Thursday 25 August 2016

MADIWANI SABA WATUPWA JELA MIEZI SITA



MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Simiyu, imewahukumu kwenda jela miezi sita, washitakiwa saba waliokuwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, kwa kosa la kumfungia ndani aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo.

Mbali na hukumu hiyo, watuhumiwa hao wametakiwa kulipa faini ya sh. 1,000, kila mmoja huku kifungo hicho kikienda kwa pamoja na kila mmoja kutakiwa kutumikia kifungo cha miezi sita jela.

Waliokumbwa na adhabu hiyo ni Mlyandingu Cheyo, ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa halmashauri, Tano Shigilu, Bulikinda Madeleke, Mbuke Mlyandingu, Ntundu Mboyi, Dotto Adam na Nicodemas Ndaki.

Katika kesi hiyo namba 148 ya jinai ya mwaka 2015, upande wa mashitaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Moses Mafuru, ulisema washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa sita.

Hata hivyo, wakili huyo hakuweza kusoma makosa hayo mbele ya mahakama chini ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, John Mkwabi, ambapo alieleza upande wa mashtaka upo tayari kusikiliza hukumu.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi, John Mkwabi, alichukua saa moja na nusu na kusema kuwa, katika maelezo ya makosa yote sita yanayowakabili washitakiwa, yalikuwa yakifanana, hali iliyofanya yachambuliwe na kubaki makosa matatu.

Alisema kosa la kwanza ni kufanya vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani kinyume na sheria namba 5 na 8 kifungu 385 ya kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambapo washitakiwa walidaiwa kwa pamoja Oktoba 6, 2014, katika ofisi za halmashauri hiyo, walimtishia kwa maneno aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa halmashauri,  Rogers Shemwelekwa.

Kosa la pili ni kufanya vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani kinyume na sheria namba 5 na 8 ya kifungu 384 cha kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambapo wanadaiwa kwa pamoja tarehe hiyo katika ofisi za halmashauri hiyo, walimtishia kwa maneno Mwanasheria wa halmashauri, Engleberth Kalekona.

Kosa la tatu ni vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani kinyume na sheria namba 5 na 8 kifungu 385 cha kanuni ya adhabu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambapo wanadaiwa kwa pamoja walifunga ofisi za halmashauri kwa kufuli.

Hakimu huyo alieleza kuwa, mahakama imetupilia mbali utetezi wa upande wa washitakiwa na kubaini ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa na ukweli, hali iliyoonyesha washitakiwa walitenda kosa kwa nia ovu.

Mkwabi alisema mahakama imewatia hatiani washitakiwa wote saba kwa makosa yote matatu, ambapo walihukumiwa kwenda jela miezi sita kwa kila mmoja na kulipa faini ya sh. 1,000 kila mmoja.

No comments:

Post a Comment