Thursday, 21 July 2016

KINANA AWACHANA WAPINZANI

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema vyama vya upinzani nchini vimejijenga kiuanaharakati zaidi na vimekuwa vikijipatia umaarufu kwa njia ya vituko na matukio ya ajabu.

Amesema vyama hivyo havijajikita kwenye sera na kuwaeleza wananchi watawafanyia nini, ndio sababu vimepoteza mwelekeo kwa kuwa mambo vinayofanya hayawapi matumaini yoyote Watanzania.

Aidha, Kinana amesema uamuzi wa wabunge wa upinzani, wanaounda kundi la UKAWA, kususia vikao vya bunge vinavyoendeshwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Acskon ni wa kukurupuka kwa vile haupo kwenye kanuni na taratibu za bunge.

Kinana alisema hayo wiki hii, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa Uhuru, ofisini kwake mjini hapa.

"Kazi yao siku zote ni kukisema vibaya chama na serikali. Kila kukicha wanalaumu, kushutumu, kukejeli na wakati mwingine bila haya wanatukana. Huo ni mtaji wa muda mfupi sana,"alisema Kinana.

Katibu Mkuu huyo wa CCM, anayetarajia kustaafu mwishoni mwa wiki hii, alisema hali hiyo ndio iliyowafanya Watanzania wapime kauli, tabia na vitendo vya CCM na wapinzani, na kuamua kuichagua CCM, kwa sababu sera zake zinatekelezeka na kauli na vitendo vya viongozi wake vinaaminika zaidi.

Kinana, ambaye staili yake ya uongozi imekuwa kivutio kikubwa kwa wanachama wa CCM pamoja na wananchi, alisema kutokana na utendaji madhubuti wa Rais Dk. John Magufuli, wananchi wataendelea kuipenda na kuiamini zaidi CCM na kuendelea kuichagua katika uchaguzi mbalimbali.

Akizungumzia uamuzi wa wabunge wa upinzani kususia vikao vya bunge, Kinana alisema wanayo haki ya kuchukua uamuzi wowote wanaoona unafaa, lakini wapo baadhi yao wanatamani kurudi, lakini hawajui watarudi vipi.

Alisema Naibu Spika Dk. Tulia alichaguliwa na wabunge wote, wakiwemo wa upinzani, hivyo anapaswa kuheshimiwa na kwamba, bunge linapaswa kuendeshwa kwa kanuni, taratibu na mila.

"Duniani kote, spika na naibu spika ni viongozi wa kuheshimika. Mgogoro uliozuka bungeni umetokana na ukiukwani wa kanuni na wabunge wa upinzani kushindwa kufuata kanuni na maelekezo ya naibu spika.

"Hiyo ni dharau isiyostahili. Wabunge wanapaswa kusikiliza na kuzingatia maelekezo ya spika. Kama hawakuridhika, wanayo fursa ya kulalamika kwa kamati husika.

"Kususia bunge haimo kwenye kanuni. Nawashauri warudi bungeni, wawasilishe malalamiko yao  kwenye kamati husika ili hatua zichukuliwe," alisema na kusisitiza Kinana.

Alisema kitendo cha wabunge wa upinzani kususia vikao vya bunge ni kuwaonea wananchi waliowachagua na kuwakosesha fursa ya kuwasilisha hoja zao na pia kuwatetea bungeni.

No comments:

Post a Comment