Wednesday, 30 September 2015

UVCCM YAVIONYA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA PEMBA





NA MWANDISHI WETU

UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM),  umevionya vyombo vya ulinzi na usalama kisiwani Pemba, kuacha kushabikia siasa na kwamba ikibidi, utaviweka hadharani pamoja na maofisa wao wanaotuhumiwa kufanya hivyo.

Umesema amani ya Pemba ni muhimu kwa Tanzania nzima na kwamba, umoja huo hautafumba macho kuona wananchi hususan wana-CCM wakifanyiwa uonevu na kunyanyaswa ndani ya nchi ambayo dola yake inaundwa na Chama chao.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea ubunge wa CCM, katika jimbo la Wawi, Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema umoja huo umepokea taarifa za kuwepo matukio ya kushambuliwa kwa wana-CCM wanaporudi kutoka kwenye mikutano ya kampeni huku vyombo hivyo vikishindwa kuchukua hatua stahiki.

Shaka alisema miongoni mwa matukio ya hivi karibuni ni pamoja na lile la wana-CCM kushambuliwa kwa mawe wakati wakitoka kwenye mkutano wa kampeni, tukio lililohusishwa na wafuasi wa chama cha CUF.

Mbali na tukio hilo, alisema lingine ni lile la wana-CCM kushambuliwa katika mazingira kama hayo na kusababisha majeruhi.

“Licha ya matukio hayo kuripotiwa, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Na licha ya kutochukuwa hatua, tunazo taarifa kwamba baadhi ya maofisa wa vyombo vinavyostahili kushughulikia tatizo hilo, wamekuwa wakiwasaidia wapinzani katika kutekeleza uhalifu huo.

“Tunalaani vikali hatua hiyo. Tunawataka maofisa hao kutambua kuwa tunawafahamu, tena kwa majina na tutakapolazimika, tutawataja hadharani kwa kuwa hawana nia njema na amani na usalama wa Pemba na Tanzania kwa ujumla,” alisema Shaka.

Kwa mujibu wa Shaka, inasikitisha kuona CUF kwa maelekezo ya mgombea urais wake wa Zanzibar, Maalim Seif Sharifu Hamad, wameanza kuonyesha dalili za kutaka kurudisha siasa za mwaka 1995 katika kisiwa hicho.

Alisema wafuasi wa CUF wameanza kufanya vitendo visivyo vya kistaarabu, ikiwa ni pamoja na kutaka kutengana kwenye baadhi ya matukio ya kijamii ikiwemo ibada.

Hata hivyo, Shaka alisema CCM na serikali yake ziko imara kulinda usalama wa raia wote wa Tanzania, wakiwemo wananchi wa Pemba na kuwataka wana-CCM visiwani humo kutoogopa chochote kwa kuwa yeyote atakayebainika kuchochea vurugu atachukuliwa hatua za kisheria.
“Msiwe wanyonge wala kuhofia chochote, nyie ndio wenye chama kinachoongoza serikali hii, shirikini kwenye matukio yote ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kuhudhuria mikutano ya kampeni bila ya kuhofia jambo wala mtu yeyote,” alisema.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Daudi Ismail, alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, hakuna namna ambayo itaifanya CCM kutoshinda kwa kuwa imefanya mambo makubwa yanayoridhiwa na wananchi.

Daudi alisema CCM imefanikisha usambazaji umeme karibu jimbo zima, ujenzi wa barabara ya lami pamoja na kuboresha huduma mbalimbali ambazo awali zilikuwa zikilalamikiwa na wananchi.

Kwa mujibu wa Daudi, endapo wananchi watamchagua kuwa mbunge wao katika jimbo hilo, amejipanga kuboresha elimu, ikiwemo kujenga majengo zaidi na ya kisasa katika Shule ya Sekondari Fidel Castro.

Katika hatua nyingine, mgombea ubunge wa jimbo la Chakechake kwa tiketi ya CCM, Suleiman Mattar, amemshutumu Maalim Seif na kusema si mtu mkweli na hakuwa na nia njema ya kuyakubali na kutekeleza kwa vitendo  maridhiano ya kisiasa yaliounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, mwaka 2010, chini ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

No comments:

Post a Comment