Thursday 21 July 2016

SIKUWAHI KUPINGA UTEUZI WA DK. MAGUFULI

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, amekanusha madai kuwa, alikuwa miongoni mwa wana-CCM waliopinga uteuzi wa Dk. John Magufuli, kugombea urais mwaka jana, kupitia chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Alhaji Kimbisa alisema kilichojitokeza ni mabishano kuhusu utaratibu wa kupata majina matano na matatu kwa ajili ya kupigiwa kura na wajumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu wa CCM.

“Watu watakuwa walinielewa tofauti. Mimi sikuwa mmoja na wala sikuthubutu kupinga uteuzi wa Dk. Magufuli. Maneno ya kwenye vyombo vya habari ni porojo za kuuzia magazeti tu ili waingize pesa,” alisema.

Alisema binafsi anaridhishwa na kufurahishwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli na kusisitiza kuwa, baada ya kupitishwa na CCM, hakuna aliyeweza kupinga uteuzi huo kwa vile ulifanyika kihalali na kwa kufuata taratibu za Chama.

"Mchakati uliokuwepo wakati ule ni wa kumpata mgombea ambaye atakivusha Chama katika uchaguzi mkuu na pia kurejesha nidhamu kwa viongozi na wanachama.

Akizungumzia maandalizi ya mkutano mkuu wa CCM, unaotarajiwa kufanyika keshokutwa mjini hapa, Alhaji Kimbisa alisema Chama kinao utaratibu mzuri kwa viongozi wa nafasi ya mwenyekiti kupokezana vijiti.

Alisema anaamini mara baada ya Rais Magufuli kukabidhiwa jukumu hilo, viongozi na wanachama wa CCM hawataishi na kufanya kazi kwa mazoezi kwa vile watalazimika kwenda na kasi yake na kufuata kauli mbiu ya 'Hapa Kazi Tu'.

Alhaji Kimbisa alisema kutokana na ukongwe wa Chama na pia kukabiliwa na majukumu mazito, kinahitaji mwenyekiti wa aina ya Rais Magufuli ili aweze kukisafisha na kukiimarisha.

Alisema tayari Rais Magufuli ameshaonyesha uwezo mkubwa wa kiutendaji katika serikali, hivyo anaamini baada ya kukabidhiwa kofia ya mwenyekiti wa CCM, hali pia itabadilika ndani ya Chama.

Akizungumzia uwepo wa makundi ndani ya Chama, alisema kwa sasa CCM haina makundi na kwamba yale yaliyojitokeza mwaka jana, ilikuwa ni kwa sababu ya uchaguzi mkuu. Aliongeza kuwa makundi hayo yalishavunjwa na kwa sasa CCM ni moja.

Aliwataka wananchi kutofautisha porojo za vyombo vya habari na hali halisi iliyoko sasa ndani ya Chama.

“Ukifanya uchunguzi wa kina utagundua kuwa CCM haina makundi na hizo zinazosemwa ni porojo tu za kuuzia magazeti. Msipoandika porojo na mambo yanayosisimua, mtafanyaje biashara? Hatuwezi kuwazuia kufanya hivyo, lakini ukweli ni kwamba ndani ya CCM hakuna makundi,”alisema.

Alisema unapofika wakati wa uteuzi wa mgombea urais ndani ya chama chochote cha siasa, lazima wanasiasa wagawanyike na kwamba, ambaye hatakuwa na kundi huyo ni mwanasiasa mfu.

Kimbisa alisema kwa wakati huu, ambapo chama kinaelekea katika mkutano mkuu maalumu wa kumchagua mwenyekiti mpya, CCM ni moja na hakuna makundi wala mgawanyiko.

Alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wajumbe wa mkutano mkuu na wana-CCM mjini Dodoma, huku akiwahakikishia kuwa hali ya mkoa ni shwari na kuna usalama na ulinzi wa kutosha.

Alimuhakikishia Rais Magufuli kwamba, wajumbe wa mkutano huo kutoka Dodoma, watapiga kura zote za ndio ili aweze kukabidhiwa jukumu la kukiongoza Chama.

No comments:

Post a Comment