za kweli
za kuahirishwa kwa mkutano huo pamoja na mingine ambayo inatolewa maelezo ya
hadaa.
Viongozi wa UKAWA walitangaza kuahirisha kufanyika kwa
mkutano huo kwa madai ya kujaa kwa watu wengi kiasi cha kuhatarisha uhai wa
waliohudhuria mkutano huo.
“Hii si mara ya kwanza kwa wenzetu kutafuta kisingizio
cha kutofanya mkutano wa kampeni. Walipokuwa Geita, walitangaza kuahirisha
mkutano kwa madai kuwa jukwaa na vipaza sauti havikuwa vikifanya kazi ingawa
aliyetangaza hivyo alipanda kwenye jukwaa na kutangaza kwa kutumia vipaza
sauti. Mabadiliko wanayohubiri wenzetu yanaanza na kusema ukweli.
“Imefika wakati sasa viongozi wa Ukawa wawaeleze ukweli
Watanzania kuhusu mgombea wao kushindwa kuhutubia baadhi ya mikutano au
kuhutubia kwa dakika tatu kuliko kuwahadaa kwa kutengeneza matukio na vioja
badala ya kueleza mapungufu ya mgombea wao.
“Katika mikutano ya kampeni, ikiwamo ya CCM na mingine
katika shughuliza kitaifa, ni kawaida kwa watu kuzidiwa na kupewa huduma ya
kwanza wakati mikutano ikiendelea. Hii ni mara ya kwanza ambapo mkutano wa
kisiasa unaahirishwa kwa sababu ya wingi wa watu,” alisema Makamba.
Katika taarifa yake hiyo, CCM iliwashukuru wanachama
wake wa mkoani Tanga kwa kubaini na kutorubuniwa na propaganda nyepesi ya UKAWA
kwamba mkutano wa Tangamano uliahirishwa kwa sababu ya wingi wa watu.
No comments:
Post a Comment