Monday, 24 July 2017
MAJALIWA AIAGIZA TAKUKURU KUWAKAMATA VIGOGO WANNE
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU), kumkamata na kumuhoji Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbozi na wakuu wa idara wengine watatu kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.
Watendaji hao waliosimamishwa kazi na Waziri Mkuu ili kupitisha uchunguzi wa TAKUKURU ni Elisey Mgoyi, ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Simon Noeli, ambaye ni Mhasibu, Bahati Chomoka, ambaye ni mwandikaji na mwandaaji wa hundi za malipo na Ofisa Manunuzi, Remmy Haule.
Pia, amesema kuanzia sasa, watendaji hao amewasimamisha kazi na kuitaka TAKUKURU ikimaliza kuwahoji, wampe taarifa kwa kuwa serikali inazo taarifa lukuki kuhusiana na halmashauri hiyo kujaa rushwa na ufisadi.
Waziri Mkuu alitangaza uamuzi huo jana, katika ukumbi wa shule ya sekondari Vwawa, wilayani Mbozi, mkoani Songwe, ambapo alisema halmashauri hiyo imekuwa kichaka cha mafisadi kwa watendaji.
Alisema madiwani na wakuu wa idara wamegawanyika na hata kushindwa kufanyakazi zao vyema za kuwatumikia wananchi, ambapo aliwaonya na kuwataka kubadilika.
"Tufanyekazi kama timu na lazima tuhakikishe tunasimamia vyema fedha za miradi pamoja na kuhakikisha fedha za mapato ya ndani zinatumika vyema na madiwani simamieni hili," alisema.
Alisema diwani anapaswa kuwa msimamizi na mshauri wa kila kitu ndani ya halmashauri, lakini kwa Mbozi, hali ni tofauti kutokana na kuwepo kwa ufisadi na rushwa inayofanywa na watendaji huku madiwani wakishindwa kuwakemea.
"Halmashauri imegawanyika na ina tuhuma nyingi za rushwa. Mnadhani hatujui, mnajidanganya mno. Haya, ofisa manunuzi yuko wapi na aje mbele sasa hivi," aliagiza Waziri Mkuu, ambaye baada ya kubaini kwamba, hakuwepo mkutanoni, aliagiza atafutwe mara moja.
Baadaye Waziri Mkuu Majaliwa alimuhoji Kaimu Mkurugenzi, Mgoyi kuhusiana na utengenezaji wa magari ya halmashauri huku akitaka kuelezwa mahali yanakotengenezwa.
Swali hilo lilimfanya Mgoyi kubabaika kulijibu na kuomba aulizwe Mhasibu wake, Noel, kwa madai kuwa ndiye anayezifahamu gereji zinazotumika kutengeneza magari ya halmashauri hiyo.
Waziri Mkuu Majaliwa pia alimwita Mwandikaji wa hundi, Chomoka na kumuuliza iwapo Kampuni ya Umbwila imeandikishwa kama gereji au duka la kuuza vipuri vya magari, ambapo alijibu kuwa ni duka la vipuri.
Chomoka alishindwa kujibu maswali mengine aliyoulizwa na Waziri Mkuu kutokana na kubabaika na kujikanganya, likiwemo lile la ulipaji wa malipo hayo kwa kampuni hiyo na nyinginezo unavyofanyika.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu alimuinua Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ambakisye, ambaye alisema anazo taarifa zake kuhusiana na jambo hilo, aliyedai kuwa kila kitu kinafanywa na watendaji hao.
Jibu hilo lilimkera Waziri Mkuu, ambaye alisema hakulikubali na utaratibu huo na kumtaka awe makini kwa kuwa ufisadi unaoendelea katika halmashauri hiyo, utaweza kumuharibia safari yake ya kisiasa kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
"Wewe jifanye mjanja kwa kuruka, ila mimi ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama, naweza kuchukua kadi yetu na tuone unafanyeje sasa? Nakuagiza isimamie halmashauri vizuri," alisema.
Alimuagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Songwe, Damas Sutta, kuwakamata Noel, Haule, Mgoyi na Chomoka kwa kosa la kuipa tenda ya utengenezaji wa magari kampuni ya vipuri vya magari na kuwasimamisha kazi hadi uchunguzi utakapomalizika.
Uhuru ilipata taarifa kuwa, Kampuni ya Umbwila ni moja ya kampuni zinazolipwa fedha nyingi kwa kazi ya kutengeneza magari ya halmashauri hiyo, huku ikiwa haina sifa za utengenezaji magari. Kampuni zingine ni Julius Diesel, Kasaba na Mtoni Garage.
Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa TAKUKURU mkoani humo, Sutta alisema maagizo ya Waziri Mkuu wanaanza kuyatekeleza mara moja kwa kuwakamata wahusika na kuwahoji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment