Thursday 25 August 2016

ATAKAYEVAMIA MSIMU WA MFILI JELA MIAKA SABA, FAINI MIL. 70/-

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema mtu atakayevunja sheria kwa kuvamia na kuharibu mazingira ya msitu wa Mfili, ambao ndiyo chanzo pekee cha maji cha wilayani ya Nkasi, atatozwa faini ya sh. milioni 70 pamoja na kifungo cha miaka saba jela.

Katika kuhakikisha hatua zinachukuliwa, Waziri Mkuu amemkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Said Mtanda, kitabu cha sheria kitachomuongoza katika kuwachukulia hatua wale  wote watakaobainika kufanya uharibifu katika chanzo hicho cha maji.

Waziri Mkuu Majaliwa, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Namanyere, katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi, kwenye viwanya vya Sabasaba.

“Mkuu wa wilaya akishindwa kuwachukulia hatua za kuwaondoa wananchi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria watu wote waliovamia maeneo ya hifadhi za misitu na kuanzisha makazi au kufanya shughuli za kijamii, naye atakuwa jipu,” alisema.

Majaliwa alisisitiza kuwa, maeneo mengi nchini yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji, baada ya wananchi kuvamia katika vyanzo vya maji na kufanya shughuli za kibinadamu, hivyo kusababisha vyanzo vingi kukakuka.

“Serikali haitakubali kuona mtu anaharibu chanzo cha maji. Wananchi mnatakiwa kuwa walinzi wa maeneo hayo na atakayekutwa anachunga mifugo, analima, kukata nyasi au kufanya shughuli zozote za kijamii ndani ya maeneo hayo, atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” alieleza.

Awali Waziri Mkuu alikagua mradi wa upanuzi wa bwawa la maji la Mfili, ambalo mwanzo lilikuwa na ujazo wa lita 1,500, lakini kwa sasa likikamilika, litakuwa na ujazo wa lita 248,067, hivyo kuwezesha wakazi 82,689 kunufaika.

Akizungumza kwenye eneo la mradi baada ya Waziri Mkuu kuwasili, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Nkasi, Julius Kaondo, alisema hadi mradi huo kukamilika, unatarajiwa kugharimu sh. trilioni 1.011, ambapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji imetoa sh. milioni 500 na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) itatoa sh. milioni 500.

Kaondo alisema mradi unakabiliwa na changamoto ya ukosefu  wa umeme pamoja na mitambo ya kusukuma maji kwa kutumia nishati ya umeme, ambapo aliiomba serikali kuisaidia halmashauri zaidi ya sh. milioni 220, ikiwa ni gharama za kupeleka umeme kwenye eneo la mradi na kununua mitambo.

Mbali na kutembelea mradi wa upanuzi wa bwawa, pia Majaliwa alitembelea hospitali teule ya wilaya ya Nkasi na kuzindua wodi mpya yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 72 kwa wakati mmoja.

No comments:

Post a Comment