Thursday 11 August 2016

UTAFITI TWAWEZA WABAINISHA HUDUMA ZA AFYA, USAFI VYAIMARIKA



UTAFITI wa 'Sauti za Wanachi' uliofanywa na Shirika la Twaweza, umebaini kuimarika kwa usafi na huduma za afya kwenye vituo mbalimbali vinavyotoa huduma hiyo nchini, tangu serikali ya awamu ya tano kuingia madarakani.

Aidha, utafiti huo umeonyesha kuwepo kwa ongezeko la wananchi wanaotibiwa kwenye vituo vya afya vya serikali kwa asilimia 61, ikilinganishwa na asilimia 47, ya mahudhurio hayo kwa mwaka jana.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa, kuna upungufu wa dawa na vifaa tiba, ambapo asilimia 59 ya wananchi, wametaka kuongezwa kwa juhudi za upatikanaji wa vifaa hivyo, ikilinganishwa na asilimia 53, iliyopendekeza kuboreshwa kwa huduma hizo mwaka 2015.

Serikali imesema mafanikio hayo yanatokana na mabadiliko yanayoendelea kufanyika katika sekta ya afya, ikiwemo kukabiliana na vitendo vya rushwa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.

Hayo yalielezwa jana, Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, wakati akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, ambapo alisema takwimu hizo zinaonyesha mabadiliko chanya katika sekta ya afya.

Alisema kwa upande wa wahudumu wa afya, utafiti ulionyesha wahudumu hao wanapatikana kazini kwa wakati,  wakiwa wasikivu kwa wagonjwa huku usafi kwenye vituo vya afya ukiimarika.

“Licha ya kuwepo kwa mabadiliko hayo, lakini upungufu wa dawa na vifaa vyingine, vikiwemo vitanda, mashuka na chandarua bado ni changamoto.

“Katika siku za usoni, ni muhimu kufanya utafiti wa kina ili kuboresha huduma za afya na kuhakikisha kuwa, wahudumu wa afya na vifaa vya matibabu vinapatikana kwa wakati,” Eyakuze alisisitiza. 

Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema, asilimia 18, ya wananchi waliripoti kuwepo kwa upungufu wa madaktari kwenye vituo vya afya miezi mitatu iliyopita, ikilinganishwa na asilimia 43, walioliona tatizo hilo mwaka jana.

Aidha, alisema asilimia 73, ya wananchi walioshiriki kwenye utafiti huo, walisema waliheshimiwa ipasavyo na watoa huduma za afya, tangu kuanza kwa mwaka huu.

Aliongeza kuwa idadi hiyo ni tofauti na asilimia 42, ya wananchi waliotoa maoni hayo mwaka 2015.

Kwa upande wa usafi, alisema kwenye vituo vya afya, kulionekana kuboreshwa kwa huduma hiyo muhimu, ambapo wananchi waliolalamikia suala hilo walipungua kutoka watatu kati ya 10 mwaka jana, hadi kufikia mtu mmoja kati ya watu 10, mwaka huu.

Eyakuze alisema malalamiko kuhusu kushindwa kumudu gharama za matibabu nayo yamepungua.

“Mwaka jana, asilimia 34 ya wananchi walisema gharama za matibabu zilikuwa kubwa na hawakuweza kulipa gharama hizo, lakini mwaka huu, asilimia 19, ndio waliolalamikia gharama hizo,” alisema.

Akizungumzia kuhusu maduka ya dawa, Eyakuze alisema wananchi waliotembelea maduka hayo walipungua kutoka asilimia 19, mwaka jana hadi asilimia 13, mwaka huu.

Aliongeza kuwa asilimia 73, ya wananchi waliripoti kusubiri kwa muda usiozidi saa moja kabla ya kumuona daktari.

“Wengi wao walikiri kupewa maelezo mazuri kuhusu maradhi yanayowasibu, ambao ni asilimia 92, kisha asilimia 81, waliandikiwa dawa stahiki.

“Asilimia 70, walifanikiwa kupata angalau baadhi ya dawa walizozihitaji kutoka kwenye kituo cha afya,” aliongeza.

Pamoja na kuimarika kwa huduma hizo za msingi kwa binadamu, wananchi kupitia utafiti huo, waliainisha changamoto zingine walizokumbana nazo katika vituo vya afya vya serikali.

Miongoni mwa changamoto walizokumbana nazo ni ukosefu wa vitanda (asilimia 31), mashuka (asilimia 27) na chandarua (asilimia 29).

Pia, asilimia 36, waliripoti kuona mgonjwa zaidi ya mmoja, wakilala kwenye kitanda kimoja, ikilinganishwa na asilimia 30, mwaka jana.

Hata hivyo, wananchi kupitia utafiti huo walisema walishuhudia makundi ya wazee, watoto chini ya umri wa miaka mitano pamoja na wajawazito, wakitozwa gharama za matibabu.

Hivyo mkurugenzi huyo wa Twaweza alisema, ni muhimu kutumia utafiti huo kujifunza kutokana na mapungufu yaliyopo huku akisisitiza kutolewa motisha kwa watoaji huduma za afya.

Aidha, alitaka kuwepo kwa ufuatiliaji kuhakikisha kuwa, kila kitu ambacho wananchi wanakumbana nacho kwenye huduma hizo, kifahamike.

Matokeo hayo yametolewa na taasisi hiyo kupitia muhtasari wa utafiti wake uitwao 'Nyota njema huonekana asubuhi', ambao ulilenga kukusanya maoni ya wananchi kuhusu huduma za afya zinazotolewa na serikali ya awamu ya tano.

Utafiti huo ni wa kwanza Afrika, wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi.

Matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wananchi waliohojiwa 1,836, kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara kati ya Mei 2 na 17, mwaka huu.

Akizungumza katika hafla ya utoaji ripoti hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla, alisema tatizo lililopo ni mfumo unaochochea kukandamizwa kwa sera ya huduma ya afya.

Dk. Kigwangalla alisema katika kuboresha huduma za afya, serikali ilizindua Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF), ambapo kwa wananchi wa vijijini, kaya yenye watu sita huchangia sh. 30,000, ambazo huwawezesha kupata huduma kwa mwaka mzima.

Aidha, kwa upande wa wakazi wa mijini, huchangia kati ya sh. 30,000 na sh. 40,000, ikitegemea mzunguko wa shughuli za kimaendeleo.

No comments:

Post a Comment