Wednesday 20 July 2016

KINANA: WALIOKISALITI CHAMA WANAENDELEA KUSHUGHULIKIWA

CHAMA  Cha Mapinduzi (CCM), kimesema viongozi wa ngazi za juu walioshiriki kukisaliti Chama katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, watachukuliwa hatua kadri ya makosa yao na kwa kadri ya vikao husika vitakavyoamua.

Kimesema tathmini ya awali iliyofanywa na Chama katika ngazi mbalimbali, imeshawatambua na kuwabaini viongozi na wanachama wote wenye kasoro, vikao vimewajadili na wapo waliochukuliwa hatua katika ngazi za chini.

Hayo yalisemwa juzi na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katika mahojiano maalumu na Uhuru, ofisini kwake mjini hapa.

Amesema Kamati Kuu ya CCM ilishatoa agizo katika ngazi zote za uongozi, ifanywe tathmini ya uchaguzi mkuu, ambapo ilidhihirika wana-CCM wengi na viongozi ni wazuri na walitumika vizuri na kwamba bila wao, ushindi usingepatikana.

"Pia wapo ambao ama hawakutimiza wajibu au kukisaliti chama na tathmini imeshawatambua wote wenye kasoro, vikao vimewajadili na wapo waliochukuliwa hatua katika ngazi za chini,"alisema.

"Wale wa ngazi za juu watajadiliwa na watachukuliwa hatua kadri ya makosa yao na kadri vikao vitakavyoamua,"aliongeza.

Katika hatua nyingine, Kinana amesema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, imeleta matumaini mapya na kujibu matakwa yote ya Watanzania.

Amesema kwa miaka mingi wananchi walikuwa wakililia nidhamu, uwajibikaji na ufanisi kwa watumishi wa serikali, mambo ambayo serikali ya Rais Magufuli imeweza kuyafanya katika kipindi kifupi.

Kinana amesema kilio kingine kikubwa cha wananchi kilikuwa kupunguza matumizi ya serikali, kukabiliana na mmomonyoko wa maadili, kupambana na rushwa katika ngazi zote na uwajibikaji serikalini katika kila sekta na kwamba mambo yote hayo yameshaanza kushughulikiwa na kuzaa matunda.

"Serikali imeongeza kasi kubwa katika kushughulikia matatizo ya wananchi, inatekeleza vyema Ilani ya Uchaguzi na kuwaletea maendeleo wananchi.

"Rais Magufuli ametujengea utamaduni mpya kwamba cheo ni dhamana na kipo kwa maslahi ya wananchi, sio maslahi binafsi,"amesema Kinana.

Amesema tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani mwaka jana, kila mtanzania amekuwa akishiriki kuchangia maendeleo kwa kulipa kodi na kwamba kila mtu anaridhishwa na utendaji wake wa kazi.

"Hayo yote anayoyatekeleza, yamo kwenye Ilani ya Uchaguzi na ni maamuzi yaliyofikiwa katika mkutano mkuu wa CCM. Kama viongozi walio madarakani wakimsikiliza na kutekeleza maagizo yake, wananchi wataendelea kumuunga mkono," alisema

Aidha, Kinana amesema uamuzi wa Rais Magufuli kuwaamini na kuwapa vijana nafasi mbalimbali za uongozi serikalini ni mzuri na unastahili kupongezwa na kuendelezwa.

Amesema kwa sasa taifa linao vijana wengi wasomi, wenye uwezo, nguvu ya kufanya kazi na mapenzi ya kulitumikia taifa lao, hivyo ni lazima waaminiwe na kupewa nafasi za uongozi.

"Hawa ni vijana wa taifa la leo, sio la kesho. Wana uwezo wa kuchacharika katika mazingira ya kila aina na kufanya kazi bila kuchoka. Ni muhimu wapewe nafasi. Naamini watatoa mchango mkubwa katika kuleta maendeleo kwa Watanzania,"amesema.

Hata hivyo, Kinana ameonya kuwa iwapo kwa bahati mbaya watafanya makosa katika uongozi wao, wanapaswa kuelekezwa, kuwasaidia na kuwalea badala ya kuwaadhibu.

"Wakiwa jasiri na kuamua au kwa bahati mbaya wakakosea, tuwaelekeze, tuwalee, tuwasaidie, tusiharakishe kuwaadhibu kwa sababu kufanya kosa ni sehemu ya kazi,"amesema.

No comments:

Post a Comment