Thursday 25 August 2016

MIKUTANO YA NDANI YA KISIASA YAPIGWA MARUFUKU

JESHI la Polisi nchini, limepiga marufuku mikutano yoyote ya ndani ya vyama vya siasa kwa kuwa  inatumika  kuwahamasisha wananchi kuvunja sheria.

Kamishna wa  Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo nchini, Nsato Mssanzy, aliwaambia waandishi wa habari, Dar es Salaam, jana, kutokana na hali ya kisiasa ilivyo nchini, ni marufuku kwa  chama chochote cha siasa kufanya mikutano ya ndani.

“Mikutano hii inahamasisha wananchi  kuvunja sheria na mingi ina viashiria vya uchochezi,”alisema  Kamishna Mssanzy.

Alisema hata kama mikutano hiyo ikifanyika jukwaani, polisi watamshusha muhusika na kumfikisha kwenye mkono wa sheria.

“Uchunguzi umeonyesha kuwa, mikutano hiyo ya ndani imekuwa ikitumika kuhamasisha mapambano dhidi ya polisi, hili halitavumilika,”Kamishna huyo, alionya.

Alisema pia kuwa mikutano hiyo imekuwa  ikitumika  kugawa  vifaa vya kufanyia uhalifu  wa kijinai na kutoa tahadhari  kwa viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama hivyo  kutii agizo hilo.

“Yeyote atakayefanya mikutano ya ndani, bila kujali  ni wa chama gani, atakamatwa na kushitakiwa kwa mujibu wa sheria,”alisema Kamishna Msanzy.

Akizungumzia tukio la kuuawa kwa Polisi lililotokea Mbagala, Mssanzy, alisema pamoja na kuwa na taswira ya ujambazi, lakini pia jeshi hilo linafanya uchunguzi  wa kina kuona kama linahusika na vuguvugu za kisiasa zinazoendelea hapa nchini.

"Katika tukio hilo, majambazi ambao idadi yao haikufahamika, walifanikiwa kupora silaha mbili aina ya SMG na risasi 60, lakini hakuna pesa wala mali ya benki hiyo kuibwa au kuharibiwa. Ni dhahiri kuwa wahalifu hao walikuwa na kusudio moja tu la kuwashambiulia askari polisi," alisema.

Alisema baada ya tukio hilo, kuna baadhi ya watu waliandika mitandaoni kubeza na kukeji mazoezi ya kawaida ya polisi na wengine waliandika ujumbe wa kushabikia tukio hilo la kuuawa kwa askari.

“Wengine walidiriki kuandika ujumbe unaosema, endapo watapigwa na polisi Septemba mosi, mwaka huu, basi viongozi wa jeshi hilo wawaondoe askari wanaoishi uraiani na kuwarudisha kambini,”alisema

Aliongeza kuwa, polisi wamejipanga vyema kukabiliana na matukio yote ya uvunjifu wa amani nchini, hususan maandamano ya UKAWA yaliyopangwa kufanyika Septemba mosi mwaka huu.

No comments:

Post a Comment