Tuesday 26 July 2016

FURAHA, HOI HOI, NDEREMO VYATAWALA KWA WAJUMBE



HOI HOI, furaha na nderemo jana vilitawala kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Center (DCC), wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipofanya mkutano wake mkuu maalumu wa kumchagua mwenyekiti mpya.

Mkutano huo, ulioanza saa 4.45 asubuhi, ulihudhuriwa na wajumbe 2,398, kati ya wajumbe halali 2,412, sawa na asilimia 99.4.

Wajumbe wa mkutano huo walianza kuingia ukumbini saa mbili asubuhi huku kikundi cha sanaa za maonyesho cha Tanzania One Theatre (TOT), kikitoa burudani ya nyimbo za kwaya na taarab.

Mwenyekiti wa CCM, Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliingia ukumbini saa 3.34 asubuhi na kuufanya ukumbi kuripuka kwa shangwe na nderemo.

Kikwete aliongozana na Makamu Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula na Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein na Katibu Mkuu,
Abdulrahman Kinana na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli.

Baada ya viongozi hao kuingia ukumbini, kikundi cha TOT kiliimba wimbo maalumu wa kumuaga Mwenyekiti mstaafu Kikwete na kuwafanya wajumbe wapunge bendera hewani huku wakitikisa vichwa na miili yao kufuatisha mapigo ya wimbo.

Kibao hicho kinachojulikana kwa jina la Jakaya Nenda, kinaelezea kazi mbalimbali kubwa na nzuri zilizofanywa na Rais mstaafu Kikwete wakati wa uongozi wake, ikiwa ni pamoja na kumtakia mapumziko mema.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wastaafu wa Chama na serikali, wakiwemo Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume.

Viongozi wengine wastaafu waliohudhuria mkutano huo ni mawaziri wakuu wa zamani, Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba, Cleopa Msuya na Mizengo Pinda, ambao wakati wakitambulishwa, walishangiliwa kwa mayowe mengi na wajumbe.

Wengine ni Makamu wa Rais mstaafu Dk. Mohamed Gharib Bilal, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Aidha, vyama 12 vya siasa vyenye usajili wa kudumu navyo vilihudhuria mkutano huo, sanjari na mabalozi kutoka nchi 39. Vyama hivyo ni Chauma, TLP, UDP, ADC, UND, JAHAZI ASILIA, CCK, SAU na AFP.

Wakati Rais Dk. John Magufuli akitambuliwa, ukumbi ulilipuka mayowe ya kushangilia huku wajumbe wengi wakiwa wamesimama vitini na kupunga bendera hewani, ikiwa ni ishara ya kuvutiwa na uchapa kazi wake.

No comments:

Post a Comment