Saturday 27 August 2016

CCM: HATUKO TAYARI KUONA DAMU IKIMWAGIKA

CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kimesema kitalinda na kutetea dhamana ilichokabidhiwa na wananchi na kamwe hakitakuwa tayari kuona damu ya Mtanzania ikimwagika kwa sababu ya uchochezi.

Kimesema wapo wanasiasa wanaofanya kazi za vibaraka kwa kuchochea maandamano kwa lengo la kuchafua taswira ya nchi, kisha kuwasiliana na vyombo vya nje ya nchi ili kujenga taswira kuwa, Tanzania sio kisiwa cha amani.

Kimesisitiza kuwa dhamira ya wanasiasa hao ni kufifisha juhudi za Rais Dk. John Magufuli, kuwaletea maendeleo wananchi, hivyo kimewaomba Watanzania kutounga mkono maandamano yaliyoitishwa na wapinzani, kwani yamepangwa kwa makusudi kwa lengo la kutotii maagizo halali ya vyombo vya dola.

Wakati CCM ikitangaza msimamo huo, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), limepinga maandamano yaliyotangazwa na CHADEMA na kupangwa kufanyika Septemba Mosi, mwaka huu, kwa kuwa hayana nia njema kwa Watanzania.

Akizungumza jana, kwenye Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam, Msemaji wa Chama, Christopher Ole Sendeka, alisema maandamano hayo ni mwendelezo wa vituko vya UKAWA kuwahadaa wananchi.

Alisema uhuru wa kujumuika, kutoa mawazo na kuabudu, ambao upo kwa mujibu wa katiba, umewekewa ukomo.

“Ibara ya 30, ibara ndogo ya kwanza ya katiba, inasema haki na uhuru wa binadamu, ambao misingi yake imeorodheshwa kwenye katiba hii, havitatumiwa na mtu mmoja kwa maana, ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki, uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma.

“Haki zote zitakoma pale ambapo zitaingilia haki au uhuru wa watu wengine, lakini uhuru huu lazima uwe na ukomo kama ambavyo, Mwalimu Julius Nyerere, alivyosema, uhuru bila demokrasia ni udikteta, lakini uhuru bila nidhamu ni fujo,” alisisitiza.

Ole Sendeka alisema uhuru huo haupaswi kutumika kama visingizio cha kile UKAWA wanachodai kwenda kuishitaki serikali kwa wananchi.

Kwa msisitizo huo, msemaji huyo wa Chama alisema, mikutano yoyote ya kisiasa, polisi wana mamlaka ya kuridhia kufanyika au kutofanyika kwake, kama ambavyo sheria ya vyama vya siasa inavyoelekeza.

Aliongeza kuwa, kwa mamlaka hayo ya polisi, hata mikutano ya kisiasa iliyopangwa kufanywa na CCM, imezuiliwa na Chama kimetii amri hiyo.

“Picha inayojengwa na upinzani ni kwamba, polisi wanatumia ubabe, mbona hata sisi (CCM), tumezuiwa kufanya mikutano hiyo na tumetii amri, lakini tunafahamu wapinzani kile wanachokitaka,”alibainisha.

Alisema ni aibu nchi kupakwa matope kwa madai ya kuendeshwa kidikteta wakati inaendeshwa kwa mujibu wa sheria.

Ole Sendeka alieleza kuwa, kauli na matendo ya upinzani ni mwendelezo wa vituko wanavyovifanya baada ya kuwasaliti wapigakura wao kwa kutoka bungeni, kuziba midomo, kugomea kuhudhuria misiba, kukataa kuwapa mikono viongozi wa serikali na sasa wanafanyakazi ya ukibaraka ili kuondoa tunu ya amani iliyopo.

“Walichobakisha ni kufanyakazi ya ukibaraka na kuchafua taswira ya nchi. Wamewasiliana na baadhi ya vyombo vya nje ili kuwaonyesha kuwa, Tanzania sio kisiwa cha amani.

“Mwingine jana, alisema tunajua wataandamana, watazuiwa, watapigwa, lakini tutahakikisha tunawapeleka kwenye mahakama ya kimataifa. Kazi hii inawezwa kufanywa na kibaraka pekee, asiyekuwa na uchungu kwa Watanzania,”alieleza.

Alisema Edward Lowassa, aliyezungumza maneneo hayo, anapaswa kukubali matokeo ya kushindwa uchaguzi mkuu, kwa kuwa alishindwa kukidhi sifa za kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM, lakini pia hakukidhi sifa ya kuongoza nchi alipowania nafasi ya urais kupitia CHADEMA.

Alibainisha kuwa Lowassa aliwaghiribu Watanzania kwa kuwaahidi atakibadilisha CHADEMA, kutoka chama cha wanaharakati na kuwa cha kisiasa, lakini matokeo yake, naye amekuwa mwanaharakati.

“Kama kweli Lowassa anaamini kuna kura yake aliyoibwa, alete ushahidi wa nakala ya matokeo inayokinzana na za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuonyesha alipata kura zaidi ya Rais Dk. Magufuli, lakini ni miezi minne tangu nilivyomtaka kufanya hivyo, hajawasilisha ushahidi,”alisema.

Alisema CCM itahakikisha Tanzania inaendelea kustawi, hivyo italinda dhamana iliyopewa na wananchi kwa gharama zozote.

Aidha, Ole Sendeka alisema CCM haiwezi kuingilia muhimili wa bunge kwa sababu, shughuli za uendeshaji wa bunge hilo zipo kwa mujibu wa kanuni husika.

Alisema hoja ya UKAWA kuwa, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, ameshika wadhifa huo kwa kazi maalumu, sio za kweli na kwamba, mbunge huyo aliteuliwa na rais kwa mujibu wa katiba.

Ole Sendeka pia, alitoa pole kwa familia za askari waliouawa kwa kupigwa risasi, Mbande, Dar es Salaam, ambapo alisisitiza kuwa wale wote waliohusika na tukio hilo wakamatwe.

Pia, alipongeza juhudi za maendeleo zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli, ikiwemo kuboresha miuondombinu ya reli, ununuzi wa ndege tatu mpya na za kisasa za abiria, pamoja na utoaji elimu bure kulikowawezesha watoto wa masikini kusoma bila michango.

Msemaji huyo wa Chama, aliwaomba viongozi wa chama cha CUF, kuacha malumbano kwani CCM inategemea upinzani imara ili kushindana kwenye majukwaa ya kisiasa.

TUCTA WATOA MSIMAMO
Wakati huo huo, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), limepinga maandamano yaliyotangazwa na CHADEMA na kupangwa kufanyika Septemba Mosi, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es salaam, jana, Rais wa TUCTA, Gratian Mukoba, alisema maandamano hayo hayana dalili nzuri kwa mustakabali wa amani ya taifa kwani yanaweza kusababisha machafuko.
“Hatuwezi kukaa kimya kusubiri machafuko kwani hayabagui na yataathiri jamii nzima, wakiwemo wafanyakazi na familia zao.
Mojawapo ya majukumu ya shirikisho ni kuhakikisha wafanyakazi kote nchini wanafanya kazi kwenye utulivu na amani,”alisema Mukoba.

Aidha, alimwomba Rais Dk. John Magufuli, alegeze msimamo wake na kukubali kukaa na viongozi wa vyama vya siasa, kwa lengo la kupata mwafaka wa kitaifa.

Hata hivyo, alisema dhamira aliyonayo Rais juu ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo Tanzania, haitaweza kufanikiwa kama kutakuwa na malumbano ya kisiasa nchini.

No comments:

Post a Comment