Wednesday, 30 September 2015

PINDA AONGOZA MAZISHI YA CELINA KOMBANI


NA LATIFA GANZEL, MOROGORO
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, ameongoza  maelfu wananchi kwenye mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Celina Kombani, yaliyofanyika shambani kwake Lukobe, nje kidogo ya Manispaa ya Morogoro.
Ibada ya kumuombea Celina aliyefariki dunia nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu, ilifanyika katika Uwanja wa Jamhuru mjini hapa kabla ya safari ya kwenda Lukobe kuanza.
Spika wa Bunge, Anna Makinda, akizungumza kwa niaba ya wabunge alisema Celina ameondoka wakati taifa bado linamuhitaji na kwamba, matendo yake ndani ya Bunge yataendelea kukumbukwa.
Alisema katika maisha matendo mema ya mtu hubaki duniani na wanaobaki wanapaswa kuyaendeleza na kwamba, hakuna mtu aliyeumbwa kwa ajili yake binafsi bali ameletewa kusaidiana katika mambo mbalimbali.
Alisema ushupavu na iumara wa Celina utabaki kuwa nguzo imara kwa viongozi wa sasa na wale wa vizazi vijavyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya mazishi, Jenista Mhagama, alisema Celina ameacha pengo kubwa serikalini na kwa wananchi wa Ulanga Mashariki pamoja na familia aliyokuwa akiiongoza.
katibu wa NEC ya CCM, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, alisema Celina kila alipopita aliacha alama nyingi nzuri kutokana na utendaji wake, na kila mtu aliyemuacha katika eneo fulani anamkumbuka kwa matendo yake na busara.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Rajabu Rutengwe, alisema mkoa umepoteza kiongozi mahiri, mchapakazi aliyekuwa mpigania maslahi ya mkoa muda wote.

No comments:

Post a Comment