Monday, 24 July 2017

WAMEANZA KUTAPIKA FEDHA WALIZOKULA-JPM


RAIS Dk. John Magufuli, amesema mafisadi na wala rushwa wameanza 'kuzitapika' fedha walizozichukua na kwamba, tumbuatumbua dhidi yao itaendelea bila kujali sura wala rangi ya mtu.

Kauli hiyo aliitoa jana, wilayani Kaliua mkoani Tabora, alipokuwa akizindua barabara yenye urefu wa kilometa 56, kutoka Kaliua-Kazilambwa, iliyojengwa kwa kiwango cha lami.

Rais Magufuli alisema fedha zilizoliwa na mafisadi zipo nyingi na kwamba, kwa sababu ya kuwabana waliozitafuna, wameanza kuzitapika na zinapelekwa kwenye maendeleo ya jamii.

Alisema katika serikali anayoiongoza, atakuwa mkali kwa kusimamia na kuweka nidhamu kwa watendaji ili watekeleze majukumu yao vile inavyotakiwa.

"Tunataka watu waliozoea kuiba mali za watu wanyonge, walizoea kutumbua mali za maskini, sasa ni zamu yao kutumbuliwa.  Nataka rushwa iwe historia. Tumeanzisha mahakama ya kupambana na wala rushwa, tutawashughulikia kikamilifu wala hatutawaogopa," alisisitiza.

Rais Magufuli alisema wala rushwa wa Tanzania wapo ndani ya serikali, vyama vya siasa vya CCM, CHADEMA, CUF na wengine hawana vyama, lakini wote watashughulikiwa.

Vilevile, alisema wala rushwa wapo wa kila aina, wakiwemo wazungu kwa sababu wanakuja Tanzania kwa ajili ya kuiba, hivyo atawatumbua kama avyowatumbua waathirika.

"Tukifanya mchezo, nchi yetu itaendelea kuwa wasindikizaji, wakati nchi yetu ni tajiri, ina kila kitu, hatutakiwi kupewa misaada, tunatakiwa kuwapa msaada wao," alisema.

Aliongeza: "Ninaomba sapoti yetu wananchi wa Kaliua pamoja na sala zenu za kuniombea kwa sababu hii ni vita kubwa."

Akizungumzia matukio ya wazee na vijana wanaowapa mimba wanafunzi, alisema wajiandae kufungwa jela miaka 30.

"Nguvu zao nyingi wakazitumikie wakiwa gerezani. Tunataka Watanzania wasome, ndiyo marais wa kesho," alisema.

UJENZI WA BARABARA

Akizungumzia ujenzi wa barabara ya Kaliua-Kazilambwa kwa kiwango cha lami, alisema umetumia gharama kubwa, hivyo wananchi wanapaswa kuitunza.

"Ujenzi wa barabara una gharama kubwa ndugu zangu. Kilomita moja huwa inajengwa kwa zaidi ya sh. milioni 1,000, ndiyo maana katika kilomita hizi 56, zimejengwa kwa sh. bilioni 61.87. Fedha hizo zote zimetolewa na serikali, hakuna mtu tuliyemuomba," alisema.

Rais Magufuli alisema iwapo wasafirishaji wa mazao watazidisha mizigo ya tumbaku, mahindi na mchele, barabara hiyo haitadumu, itafika mahali itabaki historia.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya barabara ya mwaka 2007, kifungu namba 13, tani zinazotakiwa kusafirishwa ni 56, sio vinginevyo.

"Niwaombe madereva na watumiaji wote, msizidishe uzito usiokubalika kwa mujibu wa sheria," alisema.

Vilevile, aliwaomba wananchi ambao wanaishi karibu na barabara hiyo, kutochimba kokoto kandokando ya barabara, kwani imewekewa hifadhi ambayo ni mita 25 kila upande.

Alimuagiza Meneja wa TANROADS mkoani Tabora,  kuwabomolea bila kusubiri maelezo, wale wote ambao wanajenga ndani ya hifadhi ya barabara.

"Niwaombe wasimamizi wa barabara, akiwemo meneja, ukiona nyumba inajengwa ndani ya hifadhi ya barabara, bomoa bila kutoa taarifa kwa sababu sheria ni lazima tuzizingatie," alisema.

Kuhusu nyumba zilizojengwa kando ya reli, alisema katika kuzingatia sheria, wanaanza kuzibomoa nyumba hizo kwa sababu ni lazima ziondoke.

"Ninazungumza hivi kwa sababu mimi ni rais wa nchi hii, mmenichagua ili nisimamie ukweli. Tupo kwenye mpango wa kujenga reli ya kisasa na kimataifa, kutoka Dar es Salaam, Tabora, Kaliua hadi Kigoma," alisema.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi ambao wamejenga kando ya reli, kujiandaa kisaikolojia kwa kupisha eneo la reli. "Mimi katika kusimamia sheria huwa sipindishi, ninajua kufuata sheria ni kitu kigumu sana," alisema.

Alisema anafahamu Kaliua kuna wanasiasa, ambao wengine ni wana-CCM, wanawashawishi wananchi waliojenga kwenye maeneo ya hifadhi wasibomoe nyumba zao, hivyo aliwataka wasimamizi wa barabara kuanza na nyumba hizo ili walale nje.

"Mimi ndiye mwenyekiti wa CCM na sheria ni msumeno, wengine walikuwa viongozi wakubwa tu, wanawashawishi wananchi, mimi nasema bomoa," alisisitiza.


PROFESA MBARAWA APEWA MAAGIZO

Rais Magufuli, alisema ameamua kutoka Kigoma hadi Kaliua kwa barabara ili kuangalia vipande vilivyobaki, ambavyo havijawekwa lami.

Kutokana na hali hiyo, alimuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja, anaweka mkandarasi katika barabara kutoka Kaliua-Urambo (km 28) ili kutengenezwa kwa kiwango cha lami.

"Nataka ndani ya mwezi mmoja, maana yake mwezi Agosti usiishe, pawe na kandarasi kwenye barabara hiyo iliyobaki ya Kaliua-Urambo. Nafikiri Profesa umenielewa. Nataka wananchi wa Kaliua wafurahi na fedha zipo, hata akianza leo, njoo uchukue," alisema.

Kuhusu barabara ya Kazilambwa-Chagu yenye urefu wa kilomita 42, alisema wanatakiwa kuanza maandalizi ili nayo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Akizungumzia barabara ya Chanya-Nyaua ya kilomita 84, alisema kilomita hizo haziwezi kuishinda serikali ya awamu ya tano. Alisema ameshazungumza na Mfalme wa Kuwait, ambaye aliahidi kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo.

"Kwa sababu fedha ipo, natoa siku 45, kwenye barabara hiyo kuwe na mkandarasi, ambaye atajenga kwa kiwango cha lami. Najua wengine mtasema haya ni maneno ya siasa, mimi sifanyi siasa, mimi nafanyakazi. Hakikisha waziri, mkandarasi anaanza kazi mapema," alisema.

Awali, Waziri Mbarawa alisema barabara hiyo ni muhimu kwa mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.

Pia, alisema barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya kutoka Kigoma (km430), inayounganisha wananchi wa mkoa wa Tabora na Kigoma na nchi jirani za Burundi na Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.

Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya, alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa za kuwatetea wananchi na kupigania rasilimali za Watanzania.

Alisema barabara hiyo ni muhimu na ina faida kubwa kwa uchumi wa wananchi wa Kaliua, kwa sababu kazi yao ni kilimo.

"Barabara hii itatusaidia sana kuweza kuongeza uchumi wa Kaliua na pia kuongeza uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja," alisema.

Vilevile, alimkumbusha Rais Magufuli ahadi yake aliyoitoa ya kuweka lami katika mji wa Kaliua (km 5).

"Mheshimiwa Rais, ile ahadi yako uliyotuahidi pamoja na kilomita mbili, ambazo aliahidi Rais wa awamu iliyopita (Jakaya Kikwete), tuzipate ili mji wetu uweze kuwa mzuri," alisema.

No comments:

Post a Comment