NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, ameonya kuwa mawakala
wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuingilia kazi za watendaji wa uchaguzi waliopo
vituoni.
Hata hivyo, amesema mawakala hao wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kupigiakura kwani hilo ni jambo muhimu na linalodhihirisha uwazi katika uchaguzi.
Kandoro aliyasema hayo jana, wakati akifungua mafunzo
kwa waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi, maofisa na wasimamizi wasaidizi
wa uchaguzi ngazi ya jimbo kutoka mikoa ya Iringa na Mbeya.
Mafunzo hayo yanafanyika kwenye ukumbi wa mikutano
uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Alisema watendaji wanapaswa kufanya mambo yote kwa
uwazi na kuwashirikisha mawakala wa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria na
taratibu zilizopo, ili kuepusha malalamiko yasiyo na msingi.
“Wajibu wa mawakala wa vyama vya siasa ni kuangalia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na tume zinazingatiwa katika mchakato mzima wa kupigakura hadi kutangaza matokeo,” alisema Kandoro.
Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri za mikoa ya
Mbeya na Iringa, kuhakikisha wanavihakiki vifaa na fomu mbalimbali
watakazokabidhiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ili kuona kama vinakidhi
mahitaji na viko sahihi.
Kandoro alisema katika uchaguzi mkuu uliopita, miongoni mwa matatizo yaliyojitokeza, ambayo yanawahusisha moja kwa moja watendaji hao wa uchaguzi ni pamoja na kutohakiki vifaa na fomu hizo hivyo kusababisha uchaguzi kuahirishwa katika baadhi ya kata na majimbo.
No comments:
Post a Comment