Friday, 14 October 2016

UGONJWA WA MWALIMU NYERERE HADI KIFO CHAKE



BABA wa Taifa Mwalimu Nyerere, alifariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, mjini London, Uingereza. Tangu wakati huo, ni miaka 17 sasa imepita tangu Watanzania walipompoteza kipenzi wao huyo.

Kabla ya kuondoka kwenda London kwa matibabu hadi kifo chake, Watanzania walishikwa na hofu baada ya kupatikana habari kwamba, hali ya afya yake ilikuwa inatia shaka. Wakati huo alikuwa kijijini kwao Butiama.

Habari hizo zilipotolewa katika baadhi ya vyombo vya habari, haukupita muda zikakanushwa kwamba hazikuwa na ukweli wowote. Ilielezwa kwamba Mwalimu alikuwa akiendelea na shughuli zake za kilimo kama kawaida.

Hatimaye Mwalimu aliondoka nchini Agosti 31, 1999, kwenda London huku ikielezwa kuwa alikuwa akienda kufanyiwa uchunguzi wa afya yake. Kumbe ndio ilikuwa siku yake ya mwisho kukanyaga ardhi ya Tanzania, aliyoipigania na kuikomboa katika mikono ya wakoloni.

Tangu wakati huo, habari juu ya afya yake zilikuwa zikitolewa kwa siri huku zikieleza kuwa alikuwa anaendelea vyema na matibabu. Taarifa hizo zilieleza kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa akipatiwa matibabu akitokea kwenye makazi yake binafsi.

Hali iliendelea hivyo hadi Septemba 26, 1999, wakati Rais mstaafu Benjamin Mkapa alipolitangazia taifa na dunia kwa ujumla kwamba, hali ya Mwalimu Nyerere  haikuwa nzuri.

Katika maelezo yake, Rais Mkapa alisema madaktari wamegundua kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa na kansa ya damu, ugonjwa ambao huwakumba watu wenye umri mkubwa kama Nyerere. Wakati huo, Mwalimu Nyerere alikuwa na umri wa miaka 77.

"Nilimtembelea Mwalimu pale hospitali alikolazwa, hali yake si nzuri. Hazungumzi, ingawa anaelewa yote anayoelezwa,"alisema Mkapa na kuwaomba Watanzania kwa imani zao kumuombea ili aweze kupona.

Kufuatia rai ya kiongozi huyo wa nchi, mamia ya Watanzania kutoka madhehebu mbalimbali ya dini, walikusanyika katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, siku ya Septemba 27, 1999, kwa ajili ya kumuombea. Maombi hayo yaliendelea katika sehemu mbalimbali bila kuchoka hadi pale ilipotangazwa kwamba ameaga dunia.

Siku hiyo hiyo mke wa Mwalimu Nyerere, Mama Maria Nyerere na mabinti zake Anna na Rosemary, waliokuwa pamoja naye mjini London, walianza kuwa karibu naye kwa saa 24, huku Ikulu ikiendelea kutoa taarifa kwamba hali yake likuwa na nafuu kidogo.

Pamoja na hayo, serikali ilimtuma aliyekuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Kingunge Ngombale Mwiru, kwenda London, kusimamia utoaji wa taarifa zote zinazohusu ugonjwa na maendeleo ya hali ya Baba wa Taifa.

Siku hiyo hiyo, mwanasiasa mkongwe nchini, marehemu Rashid Kawawa, aliibuka na kusema amesikitishwa na kuzorota ghafla na kwa kasi kwa afya ya Mwalimu Nyerere na kumuombea apone haraka.

HOFU KUBWA YATANDA
Baada ya Rais Mkapa kutangaza kuwa hali ya Mwalimu si nzuri, zilikuwa zikitolewa taarifa mara kwa mara juu ya afya yake, zikieleza kwamba anaendelea vizuri. Lakini hali ilikuwa ya kusikitisha zaidi pale Ikulu ilipotoa taarifa Septemba 30, 1999, kwamba Mwalimu alikuwa akilishwa chakula kwa kutumia mipira, licha ya kuwa na nafuu.

Kabla ya hapo, ilielezwa kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa amepatwa na malaria na homa ya manjano, magonjwa ambao yalitokana na tatizo la kansa ya damu, ambayo ilisababisha kukosa kinga ya mwili. Lakini ilielezwa kuwa magonjwa hayo yalidhibitiwa baada ya muda mfupi.

Hofu zaidi iliwakumba wananchi Oktoba 2,1999, pale ilipoelezwa kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa akipumua kwa msaada wa mashine na kwamba hawezi kuzungumza. Hapo kila mtu alianza kuzungumza kwa namna yake na kuonyesha dalili za kukata tamaa.

Mbali na habari hiyo iliyotolewa na Ikulu, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Profesa Abdelkadeer Shareef, alisema Mwalimu katika kipindi hicho alikuwa amezidiwa kiasi cha kushindwa hata kuyatambua mazingira.

Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo yenye kutia shaka, ndipo Ikulu ilipoamua kutoa taarifa za mara kwa mara kwenye vyombo vya habari kadri zilivyokuwa zikipatikana.

Mambo yalizidi kuwa magumu zaidi juu ya afya ya Mwalimu Nyerere baada ya Oktoba 11, 1999, ilipoelezwa kwamba alikuwa amepoteza fahamu. Taarifa hiyo ilieleza kuwa, madaktari walikuwa wakijiandaa kuuchunguza ubongo wake ili kujua sababu zilizomfanya kufikia hatua hiyo.

Siku iliyofuata, kila Mtanzania alikata tamaa zaidi pale ilipobainika kuwa, Mwalimu Nyerere hajaamka kwa siku nne mfululizo, licha ya kupumua kwa kutumia mashine na figo zake kuimarika kwa kiasi fulani.

Hali hiyo ilimfanya mmoja wa watoto wake, Makongoro Nyerere, kusema wazi alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba Watanzania wajiandae kwa msiba.

Kauli hiyo ya Makongoro, ambaye ndiye aliyefuata nyayo za baba yake katika medani ya siasa, iliwafanya Watanzania kuamini kuwa Nyerere ameshafariki dunia.

Baada ya kauli hiyo ya Makongoro,ilielezwa kuwa matumaini ya Mwalimu Nyerere kupona yalikuwa madogo na kwamba, hatima yake ilikuwa mikononi mwa familia yake, kuamua kama aendelee kupumua kwa kutumia mashine au la.

Siku iliyofuata ilielezwa wazi kuwa, Mwalimu Nyerere asingeweza kupona baada ya kukumbwa na kiharusi kikali.

MSIBA MZITO
Hatimaye ilipofika Oktoba 14, 1999, Rais Mkapa aliutangazia umma kupitia vyombo vya habari kwamba, Mwalimu Nyerere aliaga dunia saa 4.30 asubuhi, kwa saa za Afrika Mashariki.

"Kwa majonzi makubwa, nasikitika kuwatangazia kwamba mpendwa wetu, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, amefariki dunia,"alisema Rais Mkapa, akiwa pamoja na Makamu wa Rais wa wakati huo, Dk. Omar Ali Juma (marehemu) na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.

Taarifa hizo, ambazo Watanzania walizipata wakiwa katika maeneo mbalimbali, zililifanya Taifa kuzizima kwa majonzi, simanzi na vilio kila mahali.

Baada ya hapo, mipango iliandaliwa kwa ajili ya kuurejesha mwili wake nchini kwa ajili ya mazishi. Kamati ya mazishi ikiongozwa na Sumaye, iliundwa na kwenda kuufuata mwili wa Mwalimu Nyerere nchini Uingereza kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), ikiwa na jopo la marubani, wakiongozwa na Kepteni Anderson Wililo.

Wakati mwili huo ulipotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam, taifa liliendelea kuzizima kwa vilio vya kila aina, kuonyesha uchungu waliokuwa nao Watanzania kwa kuondokewa na kiongozi wao huyo.

Mizinga 21 ilipigwa uwanjani hapo, ikiwa ni ishara ya heshima kwa kiongozi huyo na hatimaye mwili wake kubebwa kwenye gari maalumu, hadi nyumbani kwake, Msasani, Dar es Salaam.

Kabla ya kufikishwa Msasani, jeneza lililobeba mwili wa Mwalimu Nyerere lilipitishwa katika barabara za Pugu (sasa Nyerere), Nelson Mandela hadi Ubungo, Morogoro, Magomeni Mapipa, Kawawa, Ali Hassan Mwinyi, Maji Machafu, TPDC Mikocheni hadi Msasani.

Oktoba 21, 1999, mwili huo uliagwa na umma wa Watanzania uli0kusanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kwa siku kadhaa kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho na baadaye kusafirishwa kwenda Butiama, Musoma kwa maziko.

Wakati wa kuuaga mwili huo, maelfu ya Watanzania walionekana wakibubujikwa na machozi, wakiwa hawaamini endapo huo ulikuwa mwisho wa kumuona tena mahali popote, Mwalimu Nyerere.

Wengi walibubujikwa na machozi baada ya ndege iliyokuwa imeubeba mwili wake kuruka uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, kuanza safari ya kwenda Musoma, ambako ulipokewa kijeshi kabla ya kupelekwa kijijini kwake Butiama.

No comments:

Post a Comment