Monday 24 July 2017

MWINGINE AUAWA KWA RISASI YA KICHWA KIBITI


LUCAS Mulungu, ameuawa kwa kupigwa risasi ya kichwa huko Bungu ‘B’ maeneo ya Kibwibwi, wilayani Kibiti mkoani Pwani na watu wasiojulikana.

Taarifa za awali zimedai kuwa, Mulungu mbaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa kitongoji cha Kibwibwi, aliuawa akiwa nyumbani kwake usiku wa kuamkia jana.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, marehemu alivamiwa na watu watano, ambao mwanzo waligonga kwa mke mkubwa, akawaambia yupo kwa mke mdogo, ambapo walimkuta na kumpiga risasi.

Wakizungumza na Uhuru, jana, wakazi wa Kibiti, Zaina Ally na Seif Abdullah walisema marehemu alikuwa na wake watatu.

"Eneo hilo la Kibwibwi sio zuri, kwani lilikuwa likitajwa kuwa wauaji hulitumia kujificha, hivyo tunaomba jeshi la polisi lipaangalie," walisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jonathan Shana, alisema jana kuwa, bado wanafuatilia tukio hilo na watatoa taarifa baadaye.

Kwa hatua nyingine, Kamanda Shana, alisema wanawashikilia watu sita kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba za watu watatu.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Omary Athumani (42), Abdallah Shomari (53), Seif Shomari (38), Uzalimala Selasela (36), Salum Shomari (40) na Jumanne Omary (49), wote wakazi wa Vikumburu, wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.

Alisema watuhumiwa hao wanadaiwa kuchoma moto nyumba ya Joseph Simbayi (55), Rebeka Yona (23) na Selina Simon (28).

"Mbali ya kufanya uharibifu huo, pia waliingia kwenye mazizi na kukatakata mifugo na kuchukua  nyama na vichwa huku wakiacha utumbo. Idadi ya mifugo haijulikani," alisema.

No comments:

Post a Comment