Na Clarence Chilumba, Mtwara
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Lindi, Mhashamu
Bruno Ngonyani, amewataka Watanzania kudumisha amani iliyopo kwa kuchagua
viongozi wenye uadilifu na watakaotenda haki na usawa kwa watanzania wote.
Alitoa wito huo juzi, wakati akiongoza Ibada ya
kufunga mwaka kwa familia za Kikristo, iliyofanyika kwenye viwanja vya Chuo
Kikuu cha SAUTI, tawi la Mtwara na kuhudhuriwa na waumini kutoka majimbo saba
yanayounda Kanda ya Kusini.
Alisema amani ni kitu muhimu kwa ustawi wa Taifa
na kwamba amani hiyo hutoweka pindi yanapotokea machafuko huku waathirika
wakubwa wakiwa kinamama na watoto.
Alisema mwaka huu ni wa kipekee katika historia ya
siasa za Tanzania kwani, wananchi wa rika mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kwa
wingi kushiriki kwenye mikutano ya kampeni huku akiwaomba kuchagua kiongozi atakayekuwa
na sera nzuri kwa taifa.
“Wananchi mnapaswa kupima ahadi zinazotolewa na
wagombea wa vyama vyote vya siasa kama zinatekelezeka au hazitekelezeki ili
siku ya kupiga kura, mfanye maamuzi sahihi kwa kumchagua kiongozi aliyetoa
ahadi zinazotekelezeka,” alisema Ngonyani.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Kanisa, wananchi
wenyewe nao wanapaswa kutendeana haki huku akiiomba serikali nayo kutenda haki
kwa raia wake katika kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuwa ni jukumu la serikali
kufanya hivyo.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Johansen Bukwali,
alisema jambo la muhimu ni kudumisha familia na amani kwa kutii utawala
uliopo na kutekeleza kanuni zilizopo ili uchaguzi uwe huru na wa amani kwani
baada ya uchaguzi, maisha yanaendelea.
No comments:
Post a Comment