Sunday 6 August 2017

WAASISI CUF WAMTOLEA UVIVU MAALIM SEIF


WAASISI wawili wa CUF, wamesema Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, hatakubalika kikatiba kukiongoza chama hicho kwa sababu ni dhaifu na wakala hatari wa ustawi wa umoja na mshikamano Afrika Mashariki.

Wamesema mwanasiasa huyo ni mgeni mwalikwa ndani ya CUF, ambaye kwa maelekezo ya anaowatumikia, amekuwa akifukuza wanachama kwa mizengwe na ni dikteta kwa waasisi na viongozi wa chama wanaopinga fikra na matakwa yake ili afikie malengo yake.

Msimamo huo ulitolewa  jana, kwa nyakati tofauti na muasisi wa chama hicho, Mussa Haki Kombo na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa kwanza wa CUF (Zanzibar), Nassor Seif Amour.

Kombo alisema kwa muda mrefu mwanasiasa huyo amekuwa akiwaondoa na kuwapangua wanachama au viongozi waasisi wa chama hicho katika mazingira ya kidikteta, ili apate mwanya wa kukihodhi na kukiburuza kwa maslahi yake.

Alisema binafsi licha ya kuwa ni miongoni mwa waasisi wa Kamati Huru ya Mageuzi ya Kupigania  Demokrasia Zanzibar  (KAMAHURU), pia ni muasisi wa CUF na ndiye aliyekuwa mratibu mkuu wa usajili hadi chama hicho kupata usajili wa muda na wa kudumu.

"Kina Shaaban Khamis Mloo, Ali Haji Pandu, Masoud Omar na Dk Makamu Abdullah na wengine, tuliunda KAMAHURU wakati Maalim Seif akiwa kizuizini. Alitoka akakutaka tumeshajenga mazingira ya kisiasa, kama kosa letu kumkaribisha, sasa tunamfukuza,"alisema Kombo.

Aliongeza kuwa, CUF kwa mujibu wa katiba yake, itaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya atakayefanya shughuli zote za katibu mkuu hadi uchaguzi mkuu utakapoitishwa.

"Sipendi kutazama uso wa mtu, awe Profesa Lipumba au Maalim Seif na mwingine yeyote. Nimelelewa katika kuheshimu utaratibu na matakwa ya katiba. Maalim Seif amevunja na kukiuka katiba ili kustawisha udikteta ndani ya chama alichokaribishwa, hawezi kutung'oa ila atatoka yeye na kukiacha chama chetu,"alisisitiza

Kombo, ambaye alikuwa mkurugenzi wa oganaizesheni wa kwanza,  alisema CUF ilimpa Maalim Seif nafasi mara tano ili akiingize serikalini Zanzibar, lakini ameshindwa. Nafasi moja aliyopewa ya Makamu wa Kwanza wa Rais hakuonyesha uwezo wala uthubutu wa kubadilisha chochote, hivyo akubali kuwa ameshindwa.

Kwa upande wake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa kwanza wa CUF Zanzibar, Nassor Seif Amour, alisema Maalim Seif na wenzake wanajitia fedheha mbele ya macho ya dunia na jumuia ya kimataifa kwa kupitisha maamuzi, ambayo yako kinyume na Katiba ya CUF.

Amour alisema Seif na wenzake hawana mamlaka ya kumfukuza mwenyekiti, makamu mwenyekiti wala katibu mkuu, kwani vyeo hivyo mamlaka yake ni mkutano mkuu wa taifa na siyo vinginevyo, kama anavyofanya mwanasiasa huyo na kundi lake.

Mwasisi huyo, ambaye ni mtaalamu wa kompyuta na takwimu, alisema Seif amekuwa mwanasiasa mhamasishaji asiye na malengo ya kuonyesha wapi anakotaka kwenda na vipi anaweza kufika anakotarajia, huku akiamiani siku zote propaganda pekee ndiyo siasa bila mikakati.

"Baraza Kuu la CUF kwa mujibu wa katiba, halina nguvu ya kumfukuza mwenyekiti, makamu mwenyekiti wala katibu mkuu, ni mkutano mkuu wa taifa pekee na wakurugenzi kikatiba huteuliwa na mwenyekiti siyo katibu mkuu,"alisisitiza.

Amour alimtupia lawama Maalim Seif kwa kukikumbatia chama cha CHADEMA, huku akiwa na malengo ya kuua CUF kiaina na ushahidi wa madai hayo ni kikao chake akichofanya na wajumbe wa sekretarieti ya wilaya ya Mtwara, waliogoma kumpigia debe Edward Lowassa katika uchaguzi wa 2015.

"Maalim alikwenda Mtwara kuwashawishi  viongozi na wanachama wamchague Lowassa, akasutwa. Akaishiwa majibu na kujikuta akisema amepewa shilingi milioni tatu kila mkoa ili zisaidie kampeni za Lowassa, jambo linalodhihirisha alipewa fungu ili aidhoofishe CUF na wagombea wake,"alisema.

Pia, mwanasiasa huyo alieleza kuwa, kuna kila dalili katibu mkuu huyo ana mpango wa kukigawa chama hicho kwa maslahi yake kwani aliweza kukaa meza moja na UKAWA ili wagombea wa CUF wasichaguliwe.

No comments:

Post a Comment