CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema makamu wenyeviti wawili wa chama hicho, Philip Mangula (Bara) na Dk. Ali Mohamed Shein (Z'bar), wataendelea na nyadhifa zao hadi Novemba, 2017.
Ufafanuzi huo ulitolewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alipokuwa akisoma ajenda za mkutano mkuu maalumu, uliofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Center mjini hapa.
Kinana alisema kwa mujibu wa kifungu cha 7 Ibara ya 105 kifungu kidogo cha 5 (a) cha Katiba ya CCM, utakapofika wakati wa uchaguzi, mkutano mkuu utamchagua mwenyekiti na makamu wenyeviti wawili kutoka Bara na Zanzibar.
Hata hivyo, alisema kutokana na utamaduni wa wenyeviti kupokezana uongozi, uchaguzi unaofanyika ni wa mwenyekiti pekee wakati makamu wenyeviti wawili wanaendelea na nafasi zao hadi wakati wa uchaguzi mkuu.
Kinana alisema kwa kuwa mkutano huo ni kwa ajili ya kumchagua mwenyekiti pekee, hawana sababu ya kufanya uchaguzi wa makamu wenyeviti wawili, hivyo wataendelea na nyadhifa zao hadi Novemba, 2017, watakapomaliza muda wao wa uongozi.
Kinana alisema utamaduni wa wenyeviti wa CCM kupokezana uongozi, haupo kwenye katiba na kanuni, bali ulianzishwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na kuendelezwa na viongozi waliofuata.
Alisema lengo la utaratibu huo ni kuleta mshikamano ndani ya Chama kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Kwa mujibu wa Kinana, Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete alielezea dhamira ya kung'atuka kwenye nafasi hiyo tangu mwaka jana, wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 38 ya CCM, zilizofanyika mkoani Singida.
Alisema baada ya Kikwete kuandika barua ya kuomba kustaafu, kiliitishwa kikao cha Kamati Kuu, ambacho kiliridhia uamuzi wake huo na kumteua Rais Dk. John Magufuli kuwa mgombea wa nafasi hiyo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 2,398, sawa na asilimia 99.4, kutoka mikoa yote ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment