Tuesday 26 July 2016

SIKUNG'ANG'ANIA UENYEKITI WA CCM-KIKWETE


MWENYEKITI mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amesema kamwe hakuwa na mpango wa kuendelea kung'ang'ania nafasi ya uenyekiti wa Chama, kama ilivyokuwa ikiriporiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Kikwete amesema yeye ndiye aliyetaka kumkabidhi mapema wadhifa huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kwa lengo la kuendeleza utamaduni uliodumu kwa miaka mingi ndani ya CCM wa kubadilishana uongozi kwa njia ya amani na usalama.

Amesema yapo baadhi ya magazeti yaliyoandika habari zinazofanana kuhusu uzushi huo, yakiwa yamegeuza ukweli wa mambo na kudai kwamba, hataki kukikabidhi Chama kwa Rais Magufuli.

"Magazeti haya yalitaka kunihukumu kwa uongo wao. Najua hawataacha kwa sababu wanao mtambo mahsusi wa kuzua uongo. Kila siku wanazua jambo jipya. Lengo lao ni kuchochea mfarakano ndani ya CCM. Inawauma moyo kuona Chama kikibaki kuwa na umoja. Wanasikitika kuona jitihada zao hazijafanikiwa,"alisema Kikwete.

Amesema vyombo hivyo vya habari vimekuwa vikiandika habari nyingi za uongo, uzushi, uchonganishi na ufitini kwa lengo la kukivuruga Chama, lakini kamwe jitihada hizo hazitaweza kufanikiwa.

Rais mstaafu Kikwete alisema hayo jana, alipokuwa akifungua mkutano mkuu maalumu wa CCM, uliofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Center, ulioko nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Alisema kazi ya kumshawishi Rais Magufuli akubali kupokea uenyekiti wa CCM, aliianza Februari, mwaka huu, lakini haikuwa rahisi na alilazimika kuwatumia Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, ndipo  akakubali.

Kikwete alisema alipomfuata Rais Magufuli kwa mara ya kwanza na kumueleza jambo hilo, alimjibu kwamba hakuwa na haraka kwa vile ana mambo mengi ya kufanya serikalini.

"Niliendelea kumshawishi kwa kutumia ufundi wangu wote, lakini hakukubali. Nikamsimulia Makamu Mwenyekiti Mzee Mangula na Kinana na kuwaomba wajaribu kumshawishi. Baada ya miezi mitatu, Mangula alirejea na majibu kwamba amekubali,"alisema.

Alisema baada ya Rais Magufuli kukubali kupokea wadhifa huo, aliwasilisha taarifa ya kutaka kustaafu kwenye Kamati Kuu ya CCM na kikao hicho kikapanga makabidhiano hayo yafanyike jana, kupitia mkutano mkuu maalumu.

Rais mstaafu Kikwete alisema majibu yaliyotolewa na Rais Magufuli kukataa kupokea wadhifa huo mapema, hayakumshangaza kwa sababu hata naye aliwahi kuyatoa wakati alipoombwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa apokee wadhifa huo.

Aliwataka wana-CCM kuendelea kuwa wamoja ili jitihada hizo za wapinzani zisiweze kufanikiwa na kuongeza kuwa, Chama kimekuwa kikijivunia kuwa na hazina ya viongozi wastaafu na wenye hekima, ambapo wameweza kukifikisha hapa kilipo.

Alisema kubadilishana nafasi ya uenyekiti ngazi ya Taifa ni utamaduni uliodumu ndani ya CCM kwa miaka mingi na ni budi udumishwe kwa manufaa ya Chama na serikali.

"Wazee walipoamua kuanzisha utamaduni huu, waliona mbali. Sikutaka mguu wangu uote tende," alisisitiza.

Alisema siku ya jana ilikuwa ya kihistoria katika maisha yake kwa sababu ilihitimisha safari yake ya miaka zaidi ya 40 na kukitumikia Chama katika ngazi mbalimbali.

"Leo ni zamu yangu. Namkabidhi uongozi mwenyekiti wa awamu ya tano. Raha iliyoje. Raha sana. Nani kama CCM?" Alisema Kikwete huku akishangiliwa kwa mayowe na wajumbe waliojibu kwamba hakuna.

"Baada ya miaka yote hiyo, kustaafu ni jambi linalostahili. Nitaendelea kuwa mwanachama wa CCM katika tawi la  Msoga na nitaendelea kutoa mchango wangu na kuhudhuria kwenye vikao mbalimbali nitakavyoalikwa,"alisema.

        AWASHUKURU MWINYI NA MKAPA

Rais mstaafu Kikwete alitoa shukurani za pekee kwa Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa kwa kumuamini na kumteua kushikilia nyadhifa mbalimbali serikalini wakati wa utawala wao.

Alimwelezea Mzee Mwinyi kuwa ndiye kiongozi wa kwanza serikalini aliyemuamini na kumfanya ajulikane kwa Watanzania wote kwa kumteua kuwua Naibu Waziri wa Nishati na Madini mwaka 1988 na baadaye kumpandisha cheo na kuwa waziri kamili kabla ya kumpandisha cheo na kumteua kuwa Waziri wa Fedha.

"Kama sio wewe Mzee Mwinyi, nisingefika hapa nilipo. Pengine ningeendelea kuhamishiwa kwenye vituo mbalimbali vya Chama,"alisema.

Aidha, alimwelezea Mzee Mkapa kuwa naye alimwamini na kumkabidhi dhamana nzito ya kuongoza diplomasia ya Tanzania kwa miaka 10 kwa kumteua kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kumfanya apate nafasi ya kuijua dunia, kuwajua watu mbalimbali na pia watu wengi kumjua.

"Sina cha kuwapa kutokana na hisani kubwa mliyonifanyia maishani mwangu. Mtalipwa na Mwenyezi Mungu,"alisema.

Akielezea historia yake ya uongozi ndani ya Chama, Kikwete alisema ilianza mwaka 1975, alipoteuliwa kuwa Katibu Msaidizi wa TANU mkoani Singida na kuendelea kukitumikia katika mikoa ya Tabora, Lindi na baadaye Zanzibar, ambako alipewa jukumu la kuboresha mfumo wa uongozi ndani ya Chama visiwani humo.

Makamu Mwenyekiti mstaafu pia aliwashukuru makamu wenyeviti wastaafu wa CCM, Dk. Amani Abeid Karume, Dk. Ali Mohamed Shein na John Malecela kwa kuwa wasaidizi wake wazuri na makini katika shughuli za Chama.

Aliwataja viongozi wengine waliomsaidia na kumuamini kuwa ni Katibu Mtendaji wa kwanza wa TANU, marehemu John Mhavile, Pius Msekwa, Joseph Butiku, Salmini Amour, Kanali Ayubu Simba.

Aidha, alitoa shukurani za pekee kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere na Makamu wa Rais mstaafu, marehemu Rashid Kawawa kwa kuwa wazazi wazuri kwake, kumlea, kumuongoza, kumuamini na kumpa fursa mbalimbali za uongozi.

Kikwete pia alitoa shukurani za pekee kwa Makamu Mwenyekiti Bara, Mangula kwa kuwa msaidizi mzuri aliyesimamia vyema nidhamu, maadini na udhibiti wa mambo mbalimbali ndani ya Chama.

Pia alitoa shukurani za pekee kwa makatibu wakuu watatu wa CCM aliofanyanao kazi katika kipindi cha miaka 10, Yusuph Makamba, Wilson Mukama na Abdulrahman Kinana kwa msaada mkubwa waliompatia wakati wa uongozi wake.

            AMFAGILIA KINANA
Alimwelezea Kinana kuwa ni jembe la kazi na la nguvu na kwamba, amekuwa akifanya kazi kubwa na nzuri na isiyo na mfano wake na kuleta mtazamo chanya ndani ya Chama.

"Kwa mikakati, ubunifu, mipango yenye tija, alitembelea mikoa yote, wilaya zote na majimbo yote. Alikutana na kuzungumza na wananchi. Alishirikiana nao katika ujenzi wa shule, alilima nao na kusikiliza shida za wananchi.

"Aliwafanya wananchi waendelee kuwa na matumaini na CCM na kuwakatisha tamaa wapinzani. Ushindi tulioupata katika uchaguzi mkuu mwaka jana, huweza kuacha kuona na kutambua mchango

"Hawa wote walikuwa wasaidizi wazuri ndani ya CCM na bila msaada wao, mambo yangekuwa magumu,"alisema.

"Ukiwa na makamu wawili wazuri, unachotakiwa kufanya ni uwezeshaji. Mambo yatakuendea vizuri na utafanya kazi zao vizuri. Utaongoza Chama na serikali bila kikwazo. CCM hakuna mafaili mengi. Wakati wa uongozi wangu, mafaili yote yalikuwa kwa Kinana,"aliongeza.

Kikwete aliwataka wana-CCM kuendelea kukijenga Chama na kukiimarisha, ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wa dhati kwa mwenyekiti mpya, Rais Magufuli.

        MASLAHI YA WATUMISHI CCM
Aliwapongeza watumishi wote wa CCM kwa kuonyesha upendo kwa Chama, licha ya kulipwa ujira mdogo kutokana na kutokuwa na posho. Alisema watumishi hao wamekuwa wakichapakazi usiku na mchana kwa moyo wa kujitolea, unaostahili kupongezwa.

Alisema chini ya uongozi wake, alijitahidi kuboresha maslahi, lakini walishindwa kuuendeleza utaratibu huo kutokana na matatizo mbalimbali, hivyo alimtaka mwenyekiti mpya kulitupia jicho suala hilo.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo kumpigia kura zote za ndio Rais Magufuli ili awe mwenyekiti mpya wa CCM na kuwataka wahakikishe wasipoteze kura hata moja.

"Atakayepiga kura ya hapana, huyo ni mchawi na wachawi hawapo CCM,"alisema Kikwete huku akishangiliwa kwa mayowe mengi na wajumbe.

Alimwelezea Rais Magufuli kuwa ni mzoefu katika uongozi wa Chama kwa kuwa amewahi kuwa mjumbe wa kamati mbalimbali katika ngazi za wilaya na mkoa na kwamba, hana wasiwasi naye.

"Naamini Chama kipo salama chini ya Rais Magufuli. Namuamini kwa sababu ni mtu anayependa kuendesha mambo yake kwa kasi.

"CCM ipo imara, bado ipo madarakani. Naipenda CCM na nitaendelea kuipenda," alihitimisha hotuba yake Mwenyekiti mstaafu Kikwete.

No comments:

Post a Comment