Saturday 27 August 2016

POLISI WADAIWA KUUA MAJAMBAZI 14 BAADA YA KUENDESHA OPERESHENI YA KUWASAKA KWA SAA NANE


RISASI za moto zimerindima na kuusimamisha mji wa Visiga, Mkuranga, mkoani Pwani kwa muda, wakati Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam pamoja na Polisi wa mkoa wa Pwani, walipokuwa wakifanya operesheni ya kukamata majambazi waliowaua askari wanne maeneo ya Mbande, Mbagala

Katika operesheni hiyo, askari mwandamizi, ASP Thomas Njiku, aliuwawa kwenye mapambano, baada ya kupigwa risasi ya kichwa na majambazi hao, ambao wanadaiwa walishiriki kwenye mauaji ya askari waliouwawa wakati wakibadilishana lindo kwenye benki ya CRDB iliyoko Mbagala, Dar es Salaam.

Taarifa za kuaminika ilizozipata gazeti hili zimeeleza kuwa, kikosi hicho cha polisi kilifanya operesheni ya kuwakamata majambazi hao kwa kushirikiana na polisi wa Pwani, kuanzia usiku wa kuamkia jana, kwenye eneo hilo, baada ya kupata taarifa za kiitelejinsia kutoka kwa raia wema kuhusiana na watu hao.

Hata hivyo, kulikuwepo na taarifa mbalimbali kuhusiana na idadi kamili ya majambazi hayo, ambayo Polisi Kanda Maalumu imesema itatoa taarifa rasmi leo kwa vyombo vya habari.

Hata hivyo,habari zingine zimedai kuwa majambazi 14, wameuawa
wakati wa operesheni hiyo.

Miongoni mwa wanaodaiwa kuuawa ni pamoja na jambazi sugu, ambaye anadaiwa kuwahi kupatiwa mafunzo ya ukomandoo.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alithibitisha kufanyika kwa operesheni hiyo, lakini alisema polisi itatoa taarifa rasmi kuhusiana na tukio zima kwa waandishi wa habari leo, kwa kuwa bado wapo kwenye operesheni.

"Bado tupo katika mapambano. Mapambano ni makali, kwa sasa siwezi kuzungumza chochote kuhusu tukio hili, nitalitolea taarifa hapo baadaye," alisema Kamishina Sirro. Mapambano hayo yalidumu kwa takribani saa nane mfululizo.

UHURU iliwasiliana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Injinia Hamad Massauni, ambaye alifika eneo la tukio na kujionea hali halisi, ambapo alisema taarifa itatolewa na polisi, lakini serikali inawapongeza askari walioshiriki operesheni hiyo ingawa baadhi yao wamepata matatizo.

Alisema Jeshi la Polisi limejiandaa vizuri kupambana na uhalifu na ndio maana ndani ya siku mbili, baada ya tukio hilo, wamepata taarifa sahihi kuhusiana na watu hao, ambapo waliamua kufanya operesheni hiyo na kwa kiasi kikubwa mafanikio hayo yanatokana na uwepo wa mifumo mizuri ya kiusalama.

"Tumejiandaa vizuri na tumebaini wahusika na tuna mifumo mizuri ya kiusalama na bahati mbaya kwa hilo lililotokea kwa askari wetu ni jambo baya, lakini tutapambana. Tunaomba Watanzania waendelee kutoa taarifa kwa polisi kila uhalifu wanaouona unataka kufanyika," alisema.

Aliwaomba wananchi wathamini juhudi za polisi, hasa kutokana na kufanya kazi kubwa ya kulinda usalama wa raia na huwa wanashiriki operesheni nzito, hivyo wasiwabeze au kutoa maneno ya kejeli, ambayo hayawezi kuwa sehemu ya kupambana na uhalifu.

TUKIO ZIMA LILIVYOTOKEA

Taarifa zilizopatikana katika eneo hilo zilieleza kuwa, ASP Njiku, alifika kwenye eneo hilo na kuwataka watu hao wajisalimishe, lakini kabla hajafika kwenye nyumba hiyo, majambazi hao walimpiga risasi iliyompata kwenye kifua na kufariki dunia.

ASP Njiku, ndiye alikuwa akiongoza kikosi cha askari polisi waliokwenda katika eneo ilipo nyumba hiyo kwa lengo la kuwakamata majambazi hao, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa raia wema.

Kwa mujibu wa watoa habari wetu, baada ya kuuawa kwa ASP Njiku,  polisi walijibu mashambulizi vikali huku askari wengine wakiwasili, wakiwa kwenye magari aina ya Land Rover, kwa ajili ya kuongeza nguvu, wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sirro.

Ilidaiwa kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu, lilipokea taarifa za kuwepo kwa watu waliohusika katika tukio la mauaji ya askari polisi wanne, waliokuwa wakibadilishana lindo katika Benki ya CRDB Mbande, Mbagala, kwamba wamejificha katika nyumba hiyo, hivyo kutuma kikosi kazi kilichoongozwa ASP Muniko kwa ajili ya kuwakamata.

Hatua hiyo ilisababisha kuanza kwa majibizano makubwa ya risasi kati ya polisi na majambazi hao.

"Baada ya mapambano kupamba moto, polisi waliongeza nguvu zaidi ya askari wake. Vikosi mbalimbali vya jeshi hilo vikiongozwa na Kamishina wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, viliwasili eneo la tukio na kuzidisha mashambulizi dhidi ya majambazi hao,"alisema mmoja wa mashuhuda.

Mabomu ya machozi na risasi za moto yalielekezwa kwenye nyumba hiyo na kuwafanya majambazi hao kuanza kutoka ndani ya nyumba hiyo huku wengine wakiuawa.

"Baada ya kuona wamezidiwa,  majambazi watano walijisalimisha mikononi mwa polisi na kutiwa mbaroni," alisema.

Habari hizo zinaeleza kuwa katika majambazi watano waliotiwa mbaroni, wapo watoto watatu.

Kwa mujibu wa taarifa, askari aliyefariki alikuwa kijana jasiri, mchapakazi na msomi, ambaye alikuwa anajiandaa kuchukua shahada yake ya pili ya sheria. Alihamia mkoani Dar es Salaam hivi karibuni akitokea mkoani Manyara.

No comments:

Post a Comment