Monday 24 July 2017

WANAOMKEJELI JPM SASA KUKIONA CHA MOTO-MWIGULU

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema wanasiasa wanaotoa kauli za uchochezi na kuendelea kumkejeli Rais Dk. John Magufuli, sasa watakumbana na mkono wa sheria.

Amesema kuwa sio kila kauli ni siasa na kwamba, maisha ya Watanzania hayahitaji siasa uchwara kwani ulinzi na utetezi wa rasilimali za taifa, hauna chama, bali unahitaji uzalendo, hasa katika wakati huu, ambao serikali inapambana kuinua uchumi.

Waziri Nchemba alisema hayo mwishoni mwa wiki, jijini hapa, wakati wa hafla ya kuchangia fedha za ujenzi wa kituo cha luninga, redio na studio ya kurekodi nyimbo ya Gombo, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Belmont Fairmont.

Kituo hicho kilichoasisiwa na marehemu Askofu Moses Kulola, kitasaidia kutangaza Injili ya Kanisa la EAGT Jijini Mwanza.

Waziri Nchemba alisema tayari serikali imeanza kuwachukulia hatua mbalimbali watuhumiwa wa ufisadi na wahujumu uchumi kwa vile wamekuwa wakirudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Nchemba, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi (CCM), alisema viongozi wa dini, watumishi wa Mungu na Watanzania wote, waendelee kumuombea Rais Dk Magufuli, wakati huu akiwa kwenye mapambano hayo ya kiuchumi ili rasilimali hizo ziwanufaishe Watanzania wote na kuwaletea maendeleo.

Alisema katika siku za hivi karibuni, wameibuka baadhi ya watu na wanasiasa uchwara, wanaotumia maneno yenye viashilia vya uchochezi, kubeza na kumdhalilisha Rais na serikali ya awamu ya tano, licha ya juhudi zinazochukuliwa kusimamia, kutetea na kulinda rasilimali za taifa.

“Hao watakutana na mkono wa sheria maana sio kila kauli ni za kisiasa. Maisha  ya Watanzania hayana siasa, hivyo ni vyema kabla ya kuzitoa kauli hizo, wazitafakari kama zina tija kwa wananchi,” alisema na kusisitiza:

“Hakuna siasa katika kulinda rasilimali zote za taifa, bali ni jukumu la Watanzania kuweka kando tofauti za kiitikadi na kushirikiana na serikali iliyopo madarakani kuzilinda.

"Kundi au watu wanaopanga maneno ya uchochezi ili wavuruge amani na utulivu uliopo nchini na kutaka kuwagawa Watanzania, kwa nmna yoyote ile watashughulikiwa kisheria.”

Alieleza kuwa serikali imejidhatiti kukabiliana nao, hasa wakati huu ikipambana na vita ya kiuchumi kwa kuwa tayari vita ya uhuru iliishamalizika.

“Wanaoshabikia na kutoa kauli za kuunga mkono mauaji yanayoendelea kufanywa na wahalifu maeneo ya Kibiti mkoani Pwani, pia tutawakamata. Tunawahesabu kama wahalifu na tutawafikisha katika mkono wa sheria.
Katika suala hili, serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani tutahakikisha tunalisimamia kwa nguvu zote,” alisema.

Awali, mtoto wa marehemu Askofu Kulola, Willy Kulola, ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Gombo Television Network cha Mwanza, kinachomilikiwa na Kanisa la EAGT, alisema ujio wa Waziri Nchemba ni utekelezaji wa  maagizo ya marehemu baba yake.

Mjane wa marehemu, Elizabeth Kulola alisema aliagizwa kumkabidhi vitu mbalimbali Waziri Nchemba ili kuvinadi na kuendesha harambee kwa ajili ya kusaidia ufanikishaji wa ujenzi wa kituo hicho. Alimpongeza kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kutekeleza agizo hilo.

No comments:

Post a Comment