Tuesday, 26 July 2016

KIMBISA: KIKWETE AMEKITUNZA CHAMA KWA UANGALIFU

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, amemwelezea Makamu Mwenyekiti mstaafu Taifa, Jakaya Kikwete kuwa ni kiongozi aliyekitunza Chama kwa uangalifu mkubwa.

Kimbisa amesema Kikwete alikitunza Chama kama mboni ya jicho lake ndio sababu kipo imara licha ya kukumbwa na misukosuko mingi na kwamba kitazidi kuwa imara.

Alisema hayo jana, wakati akitoa salamu za mkoa wa Dodoma, kwa wajumbe wa mkutano mkuu mkuu maalumu wa CCM, uliofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Convention Center mjini hapa.

Kimbisa, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alisema Kikwete alifanya hivyo kutokana na kutambua thamani ya Tanzania chini ya Chama tawala.

Alisema vyama vingi vya siasa barani Afrika, vimekuwa vikikorogana sio kwa sababu ya wanachama, bali viongozi wenye uchu, tamaa ya madaraka na kuviweka vyama hivyo kwenye mifuko yao kwa misingi ya ukabila, dini na ukoo.

"Chini ya uongozi wako, hatukuona chama kikienda Chalinze, haukukifanya kiwe mali yao, ukiona vinaelea ujue vimeundwa,"alisema Kimbisa.

"Katika maisha yako kama mwenyekiti, umekitunza chama kwa muda mrefu na kukifanya kiwe imara. Ulianza kazi ndani ya chama ukiwa katibu msaidizi wa TANU, mjumbe wa Halmashauri Kuu na baadaye mwenyekiti.

Kimbisa alisema mkoa wa Dodoma umepata bahati pekee ya kuwa makao makuu ya CCM na uliongoza kwa wingi wa kura katika mikoa yote ya Tanzania, wakati wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani, uliofanyika mwaka jana.

Alisema katika uchaguzi huo, mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Dodoma na mweka hazina wake waligombea nafasi za udiwani na ubunge, lakini walijikuta wakitandikwa bakora na wagombea wa CCM.

Aidha, alisema katika kudhihirisha kuwa mkoa wa Dodoma ni ngome imara ya CCM, ulishinda majimbo yote ya uchaguzi na kuwaacha  wagombea wa vyama vya upinzani wakitoka kapa.

Kimbisa pia alitumia fursa hiyo kumuombea kura Mwenyekiti mpya wa CCM, kwa kusema katika kipindi kifupi tangu alipochaguliwa kuwa rais, amefanya mambo mengi makubwa na kuonyesha dira kwamba, Chama kitashinda tena kwa kishindo katika uchaguzi wa 2020.

Alisema katika kipindi hicho kifupi, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli imeweza kukusanya kodi kwa wingi na kuwashughulikia mafisadi, mambo ambayo yamewafanya wananchi warejeshe imani kwa CCM.

No comments:

Post a Comment